http://www.swahilihub.com/image/view/-/2829000/medRes/1087908/-/14i78jfz/-/snmobile.jpg

 

TCRA isiache kuwabana wezi wa simu

Simu ikiwa mkononi

Simu ikiwa mkononi. Picha/MARTIN MUKANGU 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, November 2  2018 at  07:56

Kwa Muhtasari

Simu za kiganjani 4,340 ambazo Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewafungia watumiaji, inasema imebainika kuwa ni za wizi na nyingine zimenunuliwa katika maduka yasiyo rasmi huku zikiwa na ubora duni.

 

INATIA moyo kusikia taarifa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewafungia watumiaji wa simu za kiganjani 4,340, baada ya kubainika kuwa simu zao ni za wizi na nyingine zimenunuliwa katika maduka yasiyo rasmi huku zikiwa na ubora duni.

Kufungia simu ni hatua moja muhimu, lakini TCRA inapaswa kwenda mbali zaidi kupambana na tatizo hili ambalo kwa hakika ni tabia sugu kwa watumiaji wengi.

Uzoefu unaonyesha watumiaji wengi wa simu hawajali kuhusu upatikanaji wa simu zao, lakini wanachokijali ni kama simu hizo wanaweza kuzitumia kwa mahitaji yao.

Kutojali upatikanaji wa simu kunawafanya watumiaji wengi kununua simu kwa njia holela pasipo kujua kuwa wanajiweka katika hatari ya kuwa washiriki wa uhalifu.

Hili ni kosa ambalo TCRA kwa kushirikiana na mamlaka nyingine hazina budi kulitolea elimu kwa kuwa lina madhara ikiwamo hatari ya mhusika kushtakiwa mahakamani.

Kosa hili ni miongoni mwa makosa kadhaa yaliyoainishwa kwenye Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca).

Kwa mujibu wa sheria hiyo ya mwaka 2010, makosa mengine ni kusambaza ujumbe wa kuudhi, kutoripoti kupotea au wizi wa simu au laini, kuchakaa simu au laini, kuuza bila kusajili na kutoa taarifa za uongo.

Haya si makosa ya kubeza. Ni vitendo ambavyo kama tutaviacha viendelee kuota mizizi, vinaweza kuhatarisha sio tu usalama wa watumiaji wa simu, lakini hata nchi kwa jumla.

Tunapoitaka TCRA kwenda mbali zaidi kushughulikia tatizo hili tunamaanisha kwamba TCRA isiishie tu kufungia simu, lakini ijihimu kuandaa mifumo ya kiteknolojia inayoweza kubaini simu zilizoibiwa ili hatimaye wezi wabainike na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.

Ikiwa TCRA kupitia mifumo yake imeweza kuzibaini simu hizo zisizokuwa na viwango na hata zile zilizopatikana kwa njia za wizi, ni dhahiri mamlaka hiyo inaweza pia kubaini mnyororo wa watumiaji wa simu hizo, kitendo kinachoweza kuzisaidia mamlaka zinazopambana na uhalifu kama Jeshi la Polisi kuwashughulikia wahusika.

Kama ambavyo TCRA imekuwa na msaada mkubwa katika mchakato unaoendelea wa kuwashughulikia watu wanaofanya utapeli kwa kutumia ujumbe wa simu au kusimamia usajili wa laini, kasi hii inaweza pia kuelekezwa katika kuwang’amua wezi wa simu.

Maendeleo ya Tanzania na ustawi wa wananchi wake pamoja na mambo mengine unategemea pia sekta ya mawasiliano ikiwamo matumizi ya simu za mkononi ambazo kwa sasa zimekuwa kimbilio la walio wengi.

Ni dhahiri kuwa simu kwa Watanzania wengi zimekuwa sehemu ya maisha yetu. Hivi sasa simu sio kifaa cha mawasiliano pekee, simu zinafanya kazi ya kuhifadhi fedha, ni sehemu ya kuhifadhia nyaraka mbalimbali na matumizi mengine mbalimbali muhimu kimaisha.

Ni kwa sura hii tunahitaji kuwa na mikakati na mifumo imara ya mawasiliano itakayosimamia matumizi haya. Kwa kufanya hivyo, simu zitakuwa zana muhimu ya kutufikisha tunapotaka kwenda kama Taifa na pia kuboresha ustawi wa kila mwananchi.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647