http://www.swahilihub.com/image/view/-/5053068/medRes/2299882/-/k5nty2z/-/sara+pic.jpg

 

Sarah Mwandishi wa Sheria Mkuu anayeamini Mwanamke ni umakini

Na  Maura Mwingira

Imepakiwa - Tuesday, April 2  2019 at  13:07

 

’Ilikuwa usiku wa kama saa tatu hivi nilipopigiwa simu na Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo akiwa Dk Asha-Rose Migiro. Akanieleza kwamba nimeteuliwa kuwa mwandishi mkuu wa Sheria na hivyo nitafute suti maana nilikuwa natakiwa kuapishwa asubuhi yake.

“Kwa kweli nilipata mshtuko, si jambo ambalo nilikuwa nimelitarajia au hata kulifikiria. Baada ya mazungumzo yale, nikaanza kujiuliza usiku ule suti ningeipata wapi. Lakini kwa kuwa mimi ni mwanasheria nilijua sitakosa suti katika kabati langu angalau inayofaa kwa ajili ya tukio la kuapishwa asubuhi yake, kwa hiyo nikaaanza kutafuta suti.”

Hivyo ndivyo Sarah Barahomoka alivyopata habari ya uteuzi wake, uteuzi ambao ulimfanya kuwa mwanamke wa kwanza tangu uhuru kushika wadhifa wa mwandishi wa Sheria Mkuu. Kabla yake wamepita waandishi wakuu saba - wote wanaume.

Sarah mwenye hulka ya kuongea kwa utaratibu na kwa kujiamini, sasa anajiandaa kustaafu Julai mwaka huu, baada ya kuwa mtumishi wa umma kwa miaka zaidi ya miaka 30.

Anasema alipoanza kazi mwaka 1986 akiwa wakili wa Serikali daraja la pili, hakuanza moja kwa moja na kazi ya uandishi wa sheria, bali aliajiriwa kama mwendesha mashtaka jukumu analosema alilitekeleza kwa miaka sita.

Ni katika ratiba zake za kwenda mahakamani takriban kila siku, ndiko kulikoibua hamu na shauku ya kutaka kuwa mwandishi wa sheria .

‘’Nikiwa mahakamani na nje ya mahakama, nilikuwa nasikiliza na kufuatilia kwa makini namna ambavyo wanasheria wenzagu walivyokuwa wanavichambua vifungu vya sheria, namna walivyokuwa wakiwasilisha hoja zao na mpangilio wa hoja hizo. Nilivutiwa lakini kubwa zaidi sheria zile zilizokuwa zinachambuliwa zilikuwa zimeandikwa na wanasheria ninaowafahamu na ninafanya nao kazi,’’ anasema.

Anasema akazidi kujenga ari ya kujifunza na kufuatilia zaidi kwa kusoma mafaili ya wenzake, kwa kuangalia namna gani hoja zilikuwa zinajengwa, namna gani ushauri wa kisheria unavyoandikwa pamoja na jinsi ya kufanya utafiti kisheria.

Kiigizo chake

Baada ya miaka sita katika uendeshaji wa mashtaka, aliomba kuhamia divisheni ya uandishi wa sheria, huku akivutiwa na aliyekuwa Mwandishi Mkuu wa Sheria kipindi hicho Rushagara Sigflid. Kilichomvutia ni namna ya uandishi wake, ujengaji hoja na umakini katika kazi

‘’ Kupitia kwake nilianza kujifunza kwa bidii, nilikuwa nashinda maktaba, kusoma, kufanya utafiti na kufuatilia kazi za wengine pamoja na kuwauliza. Kwa namna hii niliweza pia kugundua uandishi mzuri na pia kuona upungufu wa wengine, ‘’ anasema na kuongeza:

‘’Baada ya miaka mitatu ya kuwa mwandishi wa sheria nilikuwa nimekwenda mbali sana, niliendelea kufanya kazi kwa bidii sana na nilikuwa napewa kazi ngumu sana na hata nilipokwenda kumuuliza bosi wangu au kutaka ufafanuzi alikuwa akiniambia wewe nenda kafanye. ‘’

Safari ya uteuzi

Uteuzi wa kuwa Mwandishi Mkuu wa Sheria haukuja ghafla, unaweza kusema ulikuwa ni mlima mrefu wa kuupanda ili kufikia kileleni. Anasimulia kuwa bosi wake aliteuliwa kuingia katika Tume ya Warioba na alikuwa huko kwa miaka miwili. katika kipindi hicho alipewa jukumu la kukaimu nafasi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria

‘’Niseme basi kama kuna kipindi nilifanya kazi sana sana tangu nilipoajiliwa basi ni kupindi hiki. Hii ina maana wakati bosi wangu yupo nilikuwa najua kuwa kuna mtu juu yangu, lakini sasa mimi ndiyo kaimu wenzangu walikuwa wananiangalia mimi na kazi zao zilikuwa zinakuja kwangu kama mtu wa mwisho,’’ anaeleza.

Mwanamama huyu apendaye kumtanguliza Mungu katika mambo yake anasema, alilazimika kuwa makini kuifanya kazi hiyo nyeti ili kuepuka makosa ambayo baadhi ya watu pengine wangetaka kuyanasibisha na jinsi yake.

Anaongeza kuwa umakini unahitajika kwa kila mwanamke popote alipo kwa sababu wanawake wana majukumu mengi ya kikazi na ulezi wa familia tofauti na wanaume.

Je, aliwahi kubaguliwa kwa kuwa ni mwanamke? Sarah anasema:

“ Kwa kweli sijawahi kukumbana na adha ya kubaguliwa au kunyanyapaliwa kwa sababu tu ni mwanamke, Nchi yetu na Serikali yetu imepiga hatua kubwa sana na ya kujivunia katika hili. Wanawake wengi wamepewa nafasi za uongozi za juu na uamuzi. Kwangu mimi na kwa wanawake wote kinachotakiwa ni kazi, uzalishaji, nidhamu, unadhifu na kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kwa wakati.’’

Kazi ya uandishi wa sheria

Wengi wanadhani uandishi wa sheria ni sawa na uandishi wa aina yoyote ile kama vile uandishi wa habari au uandishi wa vitabu. Kimsingi, ni kazi ngumu inayohitaji uangalizi makini.

Mwandishi wa sheria pamoja na mambo mengine anahitaji kuzingatia Katiba na Sheria nyingine ambazo ni nyingi, ni taaluma ambayo ina miiko yake na maadili yake.

‘’Bahati mbaya katika vyuo vikuu vyote vinavyofundisha sheria, hakuna hata kimoja kinachofundisha uandishi wa sheria. Kwangu mimi kazi ya uandishi wa sheria umo ndani ya damu yangu; ni kazi ninayoipenda kutokana na uhalisia wake kwamba inakuwa ni kumbukumbu ya kudumu,’’ anasema.

Maisha baada ya kustaafu

Kama alikuwa mwandishi bila shaka alikuwa msomaji. Sarah anasema ataviendeleza vyote hivyo akiwa katika maisha mapya ya kama mstaafu.

‘’Nitatumia pia muda wangu kusoma vitabu vingi zaidi. Ninapenda kusoma vitabu vyenye maudhui mbalimbali vikiwamo vya dini na vile vyenye kutia moyo,’’ anaeleza.