NGILA: Kiu hii ya mikopo ya kiholela ipunguzwe

Eurobond

Waziri wa Fedha Henry Rotich pamoja na Katibu wa Kudumu Kamau Thugge walipofika mbele ya kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma Novemba 2, 2015 ambapo walihojiwa kuhusu fedha za mkopo wa Eurobond. Picha/ EVANS HABIL  

Na FAUSTINE NGILA

Imepakiwa - Tuesday, August 1  2017 at  13:06

Kwa Mukhtasari

MAZOEA ya Kenya kuendelea kuomba mikopo kwa wingi kufadhili miradi ni tishio kubwa kwa uchumi. Yanadidimiza uwezekano wa kupata mikopo hiyo katika siku za usoni wakati wa mikasa au taifa litakapohitaji pesa kwa dharura.

 

Kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Sera za Umma na Uchanganuzi (KIPPRA), taifa letu limepita kiwango cha mikopo kilichowekwa na mataifa ya Afrika Mashariki.

Jumuiya ya Afrika Mashariki imewekea mataifa wanachama kiwango cha asilimia 50 ya utajiri kwa mikopo yote, kama kiwango cha juu zaidi taifa linaweza kukopa.

Mnamo Machi 2017, deni la Kenya lilikuwa Sh4.04 trilioni, ambalo ni asilimia 52.6 ya utajiri wa nchi, kulingana na takwimu za Wizara ya Fedha.

Kilichochochea Kenya kuvuka kiwango hiki ni miradi ya miundomsingi ambayo imefadhiliwa na mikopo kutoka Uchina.

Uchunguzi

Mataifa mengine hayajavuka kiwango hiki - Uganda asilimia 38.6, Burundi asilimia 42.6, Rwanda 37.3 na Tanzania 36.5 kulingana na taasisi hiyo.

Kenya ilikuwa na deni la Sh1.89 trilioni mwezi Juni 2013, kumaanisha mzigo huu wa madeni umeongezeka zaidi ya maradufu tangu wakati huo.

Shirika la Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) lilikusanya Sh1.365 trilioni katika kipindi kilichotamatika Juni 2017. Pesa hizi zikilinganishwa na deni tunalodaiwa, utapata asilimia 296, ambayo iko juu zaidi ikilinganishwa na lengo la Hazina ya Fedha ya kuipunguza hadi asimilia 198.3 mwaka huu.

Mwenendo huu wa serikali kukopa fedha kutoka mataifa ya nje bila kujali hatimaye utatuumiza sisi Wakenya. Ni onyo ambalo Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilikuwa limetoa mwanzoni mwa mwaka.

Lakini kuna hela za bondi ya Euro ambazo tungetumia kufadhili miradi yetu wenyewe bila kutegemea mikopo ya nje. Licha ya Wizara ya Fedha kutoa ahadi ya kuelezea Wakenya jinsi fedha hizo zilitumika, imesalia kimya kuhusu suala hilo.

Ninaiona Kenya ikiulilia Ulimwengu katika miaka ya hivi karibuni baada ya uchumi wake kuyumba kwa kuwa hakuna taifa ambalo litakubali kuikopesha pesa. Serikali isipoweka sera za kuzuia ukopaji wa kiholela na mikakati ya kulipa madeni haya, maisha ya Wakenya yatasalia kuwa magumu.