http://www.swahilihub.com/image/view/-/3302742/medRes/1385251/-/hxfax2z/-/SnMwaura2606as%25282%2529.jpg

 

Isaac Mwaura asema zeruzeru wa Kenya hawatambuliwi rasmi

Isaac Mwaura

Mbunge maalumu Isaac Mwaura kwenye mahojiano awali. Picha/JEFF ANGOTE 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, June 15  2017 at  07:27

Kwa Mukhtasari

Zeruzeru hapa nchini wameitaka serikali itilie mkazo sheria za 2014 ambazo zilitoa shinikizo za kibajeti kuwa masilahi yao muhimu yawe yakichungwa kupitia bajeti ya kitaifa.

 

ZERUZERU hapa nchini wameitaka serikali itilie mkazo sheria za 2014 ambazo zilitoa shinikizo za kibajeti kuwa masilahi yao muhimu yawe yakichungwa kupitia bajeti ya kitaifa.

Wamesema kuwa kinyume na hali hiyo ya kisheria, wengi wao wamekuwa wakinyimwa haki zao za kibinadamu, kijamii na kiuchumi kiasi cha kubaguliwa kama waathiriwa wa uchawi au laana.

Katika Kaunti ya Embu ambapo muungano huo ulitua Jumanne kuadhimisha siku yao hapa nchini, mwenyekiti wao Isaac Mwaura na ambaye ni mbunge maalum
alisema kuwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta licha ya kukumbwa na changamoto tele za kiuchumi imekuwa ikijizatiti kuwatimizia matakwa yao, "ila tu kuna dosari hapa na pale."

Ni katika hali hiyo ambapo Mwaura alishirikisha kampeni za kitaifa za kuhamasisha kuhusu haki za zeruzeru chini ya mwito; "Niko Na Haki."

Anateta kuwa wenzake wamekuwa wakitekelezewa njama hata za ufisadi ambapo rasilimali zao hufujwa na wasimamizi wa hazina za ‘walemavu.’

“Tunalenga kuhamasisha wananchi kuwa sisi sio tofauti na wao kwa kuwa sote ni binadamu. Tuko na haki zetu na kwa kuwa sisi hatuna historia
ya kubagua wengine tunaoishi nao, hata sisi tunaomba tusibaguliwe,” alisema Mwaura.

Alisema kuwa kinyume na dhana inayoshamiri hapa nchini kijamii, zeruzeru ni binadamu wa kawaida na aliye na nafasi sawa na jamii ya binadamu wengine.

Kwa mujibu wa Mwaura, changamoto ambazo wao hukumbana nazo katika maisha ni pamoja na kulengwa na wauaji wanaosaka viungo vya binadamu ili kuviuza kwa washirikina.

Changamoto za kimaisha

Alisema kuwa kuna kasumba potovu kuwa viungo vyao viko na thamani kubwa katika soko haramu la ushirikina na huwa vinatumiwa kama malighafi ya dawa ya
waganga na ushirikina ya kutibu kila hali ya changamoto za kimaisha.

Alisema kuwa maumbile yao huchukuliwa na wengine kama ugonjwa hatari unaoweza kuambukizanwa kupitia salamu za mikono, busu au kulala pamoja hivyo basi kujipata wakitengwa kwa njia zinazozua chuki.

Madaktari wanashikilia kuwa hali ya uzeruzeru sio tukio lisilo la kawaida katika Sayansi ya matibabu kwa kuwa wao ni viumbe sawa bin sawa na wengine ila tu ngozi, nywele na macho yao hukosa chembechembe muhimu ijulikanayo kama melanin hivyo basi kuwapa rangi ya ‘uzungu’ wa lazima.

Katibu mkuu wa muungano huo Francis Munyiri alisema kuwa "kuwa na upungufu wa chembechembe hizo za melanin sio ugonjwa bali ni hali tu ya kimaumbile."

Alisema kuwa ushahidi wa kuwa zeruzeru na uwe utafanikiwa maishani ukitunzwa vilivyo ni kuwa "tuko na Mwaura ambaye ni mbunge maalum na mwanasiasa msomi na aliye shupavu, tuko na Jaji wa Mahakama kuu ambaye ni Mumbi Ngugi na ambaye ametikisa safu ya kisheria kwa kutoa maamuzi ya kesi yaliyo na ustadi mkuu na pia kuwa na wengi duniani ambao ni maarufu."

