http://www.swahilihub.com/image/view/-/1412060/medRes/363143/-/k2gow4/-/DnRaila2005t.jpg

 

Ni mwaka muhimu, tuweke utaifa mbele

 Raila Odinga, ODM, CORD

Kiongozi wa ODM Raila Odinga akihutubia wafuasi wa chama hicho awali. Picha/MAKTABA 

Na SWAHILIHUB

Imepakiwa - Monday, January 2  2017 at  11:42

Kwa Mukhtasari

HATIMAYE, Mwaka 2017 umefika ambao mbali na kuwa Mwaka Mpya, ni mwaka muhimu kwa Wakenya ambao wanatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu Agosti 8 iwapo hakutakuwa na mabadiliko yoyote.

 

Siasa na malumbano ya kila aina yalishuhudiwa 2016 miongoni mwa wanasiasa huku wengine hata wakielezea maazimio yao ya 2022.

Ni muhimu hata hivyo, kwa Wakenya na viongozi kwa jumla kutambua kuwa ipo haja ya kudumisha amani ili kuepusha Kenya na majanga ama maafa yoyote.

Ni Matarajio ya taifa kwa jumla kuwa uchaguzi utakuwa wenye haki na usawa.

Wajibu upo kwa kila mmoja kuhakikisha kuwa anakumbuka kuwa Kenya ni kubwa kuliko sisi sote.

Wanasiasa lazima wawache ubinafsi na Wakenya hasa vijana kutokubali kutumiwa vibaya, kwa kuwa mwisho sawa na wapiganapo fahali wawili nyasi ndizo huumia, wao ndio wataishia kupata hasara ama kutofaidika kwa njia yoyote ile.

Lakini mbali na kuangazia uchaguzi na siasa, gharama ya maisha pia imekisiwa kupanda kwa kiasi kikubwa na serikali isaidie wananchi wake ili waweze kumudu gharama na kuweza kuishi maisha yenye hadhi kwao.

Wakenya wamebainishwa kuwa watu wenye bidii na hivyo serikali inastahili kuweka mikakati ambayo itawasaidia kuona umuhimu wa bidii yao, kama kuweza angalau kubakia na hela za kuweka akiba kwa siku zijazo, na sio kuishi kwa madeni na mikopo, ambayo mara nyingi haitumiki kwa miradi ya kujistawisha bali ni kwa matumizi ya kila siku kama kulipa kodi ya nyumba na chakula, ama kulipia karo.

Kwa hivyo, katika mwaka huu mpya, kweli Wakenya watashuhudia kila mwanasiasa akitafuta kura, na wajibu uko kwao kuangalia wale watakaowatetea kama wengi wanavyodai wakati wa kampeni.

Wananchi wanastahili kufahamu kuwa wao ndio wenye mamlaka ya kufanya uamuzi na katu wasipotoshwe na vyama ama kabila na kisha kujuta baadaye.

Ni Mwaka Mpya, na tumaini ni kuwa Kenya itakuwa na mwelekeo mpya, bora na ambao utadumisha amani na kuisaidia kujiimarisha zaidi pamoja na kukabiliana na ufisadi vilivyo.