http://www.swahilihub.com/image/view/-/4389712/medRes/1936654/-/le3q64/-/ngano.jpg

 

Narok: Kaunti maarufu kwa kilimo cha ngano

Ngano

Mfanyakazi avuna ngano Julai 21, 2016, katika shamba lililo katika eneo la Ilmashariani, Kaunti ya Narok. Picha/GEORGE SAYAGIE  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, April 12  2018 at  10:19

Kwa Muhtasari

Jamii ya Maasai inatambulika sana kwa ufugaji.

 

UFUGAJI ni shughuli maarufu ya utafutaji riziki katika kaunti ya Narok.

Hii ni kwa sababu eneo hilo jamii ya Maa ndiyo inaishi.

Tangu awali, jamii hiyo imefahamika kuthamini mifugo na aliye na ng'ombe kutambulika kuwa bwanyenye.

Ufugaji wake ni ule wa kuhamahama, kwa minajili ya kutafutia mifugo lishe na maji.

Hayo kando, ukweli ni kwamba kilimo kinanawiri sekta ya kilimo.

Unapozuru Narok miezi ya Mei hadi Agosti, unakabribishwa na rangi ya kijani kibichi kwenye mashamba makubwa makubwa.

Rangi hiyo hasa ni kutokana na nafaka aina ya ngano.

Mwezi Septemba hadi Novemba, nafaka hiyo huanza kukauka na kuvunwa.

Bi Winnie Oloshoirua, mwalimu Narok na mkulima pia, anasema ametambua kilimo kina faida tele kikilinganishwa na ufugaji.

"Ingawa mimi ni mkulima mdogo, kilimo cha ngano ni uwekezaji bora kwa kuwa hakinihitaji wakati wote kuwa shambani. Msimu wa upanzi, kupulizia dawa, kung'oa makwekwe na kuvuna ndio huwa shambani tu," aeleza Bi Oloshoirua.

Anaongeza kuwa wakazi wa kaunti hiyo wamezamia kilimo baada ya kuona mifugo, hasa wanaohamishwa hamishwa kila wakati kwa kuwatafutia lishe na maji imewafanya kuwa watumwa.

Anasema kuwa wengi wa wakazi Narok wana mashamba makubwa, hususan waliyorithi kutoka kwa wazazi wao.

"Shabaha yetu ni tufanikishe ajenda ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuangazia usalama wa chakula, iliyoko miongoni mwa zile kuu nne," aeleza.

Ngano imesheheni wanga

Aidha, kaunti hiyo ndiyo nambari mosi katika kilimo cha ngano.

Kaunti zingine zinazokuza ngano ni; Nakuru, Uasin Gishu, Nyandarua, Narok, Meru Central, Trans Nzoia, Elgeyo Marakwet na Laikipia.

Ngano ni aina ya nafaka iliyosheheni wanga; yaani carbohydrates. Wanga husaidia sana katika kuupa mwili nguvu.

Nafaka hiyo hutumika kuunda bidhaa za kula kama vile mkate, chapati, keki, biskuti, miongoni mwa zingine.

Licha ya sifa zake kuntu katika kilimo cha ngano, Narok kungali na visa vya ukeketaji wa wanawake (FGM).

Upashaji tohara kwa wanawake ulipigwa marufuku 2001 nchini. Viongozi kadha tajika nchini kama vile Bi Linah Jebii Kilimo chini ya wakfu wake wa Jebii Kilimo Foundation wamekuwa katika mstari wa mbele kupiga FGM vita.

Narok inapatikana Kusini mwa Rift Valley.

Kaunti hiyo yenye zaidi ya watu 850,920 kwa mujibu wa sensa ya 2009, inaongozwa na gavana Samuel Ole Tunai. Seneta wake ni Bw Ledama Ole Kina, huku mwakilishi wa wanake akiwa Bi Roselinda Soipan Tuya.

Kwa mujibu wa katiba ya 2010 iliyoanza kutumika 2013, Narok imeorodheshwa ya 33 kwa jumla ya kaunti 47 nchini.

Ina ukubwa wa kilomita 17,921.2 mraba na imeundwa kwa maeneobunge sita; Narok Kaskazini, Narok Kusini, Narok Mashariki, Narok Magharibi, Emurua Dikirr na Kilgoris.

Aidha, ina wadi 30 zinazoongozwa na madiwani.