http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885694/medRes/2191593/-/2x4fjpz/-/wahasibu.jpg

 

Tanzania yakabiliwa na uhaba wa wahasibu

Wanachama wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) wakishiriki kwenye mkutano wa mwaka wa bodi hiyo, uliofanyika Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis   

Na Ephrahim Bahemu

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  15:34

Kwa Muhtasari

Upungufu wa wataalamu hao unatokana na uchache wa vyuo na fikra potofu

 

ebahemu@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tanzania kuna uhaba wa wahasibu 3,000 lakini wapo ambao hawana ajira licha ya kuwa wanahitajika katika idara za Serikali, mashirika na kampuni.

Hayo yameelezwa jana na mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu (NBA), Profesa Isaya Jairo katika mkutano wa mwaka uliofanyika jijini hapa.

“Hivi sasa tuna wahasibu takriban 6,000, lakini bado kuna mashirika na idara za Serikali ambazo zina mahitaji ya wataalamu hao licha ya kuwa wapo ambao bado hawajapata ajira,” alisema Profesa Jairo.

Alisema wakati huu ambao Serikali inatekeleza mpango wake wa uchumi wa viwanda, wahasibu zaidi ya 3,000 wanahitajika.

“Huenda wakahitajika zaidi ya hao endapo kasi ya ujenzi wa viwanda itakuwa kubwa zaidi,” alisema.

Alisema upungufu wa wataalamu hao unatokana na uchache wa vyuo na fikra potofu kwamba kozi za uhasibu ni ngumu wakati si kweli,

“Wenzetu Kenya ambao ndio tunashindana nao, wana wahasibu zaidi ya 15,000,” alisema.

Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Fedha, Amina Shaaban alisema bila wahasibu, Taifa linakosa fursa nyingi za kiuchumi.