Taarifa za hali ya hewa zifanyiwe kazi

Imepakiwa - Friday, March 22  2019 at  11:44

 

Wahenga walinena kuwa mwenzako anaponyolewa wewe tia maji.

Ni msemo unaotukumbusha mengi hasa tunapotafakari juu ya matukio yanayoendelea katika nchi za Kenya, Msumbiji, Malawi, Zambia na Zimbabwe.

Nchini Kenya hasa eneo la Turkana ukame mkubwa umesababisha vifo vya watu na mifugo ambayo ni sehemu muhimu ya maisha ya watu wa eneo hilo.

Malawi, Msumbiji, Zambia na Zimbabwe ambazo ni nchi majirani upande wa Kusini wa nchi yetu, zimekumbwa na kimbunga kiitwacho Idai.

Kimbunga hiki kimeleta madhara makubwa ikiwamo vifo vya mamia ya watu na uharibifu wa miundombinu kama barabara na makazi.

Haya ni matukio ya kiasili ambayo kama yameweza kuzikumba nchi jirani,yanaweza pia kuikumba nchi yetu.

Ni kwa sababu hii kuna haja kubwa ya kutafakari, kujifunza na hatimaye kujiandaa kukabiliana nayo.

Uzoefu unaonyesha kuwa tuna udhaifu katika kubaini mapema kutokea kwa majanga na kikubwa zaidi katika kukabiliana nayo.

Tunasema udhaifu mkubwa katika kukabiliana kwa sababu hata pale Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) inapotekeleza wajibu wake wa kutabiri hali ya hewa na kutuasa juu ya madhara yanayoweza kutokea, baadhi ya vyombo husika ama hujiweka nyuma au vinasusua katika kufanyia kazi taarifa hizo.

Mara nyingi majanga haya yanapotokea sekta kama za kilimo, ufugaji, makazi na usafirishaji, ndizo zinazoathirika. Lakini inasikitisha kuwa kuna ushiriki mdogo wa wadau wanaoshughulika na sekta hizo.

Sekta hizi zote ziko chini ya vyombo maalumu kama wizara, taasisi na mamlaka ambazo kimsingi zinapaswa kutumia taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa kuchukua tahadhari na kuweka mikakati ya kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Njia mojawapo mwafaka inayoweza kutumiwa na vyombo hivi ni kila kimoja kwa wasaa wake kushitadi katika kutoa elimu kwa umma. Na hili linaweza kutekelezeka kwa ufanisi kama kila chombo kwa wasaa wake kitatumia vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii kutoa elimu juu ya majanga mbalimbali ya kiasili.

Mfano mzuri ni taarifa ya TMA kuhusu ukame uliopo katika baadhi ya mikoa nchini. Huu ni wakati mwafaka kwa Wizara ya Kilimo kutumia taarifa hiyo kutoa elimu ya kina kuhusu aina ya kilimo na mazao yanayofaa katika maeneo yenye ukosefu mvua.

Hii ni wizara moja. Lakini kama nyingine zinazohusiana na makazi, miundombinu nazo zitawajibika kwa ari ya juu, sio tu tutajiweka katika mazingira mazuri ya kupambana na majanga mbalimbali, lakini wananchi wataongeza imani kwa taasisi hizo wakiamini kuwa zinajali uhai na ustawi wa maisha yao kwa jumla.

Pia, ongezeko la majanga haya sasa yatuzindue ili hatimaye tuitazame kwa jicho la karibu idara ya uratibu wa maafa iliyopo ofisi ya Waziri Mkuu.

Tuipe nguvu ikiwamo ya uwezeshaji ili wahusika wasiwe wanaibuka wakati wa matukio pekee. Tuiwezeshe ili iweze kusimamia ipasavyo sheria za kupambana na majanga, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu namna ya kuepuka majanga, kupambana nayo yanapotokea na mbinu za uokoaji.