Ni aibu kuwa na wiki ya maji bila maji

Na Phinias Bashaya

Imepakiwa - Tuesday, April 2  2019 at  08:59

 

Upungufu wa rasilimali ya maji ni miongoni mwa mijadala inayotawala kila mwaka kupitia majukwaa mbalimbali wakati wa kuadhimisha wiki ya maji.

Hata hivyo kwa kile ninachokiona hakuna mafanikio yanayoweza kuhusishwa moja kwa moja na tukio hilo la kila mwaka.

Kimsingi Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanaendelea kuwa na taswira ya tukio la kawaida ambalo pamoja na kufanyika kila mwaka, hakuna ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la upatikanaji wa maji si mijini wala vijijini.

Kilio cha ukosefu wa maji kinaendelea kusikika kutoka maeneo mbalimbali nchini. Kilio hicho kikiendelea ahadi nazo hazikosekani kila wakati wa maadhimisho. Viongozi wanatamba majukwaani kuwa wataleta maji lakini kila siku hatuyaoni.

Pamoja na kuwa upungufu wa rasilimali ya maji unachangiwa na mambo mbalimbali zikiwamo changamoto za mazingira na uharibifu wa vyanzo vya maji, yapo maeneo yasiyoguswa na tatizo hilo na bado upatikanaji wa maji umekuwa mgumu kwa wananchi.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya maji kwa mwaka 2019 inatoa matumaini kwa wananchi kwamba hakuna atakayeachwa na kuwa kuna juhudi za kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za maji mijini na vijijini.

Hata suala la wananchi kupewa uhakika wa kupata huduma hiyo ndani ya mita 400 katika makazi yao, ni miongoni mwa ahadi nyingi za aina hiyo ambazo hutoa faraja ya muda kwa wananchi bila kuona mabadiliko waliyoahidiwa.

Kero ya maji pia imekuwa ajenda ya kisiasa ambapo wakati wa kujadili Bajeti ya Wizara ya Maji katika Bunge la Bajeti mwaka jana wabunge waliungana kuokosoa bajeti ya wizara hiyo waliyosema haikuwa na majibu ya utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi.

Wiki chache baadaye Rais John Magufuli alifanya mabadiliko ya mawaziri ili kuimarisha utendaji wa Serikali.

Katika mabadiliko hayo Profesa Makame Mbarawa alikabidhiwa wizara hiyo akirithi nafasi ya Isack Kamwele aliyehamishiwa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo awali ilikuwa ikiongozwa na Profesa Mbarawa.

Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo bado hakuna unafuu mkubwa uliopatikana na kero zilezile zimeendelea kusikika kutoka maeneo mbalimbali, ikiwamo kukwama kwa miradi ya maji katika maeneo mengi hasa vijijini.

Pamoja na kukwama kwa miradi ya maji inayohusishwa na utendaji wa kusuasua wa wasimamizi, lakini pia wizara hiyo inarushiwa lawama kwa kushindwa au kuchelewesha fedha zinazokusudiwa katika utekelezaji wa miradi husika.

Tatizo la maji ni kubwa kote nchini katika awamu zote za uongozi,ambapo changamoto zile zile zinatajwa kwenye maadhimisho yanayofanyika kila mwaka ingawa hukosa msukumo wa utekelezaji kuanzia kwenye mipango ya bajeti na utekelezaji wa jumla.

Katika baadhi ya maeneo Serikali imewekeza kiasi kikubwa kwenye miradi ya maji, lakini upatikanaji wa huduma hiyo ni tatizo na katika maeneo miradi iliyokwama inahusishwa na ubadhirifu na hujuma ya miundombinu.

Mathalani, hivi karibuni Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso alikagua miradi iliyotekelezwa katika wilaya za Mkoa wa Kagera ambapo katika baadhi ya maeneo huduma hiyo haipatikani pamoja na kuwa utekelezaji umekamilika na malipo kufanyika.

Baadhi ya miradi ilionekana kutumia kiasi kikubwa cha fedha, huku ufanisi wake ukiwa mdogo ambapo kwa bajeti ile ile ilibainika miradi ya maji iliyosimamaiwa na Mamlaka ya Majisafi Manispaa ya Bukoba (Buwasa), ilikuwa na uhai na kuonyesha thamani ya fedha.

Rais Magufuli kwa nyakati tofauti ameonya kuhusu suala la maji na kutaka eneo hilo lipewe kipaumbele na kuwa hakuna sababu ya wananchi kuendelea kulalamika kutokana na kero ya ukosefu wa maji.

Pamoja na onyo hilo kilio cha wananchi kimeendelea kusikika hali inayoonyesha kuna eneo tunakosea kuanzia kwenye suala la kupanga vipaumbele vyetu, utekelezaji na uwajibikaji kuanzia kwa wananchi na Serikali yao.

Hivyo Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanatakiwa kuwa jukwaa la kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazoiangusha sekta hiyo na kuhoji fedha zinazoteketezwa kwenye miradi ya maji vinginevyo tuone aibu ya kuwa na maadhimisho ya wiki ya maji bila maji.