http://www.swahilihub.com/image/view/-/4930264/medRes/2220969/-/12nia5n/-/tunuku.jpg

 

Rais Shein atunuku nishani 112

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akimtunuku Nishani ya Utumishi uliotukuka Bi Fatma Mohamed Said katika Hafla ya Kutunuku Nishani iliofanyika katika Viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar. Ikiwa ni shamra shamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar 

Na Haji Mtumwa, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  10:19

Kwa Muhtasari

Waliotunukiwa kati yao 40 ni marehemu na 72 wako hai

 

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewatunuku nishani ya mapinduzi, nishani ya utumishi uliotukuka na nishani ya ushujaa viongozi, watumishi wa umma, maofisa na wapiganaji wa idara maalum za Serikali na wananchi mbalimbali.

Hafla ya kutunuku nishani hizo ilifanyika juzi katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa, wananchi na baadhi ya viongozi wakuu wastaafu akiwamo Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Kutunukiwa nishani hizo ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12 Pemba.

Katibu mkuu ofisi ya Rais, Salum Maulid Salum jana alisema katika hafla hiyo, Rais Shein ametunuku nishani ya mapinduzi 45, nishani ya utumishi uliotukuka 53 na nishani ya ushujaa 14.

Alisema jumla ya watu waliotunukiwa nishani hizo ni 112 ambao kati yao 40 ni marehemu na nishani zao zilipokelewa na wawakilishi wao na 72 wako hai ambapo walipokea wenyewe au kwa niaba yao.

Salum alisema watunukiwa wote sifa zao zimekidhi matakwa ya nishani hizo, ambapo nishani ya mapinduzi hutolewa kwa mtu ambaye aliasisi au alishiriki au kuyatukuza na kuyaenzi mapinduzi hayo.

Aidha, Rais Shein ametoa nishani ya mapinduzi kwa timu za mpira na vikundi vya uhamasishaji ikiwamo timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes ya mwaka 2017, timu ya Taifa ya mpira wa ufukweni ya 2017, bendi ya Safari Trippers na kikundi cha taarab cha Siti Binti Saad.