http://www.swahilihub.com/image/view/-/5068238/medRes/2310607/-/m43w4s/-/uchambuzi+pic.jpg

 

Tumejiandaaje kuzikabili gharama za matibabu Afya kwa Wote?

Na Herieth Makwetta, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, April 12  2019 at  10:27

 

Wakati Aprili 7 dunia iliadhimisha Siku ya Afya Duniani, ajenda ya Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka huu katika maadhimisho haya ni kuhusu huduma za afya kwa wote bila vikwazo vya kiuchumi, yaani Universal Health Coverage (UHC)

Suala hili la huduma za afya kwa wote ni sehemu ya mpango wa dunia wa maendeleo yaani Sustainable Development Goals.

Bima ya afya ni mhimili mkubwa katika kufanikisha ajenda hii na kusaidia watu kupata huduma za afya bila vikwazo.

Nchi ya Tanzania haijabaki nyuma, kwa sasa inaratibu mpango mpya wa kugharimia huduma za afya (Healthcare financing strategy), lakini swali bado tunajiuliza tutayafikia malengo haya? Dira ya kiujumla ni kwamba malengo haya ya kimaendeleo yafikiwe ifikapo mwaka 2030.

Ukizingatia hatua zilizopigwa kwa sasa, msukumo wa WHO na wadau wengine wa masuala ya afya kuna matumaini kwamba nchi itaweza kufikia malengo ifikapo mwaka mwaka 2030.

Lakini wakati haya yakiendelea, hivi sasa ni asilimia 33 pekee ya Watanzania waliopo katika mfumo wa Bima ya Afya, bado tunajiuliza iwapo tutaweza kulifikia lengo namba tatu la millennia japokuwa mipango bado ni mingi kwa watunga sera.

Wakati muswada wa bima ya afya kwa wote ukitarajiwa kufikishwa bungeni Aprili mwaka huu, Serikali imesema itahakikisha asilimia 70 ya Watanzania ifikapo mwaka 2020 wanakuwa na bima za afya.

Japo taarifa zilizopo ni kuwa kumekuwa na ongezeko la watu wanaojiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Mwaka 2018, wanufaika 856,446 walijiunga na kufanya idadi yao kuwa milioni 3.9 ambao ni sawa na asilimia 7 huku asilimia 69 kati yao wanatoka sekta ya umma.

Ikumbukwe CHF ina asilimia 25 ya wanachama sawa na milioni 2.2 ambao wana wategemezi 13.5 milioni huku bima zingine zikichukua asilimia 1, bado kuna changamoto kutokana na wengi wao kujiunga wakiwa wanaumwa.

Unakuta mtu yupo hospitali ndiyo anakata bima ya afya hii ni changamoto kwa mfuko na walio wengi wanaumwa magonjwa yasiyoambukiza moyo, figo, kisukari ambayo matibabu yake ni ghali, analipia Sh76,800 anasubiri wiki tatu anatibiwa moyo kwa Sh6 milioni.

Kufuatia hili bado kuna wasiwasi mkubwa kufikia mafanikio yale tunayoyatarajia kama nchi.

Bado mikakati mingi inahitajika kuifikia asilimia 70 iliyosalia ambayo ni wananchi walio nje ambao kweli ukiwaangalia, asilimia 28 ni wale waliopo kwenye ngazi ya umaskini lakini asilimia 27 inatuonhyesha bado watu hawana elimu kuhusu bima.

Wakati nchi ikipambana kuyafikia malengo haya katika kuhakikisha afya kwa wote bila vikwazo vya kiuchumi inafanikiwa, magonjwa yasiyoambukiza yameonekana kuumiza mifuko mingi ya bima za afya.

Ukifanya rejea, utafiti uliofanywa na Serikali mwaka 2012, ulibaini kuwa Watanzania wengi zaidi wanaendelea kuwa katika hatari ya kupata maradhi yasiyoambukiza.

Hata hivyo imeelezwa kuwa ifikapo mwaka 2030 gharama za matibabu ya kisukari zitaongezeka na kufikia dola 16.2 bilioni za Kimarekani (takribani Sh40 trilioni), kwa nchi za Tanzania, Kenya na Ethiopia.

Pia, Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa wa moyo nje ya nchi.

Lakini baada ya kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwa kuwafundisha wataalamu wa ndani na kununua vifaatiba na dawa, kwa sasa Tanzania inatumia kiasi kidogo cha fedha kwa matibabu hayo hapa nchini. Licha ya kupunguza gharama za wagonjwa kwenda nje, bado gharama za matibabu hasa dawa bado haziepukiki.

Bohari ya Dawa (MSD) wamekuwa wakitumia zaidi ya Sh22 bilioni kwa mwaka kununua dawa za kutibu magonjwa yasiyoambukiza, huku ikinunua dawa aina 300.

Wakati dawa za magonjwa haya hasa zinazotibu saratani zikiwa ghali, Serikali imeshaunda sera zote dhidi ya magonjwa hayo lakini changamoto ambayo inakabiliana nayo ni namna ya kuhamasisha wananchi wengi kadri iwezekanavyo, hii bado ni dosari katika kufikia afya kwa wote hivyo nguvu za ziada zinahitajika.

Wakati tukiyajadili haya, tukumbuke nchi imebakiza mwaka mmoja tu wa kutimiza malengo hayo (2016-2020), kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kuzuia na Kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), juhudi bado zinahitajika.