http://www.swahilihub.com/image/view/-/4883866/medRes/2190521/-/npbkxxz/-/korosho.jpg

 

Serikali yatabiri uzalishaji wa korosho kushuka

Korosho 

Na Rosemary Mirondo, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  13:08

Kwa Muhtasari

Uhakiki utawatambua watu ambao wameinyima Serikali mapato

 

mwananchi@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imesema kiwango cha uzalishaji wa korosho katika msimu wa 2018/19 kitafikia tani 275,000.

Kiwango hicho kitakuwa pungufu ya tani 38,826. zilizozalishwa msimu wa 2017/18 kwa asilimia 12.4.

Katika msimu huo uzalishaji wa korosho ulifikia tani 313,826.

Hata hivyo, kuna ongezeko la tani 55,000 katika makadirio ya kiwango cha uzalishaji wa msimu wa 2018/19, ambapo Rais John Magufuli alitangaza matarajio ya upatikanaji wa kiwango cha tani 220,000 za korosho msimu huu.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliliambia gazeti la The Citizen jana kuwa tayari tani 163,000 kati ya zile zitakazopatikana msimu huu zimeshachukuliwa na Serikali na vyama vya ushirika.

“Korosho hizi zilizalishwa katika mikoa mitatu ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Kuna zaidi ya tani 100,000 ambazo bado ziko mikononi mwa wakulima na vyama vya msingi vya ushirika,” alisema Hasunga.

“Ikitokea uzalishaji wa korosho ukafanyika zaidi katika maeneo ya ukanda wa pwani; Tanga, Morogoro, Singida na Dodoma hakika utafikia kiwango cha 275,000 katika msimu huu.”

Alisema tayari Serikali imekwishalipa Sh50.02 bilioni kwa wakulima wa korosho kupitia uhakiki wa vyama vya msingi vya ushirika 199.

Hasunga alisema tayari kuna vyama vya msingi 228 vilivyohakikiwa Desemba.

Kwa mujibu wa waziri huyo uhakiki huo umebaini idadi ya watu wenye korosho, lakini hawana mashamba.

“Sheria zinawataka watu hao kuwa na leseni za ushiriki katika shughuli za kibiashara. Kwa hiyo uhakiki utawatambua watu ambao wameinyima Serikali mapato kwa kufanya biashara bila leseni,” alisema Hasunga.