http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927652/medRes/2219499/-/e6d4ey/-/mzee.jpg

 

Mzee Yusuf: Kama si ujasiri Leyla angeumia zaidi

Mzee Yusuf 

Na Nasra Abdallah

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  14:25

Kwa Muhtasari

Licha ya majambazi hao kumuumiza mkewe naye aliwapa kipigo

 

Dar es Salaam. Aliyekuwa mwimbaji taarabu, Mzee Yusuf amesema ujasiri wa mkewe, Leyla Rashid, umemsaidia kupambana na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walipovamia nyumbani kwao Chanika, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Mzee Yusuf ambaye sasa ni mwalimu wa dini, alisema licha ya majambazi hao kumuumiza mkewe naye aliwapa kipigo.

Akisimulia tukio lilivyokuwa, alisema ilikuwa ni saa 2.30 usiku Jumatatu wiki hii wakiwa sebuleni wanaangalia TV, wakasikia kishindo cha watu kikitua ndani ya uzio na kuhisi kwamba wamevamiwa na wahalifu.

“Mimi kwa haraka nilipochungulia niliwaona wawili nje nikawafuata kupambana nao kumbe walikuwa zaidi ya saba na wawili walikuwa getini.”

“Huku nyuma watatu wakaingia ndani na kukutana na mke wangu huku wakimtaka awaonyeshe pesa zilipo na kumtisha kwa bunduki, ingawa mke wangu haraka sana alibaini ilikuwa bandia ndipo alipoanza kupambana nao,’’ alisema Yusuf.

Alisema kwenye mapambano hayo kwa sababu walikuwa wengi walimzidi nguvu na kumpiga mateke ya tumboni yaliyopelekea kusikia kizunguzungu na kuanguka.

Alivitaja vitu vilivyoibiwa mbali na fedha kuwa ni simu na vifaa vya shule vya watoto.

“Mke wangu yupo hospitali akifanyiwa vipimo mbalimbali, amekuwa akilalamika kusikia vitu vinakata tumboni,” alisema Yusuf.

Kwa upande wake Leyla alisema, “ wameniumiza ingawa nimepambana nao kwa sasa naomba nipumzike,’’ alijibu kwa kifupi.