Simba isikate tamaa, nafasi bado ipo Afrika

Imepakiwa - Monday, April 8  2019 at  08:38

 

Mwishoni mwa wiki, Watanzania walibakia njia panda baada ya timu zao kushindwa kuzisimamisha timu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Timu ya taifa ya Twiga Stars kwa wanawake ililazimishwa sare ya 2-2 na Wacongo hao katika mchezo wa kuwania kufuzu Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Japan mwakani.

Wakati Twiga Stars ikitoka sare hiyo, Simba na TP Mazembe zilitoka suluhu katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Twiga Stars italazimika kwenda kushinda ugenini Aprili 9 ili kutinga raundi ya pili ya mchujo. Mshindi wa jumla wa mechi hiyo atakutana na Equatorial Guinea

Katika mchezo huo wa marudiano, Twiga Stars inaweza kufika mbali ikiwa tu itapunguza na kusahihisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza.

Ukiwaangalia Twiga Stars, bado wachezaji wake ni wazuri isipokuwa makosa madogo madogo ndiyo yaliyowamaliza.

Umakini katika kukaba,  na katika kulinda lango vinatakiwa kufanyiwa kazi zaidi kabla ya mchezo wa marudiano.

Tatizo jingine kubwa kwa ujumla wake ni idadi ya wachezaji wa Twiga Stars kutokuwa fiti.

Mfano mzuri kipindi cha kwanza, timu ilikatika, wachezaji walipotea kiasi cha kutoa nafasi kwa DR Congo kufunga mabao kirahisi.

Wachezaji wa safu ya ushambuliaji walizinduka kipindi cha pili kwa kucheza pasi za hapa na pale, lakini bado walionekana kukosa utimamu wa mwili.

Pamoja na kwamba wachezaji wengi wamekuwa katika ligi ya wanawake, lakini walikata pumzi na baadhi ya waliokuwa benchi na kuingia walisaidia upande mwingine kuimarisha baadhi ya maeneo. Kocha wa timu hiyo, Bakari Shime ana kazi ya kuunganisha timu.

Inaonekana kuna mkatiko mahali, kwamba muunganiko wa ngome, viungo na washambuliaji unapotea.

Pia umiliki wa mipira, wachezaji wanakuwa na nguvu kwa vipindi, kuna wakati walifaulu lakini kuna wakati walishindwa kuhimili mashambulizi.

Wachezaji kutofahamiana. Kuna mipira ambayo Asha Rashid na Mwanahamisi Omari walikuwa wakiipitisha, lakini walikosekana wamaliziaji.

Ukiangalia kwenye Ligi Kuu ya Wanawake, wachezaji hao wamekuwa mwiba, inawezekana kuwa mbinu wanazotumia zinakuwa dhidi ya timu za kawaida.

Kilichoiponza timu hiyo ni ukosefu wa mechi za kimataifa za kirafiki.

Mfululizo wa mechi za kirafiki kwa umoja wao, kungewajenga na hata kocha kufahamu kuna eneo linahitaji nguvu na eneo jingine kuimarishwa zaidi.

Ufundi mwingine ambao kocha anatakiwa kuwafundisha vijana wake, ni pamoja na mipira ya faulo ambayo kama wachezaji wake wangekuwa na utaalamu wa kuipiga mipira hiyo, nayo inasaidia kwa njia moja au nyingine.

Kingine ni katika kupiga penalti. Penalti waliyopoteza Twiga Stars imeonyesha wazi kuwa wachezaji hawako fiti katika eneo hilo. Mchezo wa marudiano unaweza kumalizika tena kwa mabao 2-2 na kukalazimika kupigwa mikwaju ya penalti na wachezaji walionekana kutokuwa na nguvu hata ujanja wa kupiga penalti.

Kwa upande wa Simba, kinachotakiwa ni kwa wachezaji kutulia na kujipanga kwa marudiano. Kulitokea makosa mbalimbali kwa washambuliaji wa timu hiyo, John Bocco na Meddie Kagere na zaidi umakini.

Ninawapongeza wachezaji wa Simba kwa kazi nzuri japokuwa haikuleta mabao.Kinachotakiwa sasa ni kurekebisha kasoro hizo.

Bocco alibaki yeye na kipa akapiga nje, suala la penalti ni kutulia na kumhamisha kipa lakini alichofanya ni kupaisha mpira.

Katika eneo hilo ninachokiona, pamoja na Bocco kuwa ndiye mpigaji, wapo watu ambao ni nadra kukosa penalti sasa kuna haja ya kuwaachia wale ambao ni uhakika na kama kukosa iwe inatokea tu.

Tunaamini John Bocco atakuwa sawa, lakini kuna kila sababu ya kufanya mazoezi ya nguvu kwa wachezaj wa timu hiyo kwamba inawezekana matokeo yakasimama hivi na uamuzi wa kupiga penalti ukaja na wachezaji wetu kushindwa kufunga mikwaju ya penalti.

Kimsingi, Simba na Twiga Stars wasifikirii kama watakwenda DR Congo wakiwa shingo upande kuwa matokeo hayo bado hayajawakalia sawa. Timu zote zifahamu kuwa bado kuna dakika 90 nyingine. Kutoka sare si mwisho wa matokeo mengine.

Wachezaji wote waende DR Congo kwa kujiamini huku wakiamini kuwa soka ina matokeo matatu, kushinda, kufungwa na sare. Pamoja na ugumu wa kufugika, TP Mazembe inafungika japokuwa hatua ya makundi lolote linaweza kutokea. Simba isiende kinyonge, iingie kibabe kuonyesha kwamba iko tayari kwa mapambano, kuingia Lubumbashi kwa hofu, itawaondoa mchezoni na hata kufungwa kirahisi.