http://www.swahilihub.com/image/view/-/4659374/medRes/2042271/-/yl51sj/-/agness.png

 

TMA yatahadharisha juu ya hali ya hewa

Mkurugenzi Mtendaji wa TMA, Dk Agness Kijazi  

Na Elizabeth Edward

Imepakiwa - Thursday, July 12  2018 at  14:30

Kwa Muhtasari

Vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa kujitokeza

 

Mkurugenzi Mtendaji wa TMA, Dk Agness Kijazi anasema hali ya baridi inayotarajiwa katika maeneo mengi ya nchi hususan maeneo ya miinuko inaweza kusababisha kudumaa kwa mazao kama vile ndizi pamoja na mazao ya nje ya msimu na kuathiri mifugo.

Anasema upo uwezekano hali hiyo ya hewa ikawa kikwazo cha ukuaji wa mazao hayo na kusababisha mifugo kufa kutokana na kushindwa kuhimili baridi.

“Kwa kawaida huu ni msimu wa upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi. Katika msimu wa mwaka huu, hali hiyo inatarajiwa kuwepo ikiambatana na vipindi kadhaa vya upepo kutoka Kusini Mashariki katika mwambao wa Pwani ya Tanzania.

“Pamoja na kwamba kipindi cha msimu wa JJA (Juni, Julai, Agosti) kwa kawaida huwa ni kikavu, katika msimu wa mwaka huu, vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa Pwani (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Lindi).

Athari za hali hiyo zimeanza kuonekana kisiwani Zanzibar ambapo upepo umeezua nyumba 136 katika Wilaya ya Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Tukio hilo lililotokea Julai 1 limesababisha uharibifu katika makazi ya watu na nyumba za ibada kana kwamba hiyo haitoshi watu sita wamejeruhiwa kutokana na kuangukiwa na mapaa ya nyumba upepo mkali ulipovuma.

Dk Kijazi anatoa wito kwa wananchi na sekta husika kuchukua hatua stahiki kutokana na athari hasi zinazoweza kuambatana na matarajio ya utabiri huu.

Hali hiyo ya hewa pia inaweza kuwa na matokeo hasi kwa afya ya binadamu hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari na kujikinga na baridi.

Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, Dk Ally Mzige anaeleza kuwa baridi linapokuwa kali upo uwezekano wa kutokea mlipuko wa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo.

Anasema licha ya kuwa ugonjwa huo hautokei mara kwa mara ni muhimu kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuvalia mavazi ambayo yatasaidia kujikinga na baridi.

“Hiki ni kipindi ambacho watu wanatakiwa kufanya sana mazoezi ili kuifanya miili ichangamke, vinywaji vyenye joto kama chai vinasaidia katika kupunguza baridi mwilini ikiwa ni pamoja na nguo nzito,” anasema.

Sanjari na hilo Dk Mzige anasema hali hiyo ya hewa inachangia pia kutokea kwa baridi yabisi. Hii husababisha maumivu ya viungo pale baridi linapokuwa kali na kupenya kwenye mifupa.

Kwa wale wenye ugonjwa wa pumu ni muhimu kwao kuchukua tahadhari zaidi kwa sababu baridi ikiwa kali ni rahisi kifua kubana kwa hiyo wanatakiwa kufuata maelekezo ya afya wanayopewa hospitali,”

Dk Mzige anasisitiza kuwa licha ya baridi kuwepo ni muhimu kuzingatia suala zima la usafi wa mwili ikihusisha kuoga ili kujiondoa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya ngozi.

“Baridi lisiwe chanzo cha watu kushindwa kuoga, usipooga jiandae kupata upele na magonjwa mengine ya ngozi. Hakikisha unaoga na ngozi unaipaka mafuta isikakamae,” anasema.

Hali iko vipi kwa kanda

Dk Kijazi anasema kanda ya Ziwa Victoria inayohusisha mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu kiwango cha chini cha joto kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14 na 18 katika maeneo mengi.

Kiwango cha joto cha chini ya nyuzi joto 14 kinatarajiwa katika maeneo ya miinuko hususan katika mikoa ya Kagera na Geita.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini unaohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba inatarajiwa kuwa na kiwango cha joto kati ya nyuzi joto 18 na 24 katika maeneo mengi.

Vipindi vya baridi vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya Mkoa wa Tanga hususan wilaya za Lushoto na Bumbuli ambapo kiwango cha chini ya nyuzi joto 18 kinatarajiwa.

Kanda ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara); kiwango cha joto kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12 na 17 katika maeneo mengi. Hata hivyo, katika maeneo ya miinuko kiwango cha cha joto kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 12.

Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi inatarajiwa kuwa na kiwango cha joto kati ya nyuzi joto 14 na 16 katika maeneo mengi wakati kanda ya kati inayohusisha mikoa ya Dodoma na Singida kiwango cha joto kitakuwa kati ya nyuzi joto 12 na 15 katika maeneo mengi na vipindi vichache vya baridi chini ya nyuzi joto 12 vinatarajiwa.

Kiwango cha joto cha kati ya nyuzi joto 19 na 24 kinatarajiwa kuwepo ukanda wa Pwani ya Kusini inayohusisha mikoa ya Mtwara na Lindi huku mkoa wa Ruvuma ukitarajiwa kuwa na joto kati ya nyuzi 12 na 16.

Kanda ya nyanda za juu Kusini-Magharibi (mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya Kusini ya Mkoa wa Morogoro) kiwango cha joto kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 5 na 12 katika maeneo mengi.