Miongoni mwa watu mashuhuri duniani walio albino ni pamoja na Mfalme Edward wa Uingereza, Empara Senei wa Japan, Seif Keita ambaye ni mwanamuziki kutoka Mali, mwanamitindo Connie Chiu, William Archibald ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford, Johny Edgar Winter, Winston Foster na Brother Ali—wote wakiwa ni wanamuziki mashuhuri.

Autosomal Recessive

Dkt Anne Murigi anasema kuwa wazazi wa mtoto zeruzeru huwa na chembechembe ya kimaumbile ijulikanayo kama Autosomal Recessive (AR) na ambayo huzua urithi wa uzeruzeru kwa mtoto.

Anasema kuwa hata wale kwa sasa ambao wanaonekana kuwa wa kawaida wanaweza kuwa na chembechembe hiyo ila tu hawajijui na wanaweza wakapata mtoto zeruzeru.

“Kwa hivyo, unaweza kuwa unacheka kilema cha zeruzeru ilhali wewe mwenyewe unangojewa na zamu yako ya kumzaa mwana na ushtuke umezaa zeruzeru na tukuone kwa vyombo vya habari ukisingizia wakunga hospitalini eti walikuibia mtoto na kisha wakakubadilishia na asiye wako,” aonya.

Anasema kuwa visa vya mtoto zeruzeru kuzaliwa duniani huwa ni kati ya 1:17,000 na 1:20,000.

Anasema kuwa ‘ulemavu’ wa zeruzeru huwa ni upungufu wa uwezo wa kuona, mboni za macho kuonekana zikibingirika na huwa wanaathiriwa sana na
miale ya jua.

“Zeruzeru akiangaziwa sana na miale ya moja kwa moja ya jua anaweza kupata ugonjwa wa saratani ya ngozi na ni vyema wawe wakivalia miwani spesheli na pia kujipaka mafuta yenye kemikali za kupunguza athari za jua,” asema.

Anasema kuwa ikiwa zeruzeru watapewa nafasi kamili ya kimaisha sawa na wenzao katika jamii, huwa na nafasi sawa ya kuishi, kuimarika na kuchangia ujenzi wa taifa sawa na wengine.

“Hata hivyo, cha kujua ni kuwa; hakuna sayansi yoyote ya utabibu ambayo inaweza kubatilisha hali ya uzeruzeru,” asema.

Mwaura alisema kuwa kunafaa kuwa na umoja wa kitaifa wa kulinda walemavu wote katika jamii kupitia kukumbatia maadili mema katika kutoa huduma kwao.

“Tumekuwa tukiomba serikali itekeleze hafla ya kitaifa ya kusajili wote walio na ulemavu, uorodheshwe kihali na matakwa yao kwa kila kundi ili tuwe na takwimu muhimu,” akasema.

Alisema kuwa muungano wake ungetaka serikali ichukue takwimu za kufahamu ni watoto wangapi wanaoishi na hali hiyo ili wapate msaada muhimu wanaohitaji kama wa kulindwa dhidi ya athari za jua na pia kusajiliwa katika shule spesheli ambako watapewa mawaidha ya kujikubali na pia wananchi wahamasishwe dhidi ya kuwatenga.

“Kwa sasa, juhudi zetu za kusajili zeruzeru hapa nchini licha ya kuwa na changamoto tele zinaashiria kuwa tuko takriban 10,000, na uwezekano wa mtoto zeruzeru kuzaliwa uko katika kiwango cha 1:5000,” akasema.

Anasema kuwa maisha ya mtoto zeruzeru huwa mazito sana kwa kuwa wengi wao huishi na mama mzazi pekee bila malezi ya baba.

“Mama wengi hufukuzwa kutoka ndoa zao wanapojifungua mtoto zeruzeru. Asilimia 60 hadi 70 ya watoto zeruzeru hapa nchini hupokea malezi ya aidha mama mzazi au nyanya zao kwa kuwa akina baba zao huwakataa katika boma wakisema wao ni laana,” asema.

Katika visa vingine vya ukatili, watoto wa aina hiyo huuawa punde tu wanapozaliwa kwa misngi kuwa aidha mimba za mamazao zilirogwa ndipo ‘mtoto akaharibikia uja-uzitoni.’