http://www.swahilihub.com/image/view/-/1719076/medRes/332706/-/q9p9ng/-/BDUHURU3001B.jpg

 

JAMVI: Uhuru atahimili mawimbi ya wapinzani kujitenga?

Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta. Picha/DIANA NGILA 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Sunday, November 12  2017 at  15:25

Kwa Muhtasari

TANGAZO la baadhi ya viongozi wa uliokuwa mkoa wa Pwani la kutaka kujitenga limeibua mdahalo mkali kwa mara nyingine, huku wachanganuzi wakionya kuwa huenda likawa jinamizi kwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.

 

Ingawa muungano wa NASA ulikuwa umetoa pendekezo sawa na hilo, kauli za magavana Ali Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi) pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo mapema wiki hii ndizo zimeonekana kuupa mashiko mdahalo huo.

Wawili hao wanadai chini ya mpangilio wa sasa, ambapo rais huchaguliwa moja kwa moja na wananchi, ni vigumu sana kwa jamii zenye idadi ndogo ya watu kupata urais.

“Katika hali ya sasa, ni vigumu sana kwa Mpwani na jamii zingine nchini kupata urais. Msukumo wetu wa kujitenga ni kuhakikisha wananchi wetu wanapata haki,” alisema Bw Kingi.

Kwa hayo, wachanganuzi wanasema kuwa kinyume na mazingira ya awali, huenda pendekezo hilo likapata mvuto miongoni mwa wananchi, kwa kuwa wengi sasa wana ufahamu mkubwa kuhusu siasa za nchi.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Godfrey Sang asema hali ya sasa haiwezi kulinganishwa na miaka ya sitini ama sabini, wakati midahalo hiyo ilionekana kusukumwa na sababu za kisiasa.

“Watu wameerevuka sasa, hivyo huwezi kuoanisha ufahamu uliokuwepo katika miaka hiyo na ilivyo sasa. Watu wanajua mengi kupitia mitandao na mpenyo mkubwa wa vyombo vya habari,” asema Bw Sang.

Pendekezo la kwanza la kujitenga lilianza mnamo Mei 1963, baada ya jamii ya Somali katika eneo la Kaskazini Mashariki kuanza harakati za kujitenga. Eneo hilo lilikataa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Mei 1963, uliowezesha Kenya kujipatia uhuru.

Hilo ndilo lilichangia kutokea kwa “Vita vya Shifta” ambapo wanamgambo kutoka Somalia walikuwa wakilisaidia eneo hilo kuendeleza ajenda hiyo, lakini likashindwa kwa pamoja na wanajeshi wa Kenya kwa ushirikiano na wenzao kutoka Uingereza.

Viongozi wengine ambao wametoa mapendekezo kama hayo ni aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Ford Asili, Kenneth Matiba na Rais Mstaafu, Mwai Kibaki, waliotaka eneo la Kati kujitenga kutokana na kile walichotaja kama “kutengwa kwa jamii ya Agikuyu” na serikali ya Rais Mstaafu Daniel Moi.

Na ikizingatiwa kwamba mchakato huo huhitaji mikataba mingi ya kitaifa na kimataifa, wachanganuzi wanaonya kuwa haupaswi kupuuziliwa mbali hata kidogo.

Migawanyiko

“Pendekezo hilo halipaswi kuchukuliwa kwa urahisi, hasa baada ya kutolewa na kinara wa NASA Raila Odinga. Ingawa mtazamo wake ni wa kisiasa, unaashiria migawanyiko mikubwa ya kikabila na kisiasa ambayo imeibuka siku za hivi punde,” asema Barack Muluka, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

Kulingana na Bw Muluka, wakati umewadia kwa Rais Kenyatta kubadili msimamo wake mkali, ili kuzima hisia za kutengwa kwa baadhi ya maeneo ya nchi, hasa lile la Luo Nyanza.

“Kuna hisia ya kihistoria kwamba babake Bw Kenyatta, Mzee Jomo Kenyatta alilitenga na kulidhulumu eneo hilo kisiasa, hali ambayo inaonekana kujirudia kwa sasa, hasa kutokana na dhuluma za polisi dhidi ya jamii ya Waluo. Hili ni suala zito ambalo huenda likalipuka, na kuathiri uongozi wake,” aonya Bw Muluka.

Katika mdahalo wa sasa, pendekezo kuu lililopo ni kugawanywa kwa Kenya mara mbili; Jamhuri ya Kati ya Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kenya.

Jamhuri ya Kati ya Kenya inaashiria maeneo ya Kati,  Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki (yanayoegemea mrengo wa Jubilee) huku Jamhuri ya Watu wa Kenya ikiyajumuisha maeneo ya Nyanza, Magharibi, Ukambani na Pwani (yanayoegemea mrengo wa NASA).

Katiba si suluhu

Kulingana na Bw Kiprotich Mutai, ambaye hufuatilia siasa za nchi kwa karibu, Katiba ya sasa si suluhu kwa changamoto ambazo zimekuwa zikiizonga nchi, hata baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi.

“Tunapaswa kujiuliza tatizo kuu linalotukumba kwani katiba inaonekana kukosa kuwa kiunganishi kikuu cha nchi. La sivyo, mdahalo huo utashika kasi, kiasi cha kufikia kiwango cha kimataifa,” asema Bw Mutai.

Bw Mutai anaonya kuwa, juhudi za eneo la Catalonia kutaka kujitenga na Uhispania, zinapaswa kuwa kifungua macho kwa viongozi nchini kushusha misimamo yao mikali ya kisiasa na kuangazia changamoto zilizopo kwa njia ya utulivu.

“Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wanapaswa kuzingatia miito ya wadau mbalimbali kushirikiana ili kuangazia masuala kwa pamoja,” asema Bw Mutai.

Asema majadiliano hayo yatazima hisia za kutengwa na kudhulumiwa kwa jamii hiyo, sawa na ngome zingine za NASA, zinazodai kutengwa na uongozi wa Jubilee.

Lakini licha ya miito hiyo, Bw Kenyatta amemlaumu Bw Odinga kwa kutumia kisingizio hicho kutaka kupata mamlaka kwa njia ya mkato.