Takukuru ianze mapema kufuatilia uchaguzi

Na cosmasmarian@gmail.com

Imepakiwa - Wednesday, April 17  2019 at  11:20

 

Wakati Watanzania wakijiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali wamekuwa wakiitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuanza kufuatilia vitendo vya rushwa kwa watakaowania nafasi za uongozi.

Vitendo vya rushwa vimekuwa vikikemewa mara kwa mara na Rais John Magufuli ikiwamo kuwavua uongozi watumishi wanaobainika kujihusisha na suala hilo huku akiisisitiza Takukuru kupambana kwelikweli na hali hiyo.

Pamoja na hatua hizo kuchukuliwa, harufu ya rushwa imeendelea kusikika kwa wananchi hususan wa kipato cha chini hasa wale waishio maeneo ya vijijini ambao hawana elimu ya kutosha kuhusiana na rushwa.

Tumeshuhudia mara kadhaa vitendo vya uonevu hususani kwenye chaguzi kwa baadhi ya wananchi na viongozi kupokea na kutoa rushwa lengo likiwa kuwa wachaguliwe kwenye nyadhifa hizo. Suala hilo linasababisha kudhoofisha uchaguzi na pia kupata viongozi wasiokuwa waadilifu.

Hata Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga amegusia suala hilo wakati akizungumza na wakuu wa idara wa wilaya hiyo na viongozi wa dini akiwataka kutumia nafasi zao kuwaelimisha wananchi madhara ya kupokea na kutoa rushwa, na hatimaye kuchagua viongozi wasio sahihi.

Mbali na hilo pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura.

Ni vyema sasa kwa taasisi yetu hii kuanza kumulika vitendo hivyo kabla kampeni za uchaguzi hazijaanza kuliko kusubiri siku za uchaguzi pekee.

Tumeshuhudia baadhi ya viongozi na makundi ya watu wakikamatwa kwenye kipindi hicho wakati wa kampeni, suala hilo halifanyiki baada ya uchaguzi kwani hata baadhi ya kesi zao nazo huyeyuka.

Wahenga walisema “samaki mkunje angali mbichi” na tukisubiri moto ukolee ndipo tuanze kuuzima hatutaweza.

Tujitahidi kila mmoja kwa kadri anavyoweza na uelewa wake juu ya jambo hili kuhakikisha vita ya kupinga rushwa inakomeshwa ili tuwe na viongozi bora. Na hii itasaidia kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.

Tutambue kwamba vitendo vya rushwa haviishii tu katika kutoa na kupokea fedha na vitu vingine vya thamani, hata vitendo vibaya vinavyokiuka taratibu ni ukiukaji wa sheria na taratibu.

Hivyo, Takukuru isiishie tu kufukuzana na wanasiasa wanaokusanyana kugawana chumvi, khanga na fedha, bali ifuatilie na watendaji wengine wanaokiuka taratibu kwa makusudi kwa masilahi ya watu wao dhidi ya wengine wenye haki.

Pamoja na juhudi mbalimbali ambazo Takukuru imekuwa ikifanya kutoa elimu kwa wananchi, sina hakika kwa kiasi gani imewafikia wapigakura wanaotarajiwa kushiriki uchaguzi.

Kwa mfano, takwimu za kaimu mkuu wa Takukuru mkoani Mwanza, Emmanuel Stenga kuwa taasisi hiyo imesaidia kuzifikia klabu 95 za wapinga rushwa na kufungua nyingine 142 katika shule za msingi, sekondari na vyuo, bado haifafanui kwa kina jinsi gani klabu hizo zitasaidia kuwaelimisha wapigakura.

Pamoja na klabu hizo, taasisi hiyo imetoa semina 33 katika taasisi na idara mbalimbali sanjari na mikutano ya hadhara 24 kwa wananchi ambavyo pia ni matarajio ya wengi kuwa ingesaidia kusambaza elimu ya kukabiliana na rushwa wakati wa uchaguzi.

Kwa kukosekana elimu hiyo kwa umma, hata katika idara au makundi yanayolalamikiwa kupitia taarifa zinazotolewa kwa Takukuru siyo rahisi kuona wanasiasa ambao wakati wa uchaguzi ndio vinara wa vitendo hivyo.

Hivyo ni vyema suala hili la rushwa katika uchaguzi likaongezewa nguvu kuhakikisha elimu ya kupinga kupokea na kutoa rushwa inawafikia wananchi na watu wanaobainika wanachukuliwa hatua za kisheria. Elimu hii ianze kutolewa mapema wakati tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kila mmoja atambue haki na wajibu wake.

Vilevile, iwafikie zaidi kina mama ambao wanatajwa kuwa ndio waathirika zaidi kwa kuwa ndilo kundi linalojitokeza kwa wingi kupiga kura na ndilo linaloshawishiwa kwa urahisi.

Ni rai yangu kuwa kila mmoja akiwajibika kumwelimisha mwenzake ili kuhakikisha tunapunguza vitendo vya rushwa, tutafanikiwa.

Pia Takukuru isaidie kuwaelimisha wananchi ili waweze kuchagua viongozi wazalendo watakaojali masilahi ya nchi.