Trafiki jirekebisheni ili kuzuia ajali

Askari wa usalama barabarani akisimamisha gari  

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  10:39

Kwa Muhtasari

Polisi hawafanyi kwa ufanisi wajibu wao kwa kuendekeza rushwa

 

Takriban wiki mbili zilizopita, Rais John Magufuli alinyoosha kidole kwa kikosi cha polisi cha Usalama Barabarani kwa kushindwa kuzuia ajali za barabarani.

Rais Magufuli alisema hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la ajali nyingi za barabarani zinazogharimu maisha ya Watanzania wengi. Alitoa mfano wa mfululizo wa ajali zilizotokea mkoani Mbeya hivi karibuni na kusababisha kupotea kwa maisha ya zaidi ya Watanzania 40, ndani ya muda mfupi. Rais alikitaka kikosi hicho kuchukua hatua za haraka kukomesha hali hiyo. Baada ya onyo hilo la Rais kwa polisi, kwa sasa tunaendelea kushuhudia pilikapilika mbalimbali zikifanywa na kikosi hicho.

Tunaona kazi ya ukaguzi wa magari ikifanyika kwa kasi kupita kiasi, tunaona ongezeko la askari karibu kila barabara, mabaraza ya Usalama Barabarani yanavunjwa nchi nzima na baadhi ya viongozi wa Serikali wanawaomba viongozi wa dini waiombee nchi ili ajali zipungue.

Lakini pamoja na hatua hizo za haraka, binafsi najiuliza tumefikaje mahali hapa pabaya na kumetokea nini na ni hatua gani sahihi za kuchukua kukabiliana na tatizo hili la ajali.

Labda nijieleze kidogo; nimezaliwa jijini Dar es Salaam, miaka 65 iliyopita. Nimeendesha pikipiki kwa zaidi ya miaka 10 kuanzia 1983 hadi 1993.

Nimeendesha gari kwa zaidi ya miaka 25 (kuanzia 1992 hadi sasa). Nilipata leseni ya kuendesha pikipiki na leseni ya kuendesha gari. Sijapata wala sijasababisha ajali. Sijamgonga hata kuku. Nimeyaona mengi, nimefanya mengi na ninaweza kushauri mengi. Kuna maswali yanahitaji majibu kutoka Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kwa kushindwa kutimiza kwa ufanisi wajibu wake kutokana na kuendekeza rushwa na kuwasumbua watumiaji wa barabara hasa wanaoendesha vyombo vya moto. Kwanza; kwa nini, kwa mfano, askari wa kikosi hicho wanambana na mwendeshaji wa gari ambaye kioo cha taa ya ishara ya gari lake kimepasuka, lakini taa yenyewe inawaka na kumtoza faini kwa kumhukumu kuwa amehatarisha usalama? Kwa nini askari hao hao wanamuachia mwendesha pikipiki (bodaboda) anayepita kwenye taa nyekundu bila kumchukulia hatua? Pili, kwa nini askari hao wanamhukumu mtu aliyepinda kushoto na kumwambia kuwa hapo haparuhusiwi wakati hakuna alama yoyote inayokataza hivyo. Mfano ni kona ya Jet, Kipawa ukitaka kwenda kushoto unapotokea Ukonga, wakati sehemu maalumu ya kupindia hapo imezibwa kwa makusudi kwa mawe makubwa ya zege?

Hayo hapo juu ni matukio machache tu ambayo askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani niliyobaini kuwa hutumia mwanya huo kuwanyanyasa na kuwaonea madereva.

Najiuliza, kufanya hivi shabaha yao ni nini? Je, ni kutaka kuongeza makusanyo ya faini au kuhakikisha Sheria ya Usalama Barabarani inafanya kazi yake kikamilifu kwa madereva wa vyombo vya moto? Tangu taratibu hizi za faini za papo kwa papo zianzishwe, zimekukusanywa fedha nyingi, Polisi wenyewe wametangaza lakini bado ajali zinazojeruhi na kuua watu hazijapungua.

Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani kulivyo na ombwe la utoaji wa elimu ya matumizi ya barabara. Pia, inaonyesha ni kwa jinsi gani siku hizi Kikosi cha Usalama Barabarani kisivyowatahini tena wote wanaoomba leseni. Kwa maana nyingine, mtu anaweza kupata leseni hata kama hajui kuendesha gari. Mfano mdogo ni wa marehemu Mayage S. Mayage, aliyekuwa Mwandishi wa Gazeti la Mtanzania, aliwaumbua polisi kwa kutoa ushahidi kuwa alipatiwa leseni kwa muda wa saa sita tu baada ya kutoa nakala nne za picha yake ya pasipoti na Sh100,000 kwa wakala fulani, saa 4 asubuhi na kuletewa leseni kamili, saa 10 alasiri. Kama polisi hawatabadilika, hawawezi kamwe kujinasua kutoka katika lawama hizi.

Vifo barabarani navyo vitaendelea kuongezeka siku hadi siku.

Baada ya habari hiyo kutoka gazetini, sikuona kanusho lolote la Polisi juu ya habari ile.

Kutokana na tatizo la ajira siku hizi, wengi wa hawa wanaendesha magari binafsi, ya abiria na ya biashara wakiwa na leseni lakini hawakutahiniwa.

Wengi wao ndiyo hawa wanaosababisha ajali za ovyo na kuua watu.

Kwa hiyo, kuchukizwa kwa Rais na ajali hizi zisizokwisha ni sahihi. Imebainika kuwa chanzo cha ajali ni rushwa iliyokithiri na utendaji mbovu wa Kikosi cha Usalama Barabarani na siyo bahati mbaya, laana au mapenzi ya Mungu.