Nilimtimua Visita kwa kukosa kumakinika kimatamshi - Refigah

Refigah

Yusuf Noah al-maarufu Refigah, afisa mkuu mtendaji wa Grandpa Records. Picha/PAULINE ONGAJI 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Thursday, January 5  2017 at  16:31

Kwa Mukhtasari

BAADA ya kimya cha muda kuhusiana na nini hasa kilichomfanya produsa na msanii Nickson Wesonga al-maarufu Visita kuondoka lebo ya Grandpa Records, mmiliki wa studio hiyo Refigah ameamua kuzungumzia suala hilo.

 

Kulingana na Refigah, aliamua kumuonyesha lango mwanarepa huyo kufuatia mazoea yake ya kurusha cheche za matusi kupitia mitandao ya kijamii na mahojiano na vyombo vya habari.

Inasemekana kuwa uamuzi wa kuamuachisha kazi ulijiri mwezi Septemba 2016 na hivyo kumaliza huduma yake ya miaka mitatu.

“Sikutaka kuzungumzia suala hilo hadi alipoelekea kwenye mtandao wa kijamii na baada ya kupokea simu kadha kuhusiana na matamshi yake ya kila aina,’’ alisema.

Kadhalika Refigah amefichua kuwa alichukua hatua hiyo baada ya produsa huyo kukosa kutoa huduma zake kuambatana na mkataba wao ambapo alikuwa akipokea simu kutoka kwa wasanii waliodai kuwa kazi zao hazijakamilishwa.

Lakini wakati mmoja Visita anayesemekana kuanzisha studio yake pindi baada ya kuondoka Grandpa, alimshutumu Refigah kwa kumtumia kujitajirisha na hata kudai kuwa ana deni lake.

Visita anatambulika kwa kazi yake murwa huku akiwahi fanyia kazi vibao kama vile Dumbala, Fimbo na Mapepo miongoni mwa nyimbo zingine.