Sakata la Profesa Assad lisiathiri Katiba

Imepakiwa - Thursday, April 4  2019 at  09:00

 

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha azimio kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad baada ya kumtuhumu katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa akisema kutofuatiliwa kwa ripoti zake ni “udhaifu wa Bunge.”

Azimio hilo lilifikiwa na Bunge juzi baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu Profesa Assad.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakalasa aliliambia Bunge kwamba CAG alikiri kutumia neno “udhaifu wa Bunge” lakini hakujutia kauli yake wakati alipohojiwa na kamati hiyo.

Mwakalasa alisema walipomhoji kwenye kamati kuhusu maana ya neno udhaifu kwa wananchi wa kawaida na watu ambao taaluma yao siyo wahasibu au wakaguzi, alijitetea kuwa yeye alikuwa na maana ya upungufu na si vinginevyo.

Siyo nia yetu kuendeleza mjadala kuhusu sakata hilo, tunafahamu Bunge ni mhimili unaojitegemea na una mamlaka yake kisheria katika utendaji wa kazi.

Hata hivyo, azimio hilo la Bunge limeonekana kuleta utata wa kikatiba na hata CAG mstaafu Ludovick Utouh, amekaririwa akisema itakuwa tatizo.

Kila mtu anafahamu Bunge letu ni chombo kinachowakilisha wananchi katika kusimamia utendaji wa Serikali kwa kuhoji masuala kadhaa na kutunga sheria.

Bunge limetoa azimio hilo ikiwa ni siku saba tangu CAG akabidhi ripoti mpya kwa Rais John Magufuli ambaye aliwahi kusema Serikali itaendelea kufanya kazi na ofisi hiyo. Katiba yetu inaeleza majukumu ya CAG na namna anavyohusika katika kuidhinisha fedha kutoka kwenye Hazina kuu ya Serikali, na pia ripoti yake ndiyo inayotumiwa na Bunge kuisimamia vizuri Serikali.

Siyo dhamira yetu kubeza azimio lilitolewa na Bunge dhidi ya CAG, bali tunaamini wabunge walikuwa na uwezo wa kufanya zaidi kwa kuangalia athari za mbali katika uamuzi wao.

Tunajua Bunge lina heshima yake na si vizuri wala hairuhusiwi kutoa kauli za kudhalilisha madaraka yake, lakini pamoja na mamlaka waliyonayo wabunge pia wana uwezo wa kubadili uamuzi wao na kuzingatia sintofahamu inayoweza kujitokeza kikatiba.

Si vibaya katika kuleta mshikamano na mustakabali bora zaidi katika suala hili Bunge letu badala ya kuchukua hatua za lililoyazimia, likaamua kumsamehe na kwa kufanya hivyo wala halitakuwa limejishushia hadhi yake.

Kuna wakati Samwel Sitta wakati akiwa Spika alisema ameamua kumpuuza mbunge aliyeonekana kwenda kinyume na maadili, lakini akawaomba wabunge wamshauri kwa lengo la kumrejesha kwenye maadili mema.

Tunaamini Bunge letu bado lina nafasi ya kurejea uamuzi wake dhidi ya CAG kwa kuangalia athari zinazoweza kulikumba Taifa kikatiba iwapo litajitenga naye.

Kila mtu anafahamu kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali na ripoti ya CAG ni kitendea kazi muhimu cha wabunge katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa na wananchi. Kwa kuamini Bunge letu ni sikivu na lipo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, ni vyema likaepusha mgogoro wa kikatiba nchini unaonukia kupitia suala hili.