http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885710/medRes/1607649/-/14xjsr6z/-/titus.jpg

 

Serikali inavyopoteza mabilioni migodini

Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo 

Na Kelvin Matandiko, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  15:40

Kwa Muhtasari

Serikali imekuwa ikipata mgawo mdogo wa kodi ya mapato kutoka kwa wawekezaji

 

 

kmatandiko@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali inapoteza fursa ya kukusanya kodi ya mabilioni ya fedha kama kodi kutokana na gharama kubwa za uzalishaji wa umeme wa mafuta katika migodi ya dhahabu, Mwananchi limebaini.

Uchambuzi wa Mwananchi katika migodi miwili mikubwa umebaini kuwa kushindwa kwa Shirika la Umeme (Tanesco) kusambaza umeme katika migodi hiyo kumeiongezea gharama za uzalishaji kwa zaidi ya maradufu.

Ongezeko la gharama za uzalishaji linamaanisha kuwa Serikali imekuwa ikipata mgawo mdogo wa kodi ya mapato kutoka kwa wawekezaji kwa sababu ya gharama kubwa zinatokana na manunuzi ya mafuta kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Serikali hupata mgawo wa faida baada ya mwekezaji katika mgodi husika kutoa gharama za uzalishaji.

Gharama ndogo za uzalishaji humaanisha gawio kubwa kwa Serikali linatokana na kukua kwa faida ya uwekezaji.

Kwa mfano, kampuni ya Stamigold inayomiliki mgodi wa Biharamulo uliopo mkoani Kagera inatumia Sh900 milioni kununua lita 360,000 za mafuta ya dizeli kila mwezi zinazozalisha megawati 2.25 za umeme.

Kama mgodi huo ungekuwa umeunganishwa kwenye gridi ya Taifa ungetumia wastani wa Sh350milioni kila mwezi na kuokoa Sh550 milioni, sawa na asilimia 60 ya gharama unazotumia.

Takwimu hizi zinahusisha uzalishaji kuanzia mwaka 2013/14 wa kampuni ya Stamigold iliyo chini ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

Kampuni nyingine ni Geita Gold Mine (GGM) iliyo chini ya kampuni ya AngloGold Ashanti ambayo hutumia takriban Dola za Marekani 3.2 milioni (sawa na Sh7 bilioni) kununua lita milioni 4.2 za mafuta ya dizeli kila mwezi zinazozalisha megawati 25.

Kama mgodi huo ungekuwa unapata umeme moja kwa moja toka gridi ya Taifa, ungeweza kupunguza bajeti ya mafuta kutoka Sh7bilioni hadi wastani wa Sh2.8bilioni kila mwezi.

Ukizingatia ukweli kwamba mgodi wa GGML ulianza rasmi uzalishaji mwaka 2000, gharama kubwa za uzalishaji zimeathiri karibu migodi yote ambayo haijaungwa kwenye gridi ya Taifa.

Mratibu wa shughuli za uboreshaji biashara wa mgodi wa Stamigold, Godfrey Rweyemamu anasema Sh550 milioni ambazo kampuni yake ingeweza kuziokoa kwa kutumia umeme wa Tanesco zingesaidia upanuzi wa shughuli za uzalishaji mgodini, kuongeza mapato ya Serikali na mtaji wa kampuni hiyo.

Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo ana maoni kuwa hali hiyo inatoa fursa kubwa kwa Tanesco kufanya biashara ya umeme kwenye migodi.

“To me, it’s an opportunity (kwangu, hiyo ni fursa), nadhani walitakiwa [Tanesco] hata kukopa fedha,” anasema.

Mafuta na mazingira

Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Madini na Nishati Tanzania (TCEM), Gerald Mtulia alisema uzoefu unaonyesha matumizi ya mafuta ya dizeli kuzalishia umeme huharibu mazingira, kuinyima Serikali fursa ya kupata kodi kubwa na Tanesco kuongeza mapato.

Mtafiti Mwandamizi wa Uchumi kutoka Taasisi ya Utafiti Repoa, Dk Abel Kinyondo alisema Stamigold ilitakiwa kuingia makubaliano ya kibiashara na Tanesco kama ilivyofanyika katika migodi ya Kampuni ya Acacia.

“Migodi ya Acacia ilikuwa inatumia mabilioni kuzalisha umeme wake lakini wakaamua kununua vifaa vyote vinavyohitajika kisha wakaingia makubaliano na Tanesco ili waunganishwe katika gridi ya Taifa, model (njia) hii ilitakaiwa kufanyika pia katika migodi yote ikiwamo GGM na Stamigold,” alisema Dk Kinyondo.

