Tozo mpya ya viwanja ichochee maendeleo ya uchumi

Imepakiwa - Friday, April 19  2019 at  10:55

 

Jana katika gazeti hili tulichapisha habari kuhusu hatua ya Serikali kushusha tozo ya kupima, kurasimisha makazi na viwanja ili hatimaye wananchi kupata hati ya kiwanja kutoka Sh250,000 hadi 150,000.

Hatua hiyo kama ilivyoelezwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, pamoja na mambo mengine inalenga kuwawezesha wananchi wengi kupata hati na mwishowe kulipa kodi ya ardhi.

Bila chembe yoyote ya shaka, hii ni taarifa nzuri kwa Watanzani hasa kwa kuzingatia kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakilizwa na urasimu uliopo katika kupata hati za makazi yao. Ni urasimu ambao ukiutazama kwa ndani haukuwa na sababu za msingi zaidi ya kuchochea vitendo vya rushwa, ambavyo viliwakimbiza wengi waliokuwa wakihitaji kurasimisha makazi yao.

Nje ya urasimu huo, kiwango kikubwa kilichokuwa kikitozwa awali nacho kilikuwa kikwazo kwa wananchi wengi kurasimisha makazi. Awali kiasi cha tozo hiyo kilikuwa Sh500,000, baadaye kikashushwa hadi Sh250,000 na sasa kimeshushwa tena na kufikia Sh150,000. Hapa tumetaja kiasi kilichokuwa kikitambuliwa na Serikali, achilia mbali gharama za kampuni binafsi zilizokuwa zikifikia mamilioni.

Kufuatia hatua hiyo ya wizara, tunaamini suala la ardhi halitakuwa tena eneo la watu wachache kunufaika nalo. Hawa ni wale watumishi warasimu waliokuwa wakiufanya mchakato wa kupata hati kuwa mgumu katika ofisi za Serikali, hususan ngazi ya halmashauri na hata wizara yenyewe.

Vilevile kwa Serikali kuweka bei elekezi, huo ni mkakati mzuri wa kuwabana na kuwadhibiti mawakala na kampuni zinazojishughulisha na masuala ya uuzaji na upimaji wa ardhi

Tunapopongeza hatua hii ya Serikali, hatuna budi kuitanabahisha Serikali kuwa Watanzania wamechoka kusikia kauli nyingi zenye matumaini kuhusu maendeleo ya sekta ya ardhi, ikiwamo hatua hii ya kushusha tozo. Kutamka ni suala moja, lakini lililo muhimu zaidi kwa wizara husika ni kuona utekelezaji wa hatua hiyo kivitendo.

Tozo inaposhushwa ni dhahiri kuwa wananchi wengi watajitokeza kurasimisha viwanja vyao. Hatua hiyo isiwe sababu ya watumishi kutafuta mbinu za kujipatia kipato nje ya kima kilichotangazwa.

Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tayari imeshajinasibu kufuata kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, tunaikumbusha kuwa huu ni wakati wa vitendo.

Dhamira ya Serikali kurasimisha makazi ili wananchi wachangie uchumi wa nchi kupitia kodi ya ardhi haitafanikiwa kama mpango huu utakwamishwa na baadhi ya watu katika mamlaka husika.

Mabadiliko ambayo Serikali ya awamu hii iliwaahidi Watanzania katika maeneo mbalimbali yaanze sasa kwenye ardhi kama sekta muhimu kwa ustawi wa maisha ya Watanzania na uchumi wa nchi kwa jumla.

Ni kwa kufanya hivyo tunaamini kwamba Serikali itaheshimika, kupendwa na itakuwa imemaliza moja ya matatizo ambayo yamechochea kuwapo kwa makazi mengi yasiyokuwa rasmi.

Tunaamini kwamba zama za kuwa na makazi holela zitakuwa zimekaribia mwisho wake na tunakaribia kuona Tanzania ambayo kila mwenye makazi anachangia kodi stahili zilizowekwa kihalali na Serikali.