Serikali isikilize kilio cha biashara kufungwa

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  11:04

 

Jana tulichapisha habari ikieleza namna baadhi ya wabunge walivyochachamaa, wakiitaka Serikali kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Ni kweli biashara nyingi zinaanzishwa tena kwa kiwango kikubwa kama Serikali inavyosema, lakini ni kweli pia baadhi ya biashara zinafungwa.

Takwimu kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji zinaonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Aprili, biashara zilizofunguliwa zilikuwa 147, 818 huku 16, 252 zikifungwa. Idadi hii ya biashara zinazofungwa siyo haba, ndiyo maana baadhi ya wabunge hawakusita kuonyesha hisia zao kuhusu ukweli ulivyo.

Inawezekana ikawa ni aina ya biashara, uhaba wa wateja, lakini kilio kikubwa cha kufunga biashara kwa walio wengi kiasi cha baadhi kukimbia hata nchi, ni changamoto ya mazingira ya ufanyaji biashara.

Kilio cha wafanyabiashara kipo katika maeneo kama vile kutozwa kodi kubwa, kulipishwa kodi kabla ya kuanza biashara, kubambikiwa kodi pamoja na sheria na taratibu kutokuwa rafiki kwa wawekezaji.

Wabunge waliitaja sheria, lakini pia kuwapo kwa urasimu na vipengele vya taratibu zetu zinazowavunja moyo wawekezaji, hivyo kuamua kwenda kuwekeza nchi nyingine.

Kuhusu kodi, mchakato wa ukusanyaji unalalamikiwa kwa kukosa utu katika baadhi ya nyakati. Matumizi ya nguvu zilizopitliza na ubabe kutoka kwa watendaji wa mamlaka husika wakati wa kudai kodi yanatajwa kuwa sababu inayowanyong’onyesha wafanyabiashara. Kibaya zaidi hali hii imekuwa ikiendelea licha ya kukemewa na Rais John Magufuli.

Machi 2018 akiwa mkoani Dodoma katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi wa reli ya kisasa, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango kufuatilia utozaji kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao kwa wafanyabiashara na wananchi wengi mchakato wake waliulalamikia wakiutaja kuwa ni kero.

Moja ya kero zinazolalamikiwa na wengi ni pamoja na maofisa wa TRA kukataa hesabu za mteja na kubuni za kwao ambazo huwa ni kubwa. Mazingira haya yaliyolalamikiwa na wabunge hayajaibuka, tunaamini kuwa hali hiyo ni matokeo ya mifumo tuliyojiwekea wenyewe na wakati mwingine hata kauli za viongozi.

Tunapoungana na wabunge kulisemea hili, hatuna budi kuwakumbusha viongozi kuchunga kauli kwa kuwa mara nyingi hata za kisiasa zinachukuliwa kama amri na watendaji katika vyombo vya Serikali.

Watu wanapofunga biashara, kukimbia nchi au kurudisha leseni, kutufumbue macho kuwa kuna mahala tunakosea. Ama mfumo uliopo hauna tija au kuna kasoro za uwajibikaji katika vyombo vinavyopaswa kusimamia ustawi wa biashara nchini.

Biashara ni uchumi na uchumi ndiyo unaoendesha nchi. Tunapata uzito kuona mustakabali wa Tanzania ya uchumi wa kati unaohanikizwa na viwanda, ikiwa kila siku hali ya biashara nchini ni afadhali ya jana. Tuweke mifumo imara, endelevu, rafiki na inayojali utu na masilahi ya wafanyabiashara. Tunahitaji kuona Tanzania ikiwa na wafanyabiashara mahiri watakaoisadia kukua kiuchumi. Hilo linawezekana ikiwa mamlaka husika zitaondoa kero zote zinazowasumbua wafanyabiashara.

Kodi ndiyo inayotumika kugharimia miradi katika sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa kama vile maji, elimu, afya, nishati na nyinginezo. Tuboreshe mazingira ya biashara na kuwapa ahueni wafanyabiashara ili walipe kodi stahiki kwa ustawi wao na maendeleo ya Taifa kwa jumla.