Hesabu za Stamigold

Wataalamu wanasema takriban Sh16.8 bilioni ilizokosa Tanesco Stamigold, zingesaidia kwa kiasi kikubwa ufanikishaji wa mradi wa kuunganisha umeme kwa gridi ya Taifa mgodini hapo.

Udhaifu na suluhisho

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Umeme Jadidifu nchini (Tarea), Godwin Msigwa anasema migodi inaweza kupunguza zaidi gharama za uzalishaji umeme endapo itaingia kwenye miradi ya umeme wa jua.

Anatoa mfano wa kiwanda cha Azam kilichopo barabara ya Mkuranga kilichofanya uchambuzi wa gharama za umeme wa jua na vyanzo vingine na kubaini kuwa umeme jua ni rafiki zaidi.

“Kila project (mradi) inatofautiana kutokana na mazingira. Kwa mfano ardhi ikoje na nguvu ya mionzi ya jua katika eneo husika lakini gharama ni ndogo sana ukilinganisha na bajeti ya mafuta,” anasema Msigwa.

Hofu ya umeme wa Tanesco

“Kumbuka tu kwamba supply (usambazaji) ni kitu kimoja, lakini stability (uhakika) ni kitu cha pili, sisi tunafanya kazi 24 hours (saa 24). Umeme wa Tanesco ukikatika mara moja tu wakati wa uzalishaji, hasara yake ni kubwa kuliko matumizi ya mitambo ya dizeli,” anasema meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa GGM, Tenga Tenga

Hata hivyo, taarifa ya GGM ya Oktoba 9, inasema mgodi huo unatarajia kupunguza zaidi gharama za uendeshaji, kuongeza mapato na mrabaha wa Serikali kutokana na mradi mpya wa megawati 40 za umeme utakaoanza kutumika kwenye uchimbaji.

Serikali na wenye migodi

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo anasema katika kipindi cha mwaka mmoja wizara hiyo tayari imekwishafanya majadiliano ya ndani na Wizara ya Nishati ili Tanesco iweze kupeleka umeme katika migodi yote.

“Kuna mawasiliano ya ndani yanaendelea na siyo kwa migodi mikubwa tu hata wachimbaji wadogo wanahitaji umeme wa Tanesco,” anasema.

Nyongo ambaye pia ni mbunge wa Maswa Mashariki anakiri kuwa gharama za uzalishaji katika migodi zimekuwa zikiigharimu Serikali katika ukusanyaji wa mapato.

“Hizi gharama za uzalishaji zinapokuwa kubwa zinaleta shida kwenye corporate tax (kodi ya mapato) ya asilimia 30. Gharama ikiwa kubwa, basi faida itakuwa ndogo na itaathiri kodi yetu.”

Ufumbuzi Tanesco

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Dk Alexander Kyaruzi anasema wanatamani kufikisha huduma ya umeme kwa kampuni na Watanzania wote, lakini wanakabiliwa na uhaba wa bajeti ya uendeshaji wa miradi mikubwa.

“Sisi tunaiangalia nchi kwa ujumla wake. Kigoma hatujapeleka gridi, bado wanazalisha kwa mafuta lakini changamoto ni kwamba hatujawa na pesa, tunazitafuta tukizipata tutapeleka huduma, na kwa GGM watapelekewa umeme hivi karibuni, Geita itapata umeme mwingi,”anasema.

Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa Tanesco anayeshughulikia uwekezaji na miradi, Khalid James anasema uchelewashaji wa gridi ya Taifa katika maeneo ya migodi kadhaa umechagiwa na ukosefu wa miundombinu.

Anasema siku chache zijazo wanatarajia kuanza mradi wa kusambaza umeme wenye msongo wa 220KV kutoka Bulyanhulu hadi Geita ambao ni umbali wa kilomita 55.

Mradi huo utasafirisha megawati 460 na kati ya hizo, megawati 80 zitatengwa kwa ajili ya Mkoa wa Geita ikiwamo GGM.

Mradi huo utakaochukua miezi 17 kukamilika kwa gharama ya Dola za Marekani 23 milioni (zaidi ya Sh50.6 bilioni), ulianza miaka kadhaa iliyopita lakini changamoto ilikuwa ni bajeti kwa ajili ya utekelezaji.