Ni jukumu letu kutokomeza malaria

Imepakiwa - Thursday, April 25  2019 at  12:02

 

Leo ni siku ya maadhimisho ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria duniani ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kaulimbiu mwaka huu inasema “ziro malaria inaanza na mimi.”

Malengo ya WHO ni kuutokomeza ugonjwa huo duniani ifikapo 2030. Lakini wakati huohuo ni vyema tujue kwamba malaria ni moja ya magonjwa yanayoongoza kwa vifo hapa nchini.

Ugonjwa huu unatisha kutokana na watu wengi kuugua, na wengine kufariki dunia. Hata hivyo ni ugonjwa ambao kwa maamuzi na bidii za binadamu unaweza kutokomezwa. Waswahili wanasema “kinga ni bora kuliko tiba” ikiwa na maana kuwa ugonjwa huo usipodhibitiwa ni kikwazo kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Rai yetu ni kuwa ugonjwa huo unaoweza kudhibitiwa ni vyema wananchi wakaamua kuukataa kwa kuchukua tahadhari za kujikinga nao. Kujikinga na ugonjwa huu ni muhimu wananchi wakasikiliza maoni yanayotolewa na wataalamu, na kuyatekeleza kulingana na maelekezo yanayotolewa.

Miongoni mwa njia ambazo wataalamu wanashauri ni matumizi ya vyandarua vilivyowekwa dawa ya kuua mbu.

Hata hivyo, tunashauri kwamba wananchi kabla ya kununua vyandarua wanapaswa kuuliza na kujiridhisha kama wanavyonunua vimewekwa dawa.

Pia, inapaswa wananchi wakazingatia usafi wa mazingira kwa kufukia madimbwi na mashimo yanayosababisha maji kutuama. Maji yanayotuama huzalisha mbu kwa kuwa wadudu hao hupendelea maeneo yenye majimaji.

Kwa mfano, madimbwi ya maji ya mvua yaliyokaa muda mrefu bila kukauka, unyevunyevu vichakani na kwenye nyasi ndefu, makopo yenye uwazi yaliyotelekezwa na kujaa maji, magari mabovu yaliyonyeshewa mvua na kukusanya maji ndani na mabwawa madogomadogo kama ya kufugia samaki ni mazalia ya mbu.

Hivyo ni vyema kufukia madimbwi, kufyeka nyasi, kuchoma au kusafisha makopo na pia kuondoa magari mabovu na chochote kinachoweza kukusanya maji kwa muda mrefu maeneo yote yanayozunguka nyumba zetu.

Pia, kwa wajawazito ni muhimu kujikinga na ugonjwa wa malaria kwa kuwa wajawazito wana hatari kubwa ya kung’atwa na mbu.

Katika kuhakikisha kwamba udhibiti wa malaria unafanikiwa, tunawashauri wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za malaria kwa wagonjwa.

Hili ni pamoja na kuzingatia dozi sahihi kwani kutomaliza kunamaanisha ni kuviacha baadhi ya vimelea mwilini ambavyo havikufa na kusababisha hatari nyingine ya kuugua tena malaria. Ni rai yetu kwa wananchi kutumia dawa baada ya kumuona daktari, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaongeza usugu wa dawa mwilini bila sababu za msingi, na pia kuhatarisha maisha yao.

Sote tunafahamu usugu wa dawa za malaria kuwa ni hatari na inamaanisha ukipata malaria na vimelea ulivyonavyo vimeshakuwa sugu kwa dawa zilizopo za malaria, maisha yako yanakuwa hatarini kwani madaktari watashindwa kukutibu.

Ni vyema tukazingatia kwamba malaria ni ugonjwa hatari unaoua kwa haraka, hivyo pindi unapohisi una dalili za malaria wahi zanahati, kituo cha afya au hospitali ili upatiwe tiba sahihi.