http://www.swahilihub.com/image/view/-/4391086/medRes/1937408/-/7q38i7/-/orierogo.jpg

 

Orie Rogo Manduli: Kitambaa maridadi kichwani ni kitambulisho tosha

Orie Rogo Manduli

Orie Rogo Manduli. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, April 13  2018 at  07:59

Kwa Muhtasari

Orie Rogo Manduli watakuambia ni mwanamama Mkenya ambaye ana mazoea ya kujifunga kichwani kitambaa cha kupendeza; bora tu kiwe kirefu.

 

WANAOMTAMBUA Orie Rogo Manduli watakuambia ni mwanamama Mkenya ambaye ana mazoea ya kujifunga kichwani kitambaa cha kupendeza; bora tu kiwe kirefu.
Yuapenda sana vazi la 'Kitenge'.

Baadhi ya watu watakuambia Orie Rogo ni kama kinanda akianza kuongea - itakubidi unyamaze akuhutubie.

Swahilihub iliyapata maoni katika mtaa wa Thika baada ya kutagusana na Orie Rogo Manduli jijini Nairobi katika Jumba la Loita.

Hapo alikuwa ameenda kutengenezwa nywele na kwa uhakika, ana ufahamu mzuri na yuakumbuka vizuri kwa sababu licha ya kuwa mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa ni miaka minane iliyopita, alimtambua mwandalizi wa makala haya.

Alikuwa mkurugenzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Ni mwanamke thabiti kimawazo na asiyeogopa kukabiliana na hali yoyote ile kwa kuwa wakati miungano ya mashirika hayo yasiyo ya kiserikali ililenga kumng’atua kutoka afisini, alikatalia huko na akawa wa kulala huko afisini ili asiondoke!

Ana maoni thabiti ya kisiasa na kijamii kuwa ili uaminike kuwa kiongozi wa taifa au katika wajibu mwingine wa umma, ni lazima uwe na familia.

Anasisitiza kuwa hufai kuchaguliwa kuwa kiongozi hapa nchini au kwingineko duniani ukiwa huna familia kamili na halali iliyo pia na watoto ikiwezekana.

“Utakuja kutuambia utatusimamia kwa lipi ikiwa wewe mwanamume huna mke, huna nyumba na huna watoto?” auliza Manduli.

Manduli anasema kuwa rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron, 39, ni mfano bora zaidi wa “jinsi ya kuchaguliwa kwa wasiofaa kamwe kuongoza katika jamii”.

Anasema kuwa Macron ameoa mwanamke mwenye umri wa miaka 64 “na hawana uwezo wowote wa kupata watoto katika ndoa yao ya kushangaza, sio ya
kushangaza, ya kuchukiza…”

Anasema hali ni iyo hiyo hapa nchini Kenya ambapo ili uaminike kuwa unaweza ukaongoza, unafaa uwe na familia iliyo habari wazi kwa kila mtu na ambayo iko na uthabiti wake.

“Tukiangalia familia yako, tupate ushahidi kuwa umejiweza kiuongozi katika boma lako. Sio uwe mkora mkora au kiruka njia mtaani na bado unataka kutuongoza. Uongoze familia yako kwanza, kisha utupe ushahidi kuwa unaweza ukatuongoza,” asema Manduli.

Anaongeza kuwa imekuwa 'mila na desturi' katika bara la Afrika kuwa ni lazima kiongozi awe mtu wa familia thabiti na halali.

“Hii elimu ya kisasa na 'Uzungu' mwingi ambao tumejitwika katika bongo zetu ni kichocheo kikuu cha kusambaratisha mtazamo wetu kuhusu uongozi. Ni msimamo wangu wa dhati usiobatirika kuwa ni lazima kiongozi atupe ushahidi wa kuwepo kwa familia yake,” asema.

Familia yake

Kuhusu familia yake, anasema kuwa kuwa si domo tu, bali yeye kwa matendo ni mwanamke ndani ya familia iliyo wazi.

Anasema kuwa ndoa yake ya kwanza ilimwingiza ufahamu mkubwa wa kimaisha. Ilivunjika kupitia talaka.

“Nilikuwa mchanga sana nilipojipata katika ndoa hiyo. Sikuwa na kazi wala pato lolote na nilikuwa wa kutegemea bwanangu anisaidie kimaisha. Hakuwa akiona manufaa ya kusaidia mke na majukumu ya kulea watoto yaliachwa mikononi mwangu nikiwa mwanamke,” asema.

Alitoka katika ndoa hiyo akiwa na watoto watatu wasichana.

Muda baadaye alitua mikononi mwa Misheck Norman Manduli kama mume mpya na ambaye alikuwa kutoka himaya ya ukoo wa Lunda kutoka taifa la Zambia.

Anasema alipata raha katika ndoa hiyo kwa kuwa ukoo huo ulimhitaji awe mwanamke wa kweli ambapo hata akisalimiwa na mumewe ni lazima yeye kama Orie Rogo anayekiri kujivunia kuwa Mluhya na Mkenya sawia na Mwafrika aliye na bongo la kimataifa, awe amepiga magoti.

“Nikimpa chakula, magoti. Chai, magoti. Kuomba kitu, magoti. Si nilipiga magoti jameni!” asema.

Alipata mtoto mvulana katika ndoa hiyo iliyoisha kufuatia kifo cha mume huyo mwaka wa 2003 na hadi leo hii, amebakia bila kutaka kuchumbiwa.

Anasema kuwa anapenda siasa na katika uchaguzi mkuu wa 2017 alipania
kuwania uwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Trans-Nzoia lakini mawimbi nyanjani yakamlemea.

Hata hivyo, anasema kuwa hajaishiwa na ya kumpa tabasamu maishani ambapo anasema kuwa kusoma kwa upana majarida na vitabu ni uraibu wake.

“Hicho ndicho kiini changu cha kubakia mwerevu na mjanja maishani,” asema akichekacheka.

Anasema kuwa muziki wa Rhumba na ule wa Salsa ni tosha kwake.

Anasema kuwa muziki ni ule unaochumbia hisia za mwili na kusisimua ubongo kiasi kwamba unaweza ukalia ukiusikiza na ukiunengulia kiuno.

Kimavazi, anakuambia mwanamke ni kujitunza na ikiwa huna ufahamu kuwa sura ya mwanamke ni pambo, basi umwendee akakufafanulie maana ya mtazamo huo wake.

Anasema kuwa ako na manguo ambayo hawezi akahesabu kwa kuwa ni mengi, viatu wachana na kuhesabu na jinsi anavyotambua ya kuvaa leo, achana na maswali kama hayo kwa kuwa hata yeye hajui ila tu hujipata amejipata amevalia umwanavyo kwa wakati huo unamwona.

Anasema anapenda kujipikia chakula chake na kamwe hapendi kuhamishia majukumu yake ya pale nyumbani kwa yaya.

Akiwa msichana mwenye umri wa miaka 16, alitawazwa kuwa bingwa wa warembo nchini katika safu ya Utalii na mwaka wa 1974, akaibuka mwanamke wa kwanza
Mwafrika kumaliza mashindano ya mbio za magari ya World Circuit Safari Rally.

Ni mwanamke wa kwanza nchini Kenya kuongoza afisi ya Kenya Non-Governmental Organisation Council (NGO Council).

Anasema hisia zake za uchumba bado ziko hata akiwa wa miaka ambayo ukimuuliza mtakosana.

Kwa kweli, kuongea na Orie Rogo Manduli ni raha, mama mkarimu na mwenye roho inayoweza ikasemwa ni ya dhahabu.