TMA imetoa angalizo, wadau wajipange

Na GAZETI LA MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, September 7  2017 at  14:54

Kwa Mukhtasari

Mwishoni mwa wiki hii, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ilitangaza kwamba mikoa sita itakabiliwa na ukame kuanzia mwezi huu na kuzitaka mamlaka nyingine kujippanga kwa ajili ya kukabiliana na majanga Kwenye maeneo yatakayokuwa na mvua juu ya wastani.

 

Mikoa itakayokuwa na mvua chini ya wastani na vipindi virefu vya ukame ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Unguja Pemba na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.

Mikoa ambayo inatarajia kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani ni ile ya Magharibi mwa Ziwa Victoria, Pwani ya Kaskazini ma Mkoa wa Kilimanjaro na Kaskazini mwa MKoa wa Kigoma ambayo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Dk Agnes Kijazi alisema mvua za wastani na vipindi virefu vya ukame  vinatarajiwa kujitokeza katka kipindi ca msimu wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba  hadi Desemba.

Alisema mvua hizo  zinatarajiwa kuanza kuanza mwezi huu katika maeneo ya Ziwa Victoria na Oktoba kwenye ukanda wa Pwani ambapo mwezi Novemba ikitarajiwa kunyesha katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.

Dk Kijazi alisema hali ya vipindi virefu vya ukame vinatarajiwa  kujitokeza mwezi Oktoba na ongezeko la la mvua linatarajiwa kuanza Novemba na Desemba.

Kwa sababu  hiyo, Dk Kijazi aliwataka wakulima wa mikoa hiyo kuandaa mashamba  mapema na kuandaa mapema mazao yanayokamaa kwa muda mfupi katika maeneo hayo.

Alizitaka taasisi za Serikali zinazoshughulika na maafa  wakiwemo wadau wa afya  na mamlaka za miji kuchukua hatua  kupunguza athari zinazoweza kutokea  katika msimu wa mvua hizo.

Alisema mvua katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba ambazo zitakuwa za wastani na chini ya wastani isipokuwa Kusini mwa Mkoa wa Morogoro  zitakuwa  za wastani na juu ya wastani.

Tunapenda kutilia mkazo angalizo la TMA kuhusu  wadau wengine kuuchukulia  kwa uzito unaostahili utabiri huo na hasa ikizingatiwa tahadhari ya ukame katika maeneo hayo.

Kama inavyoeleweka, asilimia zaidi ya 75 ya Watanzania ni wakulima na karibu wote wanategemea mvua, hivyo utabiri huo una maana kubwa mno kwao.

Ni matumaini yetu kwamba wadau wa kilimo  na maofisa ugani katika halmashauri husika watashinda  mashambani  wakitoa elimu  kuhusu ni kipi kinachostahili kufanywa katika kipindi hiki.

Mafunzo hayo yanaweza kuwa ya kuwaelekeza aina ya mazao yanayostahimili ukame na kama hata hayo hayatakuwa na uwezekano wa kustawi basi washauriwe kufanya shughuli nyingine ili wasipoteze nguvu zao na rasilimali kidogo waliyo nayo kufanya kazi ambayo haitawalipa.

Sambamba na maofisa ugani katika mafunzo ya kilimo kuendana na hali ya hewa huu ni wakati mwafaka kwa asasi zisizo za Kiserikali kuhakikisha kwamba wanashirikiana na Serikali za Mitaa kuwasaidia wakulima kuwa na mipango bora ya matumizi ya rasilimali walizonazo  kwani kwa kufaanya hivyo wanaweza kuwasaidia kuondokana na adha ya kuomba chakula cha msaada.