TRA iimarishe miundo ya ukusanyaji kodi

Haji Semboja

Profesa Haji Semboja. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, July 14  2017 at  12:40

Kwa Mukhtasari

Juzi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitoa taarifa ya makusanyo ya kodi ikibainisha kuwa katika mwaka unaoishia 2017 ilifanikiwa kukusanya Sh14.4 trilioni ikiwa ni pungufu kwa TSh700 bilioni.

 

JUZI Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitoa taarifa ya makusanyo ya kodi ikibainisha kuwa katika mwaka unaoishia 2017 ilifanikiwa kukusanya Sh14.4 trilioni ikiwa ni pungufu kwa TSh700 bilioni.
Upungufu huu ni kwababu TRA ilijiwekea lengo la kukusanya Sh15.1 trilioni. Pamoja na kutofikiwa kwa lengo hilo taarifa ilisema makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 7.6 jambo ambalo kimsingi sisi tunaamini si jambo la kujivunia.

Tukikopa maneno ya mchumi bobezi nchini Profesa Haji Semboja makusanyo hayo yanaakisi uhalisia kwamba tumekuwa tukitegemea ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye vyanzo vilivyowategemea watu wachache.

Semboja ambaye pia ni Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kwamba kiasi kilichoelezwa kupanda ni kioo cha uchumi wenye wigo mdogo wa ulipaji kodi.
Ni kweli Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kulipa kodi na mfano mzuri ni huu alioutoa mchumi huyu kuwa takriban asilimia 70 ya Watanzania waliopo vijijini hawalipi kodi licha ya ukweli kwamba wana miradi inayowaingizia kipato.
Kwa sababu hii, kwa miaka nenda rudi, moja ya vyanzo vikubwa vya mapato ya Serikali kimekuwa ni kodi ya mapato inayotozwa kwa wafanyakazi nchini.
Wafanyakazi wana kilio kuwa wamekuwa wakibeba mzigo mzito wa kodi ambao pengine ungeweza kupungua kwa kiasi kikubwa kama Serikali ingejihimu kutanua wigo wa kukusanya mapato kutoka kwa vyanzo vingine.
Bado kuna kundi ambalo wafanyabiashara hasa waliopo mijini na vijijini ambao pamoja na kupata kipato kizuri hawalipi kodi.
Inawezekana kundi hili na mengine mengi yasiyofikiwa na mchakato wa ukusanyaji wa mapato yanakwepa kodi kwa sababu ya kukosa elimu ya ulipaji kodi au kutokuwapo kwa mazingira rafiki kwa kufanya hivyo.
Hapa ndipo unapokuja wajibu wa TRA kuboresha kitengo cha mlipa kodi kwa maendeleo ya nchi.
Mbinu nyingine tunayopendekeza ya kuwafikia watu wengi zaidi ni pamoja na vyombo husika serikalini kujitahidi katika mchakato wa kurasimisha biashara ili kila mfanyabiashara ajisajili na kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi yaani TN.
Hatua hii itamfanya kila mfanyabiashara au mjasiriamali kuendesha biashara halali ambayo inalipiwa kodi kutokana na mauzo au faida ya biashara husika.
Tunaamini kama TRA itajipanga barabara katika utoaji elimu kwa umma na kuwa na utaratibu wa mzuri na wa kisasa wa kukusanya kodi, siyo tu kiwango cha makusanyo kitarimaika bali pia kiasi cha makusanyo kitakuwa kikubwa na itapunguza mizozo ambayo hujitokea kati ya TRA na walipa kodi hasa wafanyabiashara wadogowadogo na wa kati.
Watanzania tunao wajibu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na kuboresha ustawi wa wananchi.
Ili kufika huko tunahitaji kuwa na TRA iliyojipanga kikamilifu kimuundo na kiteknolojia ili hatimaye mchakato wa ukusanyaji kodi uwafikie watu wengi zaidi. Tunaamini kwamba hili litawezekana na la msingi ni kiasi cha kujipanga tu.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.