Nelson Marwa: Baadhi ya viongozi wapendekeza ateuliwe Inspekta Mkuu wa Polisi

Nelson Marwa

Mshirikishi wa eneo la Pwani Nelson Marwa. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, December 30  2017 at  15:07

Kwa Mukhtasari

Nelson Marwa ni hasidi mkuu wa walanguzi wa mihadarati, wafuasi wa magenge na makundi mengine haramu hasa ya ugaidi, viongozi ambao hawana heshima kwa serikali na mtiifu kwa serikali anayohudumia.

 

NELSON Marwa. Hili ni jina ambalo Wakenya wengi wana ufahamu wa ni mtu wa aina gani. Cha maana kujua ni kuwa yeye ni mfanyakazi wa umma ambaye ametesa wengi wasiozingatia analowajibikia kudumisha.

Ni hasidi mkuu wa walanguzi wa mihadarati, wafuasi wa magenge na makundi mengine haramu hasa ya ugaidi, viongozi ambao hawana heshima kwa serikali na mtiifu kamili kwa serikali anayohudumia.

Amenukuliwa akisema: “Ninaheshimu serikali iliyoko mamlakani na ndiyo nawajibikia. Katika kuwajibika kwangu, ni lazima niwajibikie kila Mkenya katika hali zake kwa kuwa serikali huwa ni ya kitaifa. Ukitaka nikuhudumie kwa kiwango sawa, shinda kura kwa njia halali na ukiniteua kuwa mfanyakazi wako, tutachapa kazi jinsi unionavyo leo.”

Marwa akikulenga, utamchukia au umpende ukigundua kuwa alikuwa akikuweka kwa mkondo wa utiifu kwa sheria.

Akiongea, na iwe ni wewe analenga; na iwe ni kwa mabaya yako, basi jiandae kupakwa angalao 'tope la aibu'.

“Kwani wewe unafikiria ndiye nani? Eti kazi yako ni kufadhili magenge pale mtaani na unarejea kwa bibi yako kusherehekea jinsi umehangaisha watu wasio na hatia? Si uwe mwanamume kamili ulenge kuhangaisha mtu kama mimi anayejielewa? Mbona upige wanyonge na kisha unajigamba?” akauliza Agosti 2017 akilenga mwanasiasa mmoja wa Pwani.

Kwa sasa, Marwa ni mshirikishi wa kiusalama wa eneo la Pwani na taifa likielekea katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017, alionya gavana Hassan Joho wa Mombasa kuwa “huo utundu wako wa kutoheshimu Rais nitauzima”.

Wakiona walioshuhudia akisema hayo kama alikuwa tu akitoa mzaha, akaweka mikakati ya kila wakati Rais Uhuru Kenyatta akizuru Pwani, Joho alikuwa akiwekwa katika nyumba yake au afisi bila idhini ya kutoka nje.

“Mimi sijali utasema nini au utaniita majina gani. Bora tu uelewe rais sio mtu wa kutukanwa hapa Pwani. Unamtukana au kubishana naye kwani wewe ni nani?” akahoji katika majibizano yake na Joho.
Aliendelea mbele na kutekeleza ilani yake ya kumpokonya Joho maafisa wa polisi waliokuwa wakimlinda.

“Uwe na bahati gani eti unalindwa na maafisa wa polisi walio katika huduma ya serikali ambayo unadunisha kila saa?” akateta wakati wafuasi wa Joho walizidisha kilio kuwa anadhulumiwa.

Alisema tofauti zake na wanasiasa sio za kibinafsi bali ni za kikazi.

"Kama mtu aliyeelimika, nina uhuru wa kufuata yale ninayoyaona kuwa ya busara na kususia yale ambayo naona hayafai. Usisahau kuwa mimi sio mwanasiasa, kwa hivyo, laini zetu zikihitilafiana, usituone kama maadui bali tunarekebishana. Ananisema nami namsema,” akasema.

Anarejelewa kuwa ni mfanyakazi asiyependa mzaha na ambaye kicheko chake labda huwa cha usiri katika giza totoro.

Nelson Marwa amerekodiwa kuwa mwana wa mwanamisheni na ambaye alizaliwa katika taifa la Uganda na akalelewa katika taifa la Tanzania.

Kinasaba,, wazazi wake yumkini wana asili ya Kuria katika eneo la Nyanza.

Ana shahada tatu za uzamili, hivyo basi kumweka katika orodha ya maafisa wa kiusalama nchini ambao wana ukwasi mkuu wa elimu.

Alisomea biashara katika Chuo Kikuu cha Baraton na akaelekea hadi Australia kwa shahada ya uzamili katika somo hilo. Ako na kiwango sawa na hicho katika somo la Mikakati ya Kiusalama kutoka Chuo Kikuu cha Virginia School of Coast Guards na shahada sawa na hiyo katika somo la udhibiti wa majanga - alisomea nchini Israel.

Mhadhiri

Mwaka wa 1991 alikuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Egerton kabla ya kujiunga na utawala nchini.

Tangu aelekezwe kuhudumu Pwani, kila mdadisi wa masuala ya kiusalama anaungama kuwa “Marwa ndiye Pwani na Pwani ni Marwa kiusalama”.

Novemba akitangaza kuwa msitu wa Boni ulikuwa unatumika kama hifadhi ya wanamgambo wa Alshabaab, alisema kuwa atamwaga mabomu huko na afuatilize kwa kumimina risasi ndani ya msitu huo, akionya raia wakae mbali na msitu huo.

Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Sabina Chege, Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ni miongoni mwa wengi ambao wamependekeza Marwa ateuliwe kuwa Inspekta Mkuu wa Polisi kutokana na misimamo yake mikali na isiyo na unafiki kuhusu usalama wa taifa.

Amehudumu Nyeri, Kinango, Rift Valley, Mombasa kabla ya kupandishwa cheo na kukabidhiwa masuala ya kiusalama Pwani yote ayashughulikie.

Machi 3, 2017, uvumi uliibuka kuwa amehamishiwa hadi eneo la Rift Valley kutokana na ushawishi wa wanasiasa wa Pwani na mitandao ya ulanguzi wa mihadarati.

“Yaani mnajua kuhusu kazi yangu kuliko mimi ambaye ndiye mwenye hiyo kazi? Tangu lini afisa wa serikali akahamishwa kienyeji kupitia udaku mitaani? Sasa sababu nimewaita kwa afisi yangu ili niwape dokezi za hali ilivyo kiusalama hapa Pwani, mmekuja Rift Valley au mko Pwani?” akawauliza waandishi wa habari.