http://www.swahilihub.com/image/view/-/4926220/medRes/2037617/-/yh9ingz/-/lugola.jpg

 

Polisi walarushwa kuchunguzwa

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola 

Na Shaaban Ndyamukama, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  15:02

Kwa Muhtasari

Watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

 

 

Ngara. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewashukia baadhi ya askari polisi na maofisa uhamiaji akiwatuhumu kudai na kupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali wakiwamo raia wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha sheria.

Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Ngara juzi, Lugola alisema uchunguzi wa kina unaendelea kuwabaini wahusika na kuonya watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

“Baadhi ya askari polisi na uhamiaji huwakamata watuhumiwa wakiwamo raia wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha sheria na kuwatoza fedha kwa njia ya rushwa badala ya kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria,” alisema.

Lugola alisema watendaji hao wa vyombo vya ulinzi na usalama hufikia hatua ya kushikilia mali za raia hao wa kigeni na watuhumiwa wengine wa uhalifu kama dhamana ya kupewa rushwa baadaye.

Alisema baadhi ya askari hao hutumia vitisho kufanikisha rushwa na wengine wanaokamatwa huangaliwa kwa maumbile na sura zao badala ya kuzingatia sheria na kanuni.

Akizungumzia huduma ya idara ya Zimamoto, Lugola alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kununua vifaa vya zimamoto kwenye shule zote za msingi na sekondari pamoja na vituo vya umma vya huduma ili kuwahakikishia wananchi usalama wakati wa matukio ya ajali za moto.

Awali, Mbunge wa Ngara, Alex Gashaza aliwasilisha kilio cha wapiga kura wake akisema wananyanyaswa na askari polisi na wa uhamiaji wakituhumiwa kuwa si raia kwa kuangalia maumbile na sura zao.

“Wakazi wa Ngara wana muingiliano na baadhi undugu wa damu na wenzao wa nchi jirani kuanzia kwenye biashara, sanaa, utamaduni, mila na desturi, lakini hii haiwaondolei haki ya kuwa raia wa Tanzania kisheria. Tunaomba suala hili lishughulikiwe,” alisema.