Tutafute dawa ya kudumu ya ajali za petroli

Imepakiwa - Monday, March 11  2019 at  11:33

 

 Habari kwamba watu watano wa familia moja wameteketea kwa moto uliotokana na mlipuko wa petroli na wenzao wawili wanauguza majeraha ya moto huo wilayani Same, Kilimanjaro ni za kusikitisha.

Wakati tukiwaombea marehemu hao pumziko la milele na majeruhi uponaji wa haraka, tumeona ni vyema pia kutafakari kuhusu ajali za namna hiyo tukijiuliza swali, hizi ajali zitaendelea hadi lini?

Kwa mujibu wa taarifa hizo zilizoripotiwa na gazeti hili jana, mmoja wa waliofikwa na mauti hayo alikuwa akimpimia mteja mafuta. Familia hiyo ilikuwa inafanya biashara ya petroli jikoni huku shughuli za upishi zikiendelea katika jiko la mkaa.

Si mara ya kwanza wala ya pili kusikia mlipuko wa petroli umeua watu katika maeneo mbalimbali nchini na katika nchi mbalimbali.

Mathalan, katika miaka ya 1990 ulitokea mlipuko mkubwa katika Kijiji cha Idweli mkoani Mbeya na moto kuteketeza watu wengi waliokuwa wanachota mafuta katika lori lililopata ajali.

Kana kwamba hiyo haikuwa somo, Februari 2015 tukio kama hilo lilijirudia katika kijiji hichohicho kilichopo Kata ya Isongole na kuua watu wengine wawili waliokuwa wanachota mafuta katika lori lililopata ajali.

Tukio baya zaidi kama hilo liliwahi pia kuwapata majirani zetu Kenya ambako watu zaidi ya 100 walifariki dunia na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa wakichota petroli katika lori lililopinduka kwenye mji wa Molo Mkoa wa Rift Valley mwaka 2009.

Ipo mifano tele ya matukio ya moto yanayohusisha mlipuko wa petroli, lakini hii tuliyoitaja inatosha kueleza kwa uzito jinsi mafuta hayo yalivyo hatari na jinsi gani tunatakiwa kuchukua kila aina ya tahadhari tunapokuwa karibu nayo.

Hata hivyo, hatuamini kama juhudi kubwa zimefanyika kuelimisha jamii kuhusu athari za kuwa karibu na mafuta hayo au tahadhari tunazopaswa kuchukua. Na hapo ndipo tunaona kwamba ajali hizo zinajirudia kutokana na watu kukosa elimu ya kutosha.

Hivi wale wanaotembea na spana na kufungua mabomba ya mafuta katika magari na kujaza mafuta katika mifuko ya plastiki, tena katika msululu wa magari wanakuwa wanafikiria nini na mamlaka zinazowafumbia macho zina malengo gani?

Hivi kama inakuwa rahisi askari kusimama barabarani kusubiri waendesha pikipiki wenye makosa mbalimbali inashindikana nini kuwakamata vijana wanaofungua matenki ya magari kuchota mafuta?

Hili ni jambo la kukemewa na kila mtu maana ni la hatari kwa usalama wa kila mmoja anayetumia barabara na vijana hao wasipochukuliwa hatua, na vitendo hivyo kukomeshwa ipo siku tutalia kilio kikubwa zaidi huku tukisema “kama tungejua.”

Si hilo tu, inashangaza na haiingii akilini kuona hadi karne hii mtu anauza petroli ndani ya nyumba anakoishi, tena jikoni ambako shughuli za upishi zinaendelea. Bila shaka Serikali iliyopo kila mahali inamuona na pengine inachukua kodi.

Kwa kuwa bado watu wa namna hiyo ni wengi, kazi kubwa ya kuelimisha jamii inatakiwa kuanzia shuleni ili kuhakikisha masuala yanayohusu usalama wa watu na mali zao yanazama akilini.

Pamoja na kuwapo alama za tahadhari katika magari au katika vituo vya mafuta bado ushirikishaji jamii unatakiwa kuendelea zaidi ili kuepuka ajali kama hizo zinazoweza kuzuilika.

Vilevile hatua madhubuti ziendelee kuchukuliwa dhidi ya vitendo vya kuuza na kununua mafuta katika chupa za maji na vidumu au biashara hizo kufanyika katika maeneo yasiyofaa.

Pia, mamlaka zinazohusika ziendelee kufanya udhibiti katika uanzishaji na uendeshaji wa vituo vya mafuta karibu na makazi ya watu au watu kuvisogelea kwa lengo ama la kuishi au kufanya biashara.

Tahadhari nyingine ni kuendelea kusisitiza elimu kuhusu matumizi ya simu na umuhimu wa kuzima vyombo vya moto tunapokuwa katika vituo vya mafuta.