http://www.swahilihub.com/image/view/-/4865496/medRes/2178773/-/v43jjr/-/maia.jpg

 

Ni wajibu wetu kutunza mazingira

Mianzi

Mkurugezi wa idara ya misitu katika kaunti ya Busia, Fredrick Asonya (na mche mkononi akiongea kwa simu) baada ya kuongoza upanzi wa mianzi katika kingo za mto Suo eneobunge la Matayos Novemba 22, 2018. Amesema mti huo una manufaa chungu nzima kwa mkulima kando kulinda mazingira. Picha/GAITANO PESSA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, December 28  2018 at  12:46

Kwa Muhtasari

Tukihifadhi mazingira tunajihakikishia kuishi raha mustarehe.

 

MWAKA 2017 na mapema mwaka 2018 taifa lilishuhudia ukame uliosababisha uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo nchini, lakini pia raia katika kila pembe ya nchi aghalabu walionja athari hasi za hiyo.

Ukataji wa miti kiholela na uchomaji wa makaa ulinyooshewa kidole cha lawama kama kiini kikuu cha janga hilo. Kilichofuata kikawa kampeni ya kitaifa ya upandaji wa miti iliyoongozwa na wizara ya mazingira chini ya kigogo wake Keriako Tobiko.

Machi 2018 Naibu Rais Dkt William Ruto alitangaza marufuku kwa muda wa miezi mitatu mfululizo ya ukataji wa miti katika misitu ya serikali.

Marufuku hayo yalionekana pia kuelekezwa kwa misitu ya wapanzi binafsi.

Aidha, Dkt Ruto alizindua jopokazi maalumu kutegua kitendawili cha uharibifu wa misitu nchini ikiwa ni pamoja na kuongoza kampeni ya upandaji wa miti. Jopo hilo linaongozwa na waziri Tobiko.

Athari za marufuku hiyo zimesababisha bidhaa zitokanazo na miti kuuzwa mara dufu.

Mojawapo wa misitu iliyoripotiwa kukumbwa na uharibifu mkubwa ni ule wa Mau. Msitu huo una utata kutokana na kufurushwa kwa baadhi ya wakazi wanaotuhumiwa kunyakua ardhi yake na kuendesha shughuli haramu ya ukataji wa miti kiholela na kuchoma makaa.

Suala la kuwaondoa limeingiliwa kisiasa, huku viongozi wa Bonde la Ufa wakionekana kugawanyika. Baadhi yao wanadai wakazi waligawiwa ardhi kisheria katika serikali ya Rais (mstaafu) Daniel Arap Moi, wengine wakiwataja kama "wanyakuzi wa ardhi".

Hata hivyo, wanaochukulia ufurushaji kuwa haramu wanataka kufidiwa kwa waliondolewa na watakaondolewa. Mlima Kenya na Aberdare pia imevamiwa kwa ukataji wa miti, washirika wakigeuza migunda hiyo kuwa uga wa kilimo.

Kigezo cha Umoja wa Mataifa (UN) cha misitu ni asilimia 10, Kenya ikiwa katika asilimia saba kwa sasa.

Kwenye ruwaza yake, serikali inalenga shabaha ya asilimia 15 kufikia mwaka wa 2022. 

Serikali inasema ili kuafikia hitaji la UN, kila kaunti inapaswa kupanda aghalabu miti milioni 10 kwa mwaka.

Rais Uhuru Kenyatta mapema mwakani alisema lengo lake ni kuona taifa linapanda karibu miti milioni 500 kila mwaka. Hata hivyo, wachanganuzi wa masuala ya mazingira wanasema kampeni hii itaafikiwa kikamilifu ikiwa Rais ataagiza wizara zote zivalie njuga jambo hili.

"Baraza la mawaziri ndilo mikono ya kazi ya Rais, ashinikize wizara zote zifanye kampeni ya upanzi wa miti nchini mbali na majukumu waliyotwikwa," apendekeza Kiruthi Junior, mtaalamu wa miti na kilimo.

Ushirikiano

Baadhi ya kaunti zimetilia maanani upanzi wa miti na kulingana na Bw Kiruthi ni kuwa shughuli hii itashika kasi wizara zikishirikiana nazo sako kwa bako.

Ingawa anashauri haja ya serikali kufadhili wananchi kwa miche ili malengo yake yatimie.

"Ina uwezo wa kumpa kila Mkenya miche apande ili tuokoe misitu yetu," anasema Bw Kiruthi.

Wizara ya Usalama wa Ndani inayoongozwa na Dkt Fred Matiang'i pamoja na ya Utumishi ya Umma chini ya Profesa Margaret Kobia, zimeonesha juhudi zao kushirikiana na ya mazingira. Wiki iliyopita, Desemba 21, Bw Matiang'i alionya machifu na manaibu wao kwamba watabeba mzigo wa ukataji wa miti katika misitu iliyo katika kata zao.

Waziri aliwataka viongozi hao kuongoza kampeni dhidi ya uharibifu wa misitu nchini, akiagiza idara ya polisi kuwa macho kwa uchomaji wa makaa na usafirishaji wa mbao.

"Machifu watakaoruhusu ukataji wa miti watakuwa na kibarua kueleza sababu ya sheria kukiukwa. Kila mmoja atabeba msalaba wake," alionya. Alisema wizara yake itafanya kazi kwa karibu na makamanda wa kaunti ili kutia nguvuni na kiadhibu wanaoharibu misitu.

Dkt Matiang'i alisema hayo wakati akizindua kampeni ya upanzi wa miti nchini, Kenya Greening, katika Gereza la Ruiru, kaunti ya Kiambu. Kampeni hii inaongozwa na shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) kwa ushirikiano na idara ya magereza Kenya, ambapo wanalenga upanzi wa miti milioni 50 kote nchini kufikia Mei 2019.