Nadharia ya sarufi katika Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  14:26

Kwa Muhtasari

Sarufi ni taaluma ya uchambuzi wa lugha inayojumuisha viwango vyote vya uchambuzi.

 

ILI kuichambua kikamilifu nadharia hii, ni muhimu kuelewa maana ya sarufi katika Kiswahili.

Maana ya sarufi imefafanuliwa kwa namna anuai na wataalam mbalimbali kama ifuatavyo.

Kwa mujibu wa Kihore (2005), sarufi ni sayansi ya muundo wa lugha pamoja na sheria, kanuni na matumizi yake ambayo kwa kawaida hukubalika kwa watumiaji wake.

Massamba na wenzake (1999) wanaeleza kuwa, sarufi ni kanuni na sheria au taratibu za uchambuzi zinazotawala lugha.

Hivyobasi, sarufi ni taaluma ya uchambuzi wa lugha inayojumuisha viwango vyote vya uchambuzi yaani kiwango cha umbo, sauti, miundo na maana.

Nadharia ya Sarufi Zalishi

Mwasisi wa nadharia hii ni mwanaisimu Noam Chomsky (1928).

Dhana ya sarufi zalishi iliwezesha mapinduzi ya msingi katika taaluma ya isimu.

Aidha, mawazo ya Chomsky yalidhihirisha kuwa mbinu za uchanganuzi wa sentensi zilizotumika hapo awali hazikuwa toshelevu, hivyo sarufi zalishi ilizuka kutokana na kasoro za sarufi miundo katika uchanganuzi wa lugha.

Chomsky, amewasilisha mtazamo wa Sintaksia unaotambuliwa kama Sarufi  Zalishi.

Azma kuu ya Chomsky ilikuwa kukuza fafanuzi mwafaka za hali ya sintaksia ya lugha mbalimbali, yaani jinsi lugha mahususi zinavyounganisha maneno kuunda sentensi.

Vilevile, alidhamiria kukuza nadharia ya jumla ya sintaksia inayobainisha ni mambo yapi yanayopatikana katika lugha mbalimbali na jinsi yanavyotofautiana katika uwanja wa sintaksia.

Ni muhimu kumaizi kwamba msingi wa Sarufi Zalishi unajikita katika uundaji wa nadharia ambayo ingeeleza namna lugha hutumiwa na watumiaji wake hasa kwa kutazama namna wanavyotumia kanuni chache zilizopo katika lugha yao kuzalisha sentensi nyingi na zisizo na kikomo, katika kurejerea hali mbalimbali, ingawa sentensi hizo zinaweza kuwa sahihi au zisizo sahihi. (Matinde, 2012).