TRA iwatupie jicho waliofunga biashara

Imepakiwa - Wednesday, May 8  2019 at  11:49

 

Juzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilisema imefuta utaratibu wa kuwafungia biashara wadaiwa wa kodi ya mapato.

Ilisema, kuanzia sasa hakuna mtu atakayefungiwa biashara yake kwa sababu ya kuchelewa kulipa kodi au malimbikizo ya kodi, na endapo itaonekana kuna ulazima wa kufanya hivyo kibali kitatolewa na kamishna mkuu wa mamlaka hiyo pekee.

Suala la kufunga biashara kwa sababu ya madai ya kodi limekuwa likilalamikiwa na wafanyabiashara wengi pamoja na viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Rais John Magufuli na wote wamekuwa wakihoji ni wapi mfanyabiashara atapata fedha anayodaiwa ikiwa biashara yake imefungwa.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jambo hilo limesitishwa tangu mwishoni mwa mwa mwaka jana na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amekwishatoa maelekezo kwa mameneja wa mamlaka hiyo wa mikoa na wilaya kulitekeleza.

Kwa sasa utaratibu uliopo, kwa mujibu wa Kayombo ni kwa maofisa wa mamlaka hiyo kuzungumza na mfanyabiashara husika na kukubaliana namna ya kulipa na utaratibu utakaotumika na endapo atakaidi kulipa kwa makusudi na ikaonekana kuna ulazima wa kumfungia, kibali cha kufanya hivyo kitatolewa na kamishna mkuu.

Sambamba na hilo, TRA imeachana na utaratibu wa kumtaka mfanyabiashara kulipa kodi kabla ya kuanza biashara na badala yake, anaweza kulipa baada ya kufanya biashara kwa miezi mitatu.

Tunaipongeza TRA kwa habari hizi njema kwa wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla, kwa sababu ni ndoto ya wengi kujiingiza katika biashara lakini kikwazo kimekuwa hofu ya kodi.

Vilio vya wafanyabiashara na viongozi dhidi ya mamlaka hiyo vimekuwa vikubwa.

Mathalan, wapo waliokuwa wakidai kukwamishwa kuanza biashara wakitakiwa kulipa kodi kabla, wengine wakibambikiwa kodi kubwa na hatimaye kufungiwa biashara. Pia, kuna kundi jingine la waliofikia hatua ya kukata tamaa na kufunga kabisa biashara zao kutokana na kufuatwafuatwa na maofisa wa mamlaka hiyo au mawakala wao ili walipe kodi, ilhali biashara zao zikijikongoja.

Tunaipongeza TRA kwa kujitathmini na hatimaye kuamua kuondokana na vikwazo hivyo, kwani imeonyesha kwamba hawakuwa ‘sikio la kufa lisilosikia dawa’. Hii ni hatua njema na inayotia moyo kwa sekta ya biashara na uwekezaji nchini.

Sambamba na hilo, tunaiomba mamlaka hiyo iangalie namna bora ya kuwarejesha katika shughuli zao wafanyabiashara ambao kwa njia moja au nyingine walilazimika kufunga biashara zao, iwe ni kwa kufuatwafuatwa na maofisa wao ili walipe au walifilisika baada ya kubanwa na kuamua kulipa kodi kiasi cha kuyumbisha mitaji yao.

Tunalisema hili tukimaanisha kwamba, wafanyabiashara waliolazimika kufunga shughuli ni wengi na mifano halisi inaonekana huko mitaani ambako biashara zimefungwa, na kwa kufunga kwao ina maana mzunguko mkubwa wa fedha umeondoka katika uchumi wa nchi yetu.

Ni vyema sasa TRA kwa kushirikiana na mamlaka zingine zilizowafikisha wafanyabiashara hao katika hatua hiyo, ziwajibike kuwarejesha katika hali ya zamani ili nao washiriki kujenga uchumi wa Taifa letu.

Mara kwa mara viongozi wamekuwa wakiwasihi wananchi wafanye kazi, hivyo hata hawa walioondoka katika mzunguko wa biashara kwa sababu za kukimbia kero ya kodi, wakirejea katika shughuli zao, tunaamini kwamba mchango wao utaonekana katika sekta zingine ikiwamo ya ajira maana miongoni mwao watawaajiri Watanzania wenzao.

Kwa mara nyingine tunaiomba TRA iendelee na usikivu wa namna hii na kuufanyia kazi. Tanzania ni yetu sote.