Tunaipongeza Serikali mpango mpya wa Tahasusi

Imepakiwa - Monday, April 1  2019 at  09:20

 

Juzi Serikali ilitangaza mpango mpya utakaoanza kutumiwa na wanafunzi wanaohitimu masomo ya kidato cha nne kuanza kufanya chaguo la tahasusi (combination), mara baada ya kumaliza mitihani yao na matokeo yakishatoka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema kuwa mfumo huo ni mpya na unalenga kuwasaidia wanafunzi ili washauriane na wazazi au walezi wao kuhusu kufanya chaguo wanaopenda kulingana na masomo waliyofaulu.

Jafo alisema uchaguzi wa tahasusi kwa mwaka huu utaanza Aprili Mosi hadi Aprili 15 - muda ambao hautaongezwa, lakini ukiwa na lengo la kuwasaidia wahitimu kufanya upya uchaguzi wa tahasusi watakazosomea kidato cha tano na vyuo vya ufundi.

Tayari wadau wa elimu wamekwishazungumzia suala hilo wakiipongeza Serikali kuanzisha mpango ambao unalenga kuwaokoa wahitimu ambao awali walikosea au walifanya chaguo usio sahihi.

Tunaungana na wadau kuipongeza Serikali kuja na mpango huu tukiamini kwamba kuanzia sasa wahitimu watapata uhuru zaidi wa kuchagua masomo ambayo wamefaulu vizuri na vilevile watakuwa na fursa ya kujadiliana vyema na watu wao wa karibu.

Ingawa mpango huu umechelewa, lakini kwa kuanzia si vibaya kwamba, wahitimu ambao walikuwa wakifanya uchaguzi wa tahasusi kabla ya mitihani, tena wakati mwingine bila malengo, hivi sasa watakuwa wakifanya baada ya miezi kadhaa tangu walipomaliza mitihani yao na huenda wakachagua vizuri masomo watakayosoma mbele ya safari yao ya elimu.

Tunajua kwamba utaratibu wa mwanafunzi kufanya uchaguzi kabla ya kufanya mtihani ulikuwa unamnyima uhuru kwa kudhani huenda akafanya vyema na baadaye akafeli, hivyo kwa fursa hii tunaamini kwamba wahitimu watakuwa wanafanya uchaguzi wakizingatia namna walivyofanya mitihani yao na matokeo waliyopata.

Huko nyuma wanafunzi walikuwa wanafanya chaguo wa tahasusi na baada ya matokeo kutoka, baadhi yao walionekana kutofanya vizuri, hivyo kukosa fursa ya kuendelea na elimu ya juu ikizingatiwa kwamba hakukuwa tena na namna nyingine ya kufanya.

Kama walivyosema wadau wa elimu, mpango huu ni fursa nzuri kwa wanafunzi kwa kuwa watapata nafasi ya kutobaki hewani na utawarejeshea matumaini wale ambao wangebaki mitaani na kujikuta wakijiingiza katika makundi yasiyofaa ikiwamo uhalifu.

Wakati tunaipongeza Serikali kwa kuja na mfumo mzuri unaowaruhusu wanafunzi kufanya uchaguzi bora katika elimu yao, tunaamini kwamba hii ni hatua mojawapo ya maboresho yanayofanywa kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa bora zaidi. Hivyo hata changamoto zingine zinazoikabili sekta tunaomba zitazamwe kwa jicho la karibu.

Zipo changamoto nyingi zikiwamo za madarasa, madawati na hata walimu katika shule nyingi zinazomilikiwa na Serikali hususan wale wa sayansi ambazo kwa miaka mingi sasa zimekuwa vilio vya wadau. Tunaiomba Serikali izitolee macho kwa kuzitatua na kuondokana nazo.

Tunasema hivyo kwa sababu mfumo wowote ukiwamo wa elimu una unapaswa kuwa na mfuatano unaoeleweka. Mathalan, iwapo mwanafunzi anasoma shule ya msingi yenye walimu wa kutosha, madawati, vitabu na madarasa yapo ya kutosha akienda sekondari na kukutana na uhaba wa vitu hivyo isitegemewe kwamba atafanya vizuri katika masomo yake.

Hivyo, ni wajibu wa Serikali, wadau na wananchi kushirikiana kuhakikisha kwamba changamoto hizo tatu sugu na nyinginezo zinamalizwa katika mfumo wetu wa elimu ili tuwe na kizazi kitakachoifurahia, lakini pia Taifa lifaidike nacho kielimu katika siku za usoni.