Tuwekeze kwenye umwagiliaji kukabili mabadiliko ya tabianchi

Na Joseph Mwacha

Imepakiwa - Thursday, April 18  2019 at  11:29

 

Ripoti mbalimbali zinaonyesha mabadiliko ya tabianchi yameathiri uzalishaji wa sekta ya kilimo ndani hata kimataifa.

Inafahamika kilimo kinahusisha uzalishaji mazao ya mimea, misitu, ufugaji wa wanyama, samaki, ndege na jamii nyinginezo. Hivyo Taifa linapoendeleza miundombinu ya kilimo moja kwa moja inahusisha kuhudumia mifugo na samaki.

Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania ni wakulima. Takwimu hizo zinabainisha kuwa wakulima ni asilimia 62.1, wafugaji asilimia 2.4 na wavuvi asilimia moja.

Hata hivyo taarifa mbalimbali zinaonyesha wakulima wengi bado wanatumia nyenzo duni kutekeleza shughuli zao za uzalishaji huku wakikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo mabadiliko ya tabianchi yenye nyingi kwa binadamu.

Mvua ambazo ni muhimu kwa kilimo, hazinyeshi kwa wakati kama ilivyokuwa awali hivyo kuongeza ugumu katika mafanikio ya mkulima.

Moja ya njia ya kisayansi inayoweza kupunguza utegemezi wa mvua zisizotabirika na kuzalisha zaidi katika eneo dogo ni ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Takwimu za mwaka 2018 zinaonyesha Tanzania kuna hekta milioni 29.4 ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kati ya hizo, hekta milioni 2.3 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji mkubwa. Hekta milioni 4.8 zinafaa kwa kilimo cha kati na hekta milioni 22.3 kwa umwagiliaji mdogo.

Hadi Machi 2018, ni hekta 475,052 pekee sawa na asilimia 47.51 zilikuwa zimetumika kati ya hekta milioni moja zilizokusudiwa katika mpango unaokamilika mwaka 2020 na asilimia 1.6 ya eneo lote linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini.

Eneo lililotumika hadi sasa limechangia asilimia 24 ya mahitaji yote ya chakula nchini. Kama asilimia 1.6 limechangia asilimia 24 ya mahitaji ya chakula, ina maanisha matumizi ya asilimia 6.67 ya eneo lote yatakidhi mahitaji ya chakula kwa asilimia 100.

Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Serikali ilikuwa na mpango wa kukamilisha mabwawa 30 ya umwagiliaji na kujenga mapya 40 ili kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na matumizi mengine.

Utekelezaji wa mpango huo hauridhishi kutokana na changamoto kadhaa ikiwamo kutoidhinishwa kadiri ya mipango na bajeti iliyopitishwa na Bunge. Kwa mfano mwaka 2017/18, Wizara ya Maji na Umwagiliaji ilitengewe Sh20.1 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini hadi Machi 2018, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilikuwa imepokea Sh2.5 bilioni.

Pili, ni utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji hali inayodhorotesha kilimo cha umwagiliaji pale wafadhili wanapochelewa au kutotoa fedha kabisa.

Tatu ni baadhi ya maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kutomilikiwa na Serikali. Hii husababisha Serikali kulipa fidia kwa wahusika pindi inapotaka kuyaendeleza.

Nne ni baadhi ya maeneo ya umwagiliaji kutegemea maji vyanzo mbalimbali ikiwamo mito. Mabadiliko ya tabianchi yanapoathiri mito miradi husika hushindwa kutekelezwa.

Haya yote yanatokea licha ya uwepo wa faida nyingi za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Uwepo wa miundombinu ya umwagiliaji husaidia kaya, jamii na Taifa kwa ujumla kuwa na uhakika wa chakula katika kipindi chote cha mwaka.

Pia husaidia wafugaji kuwa na uhakika wa maji kwa ajili ya mifugo na wavuvi kuendesha shughuli zao kiasi cha kukidhi mahitaji yao. Vilevile husaidia kupunguza umasikini kutokana na biashara ya bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi.

Aidha miundombinu ya umwagiliaji husaidia kuepusha mafuriko wakati wa mvua kubwa kwani maji huelekezwa kufuata mkondo wa mabwawa hivyo kuepusha hasara ikiweamo kuharibika au kupotea kwa mali na vifo vya wanyama au binadamu.

Pamoja na mkakati wa Serikali kuikaribisha sekta binafsi kuinua uchumi wa nchi, bado ushiriki sio wa kuridhisha. Ni wakati sasa kwa sekta binafsi kushiriki kilimo cha uwagiliaji ili pamoja na mambo mengine kuwa na uhakika wa chakula na kupambana na umasikini.

Badala ya kila halmashauri kuanzisha skimu yake ya umwagiliaji ambayo hugharimu bilioni kadhaa hadi kukamilika, ni vyema kila mkoa ukateua halmashauri moja kutekeleza mradi mmoja mkubwa utakaohudumia mkoa mzima.

Pili, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iwe na mtaalamu hadi kwenye halmashauri badala ya kuishia ngazi ya kanda ili kuongeza uwajibikaji wa pamoja. Tatu, Serikali ihamishe sekta ya umwagiliaji kutoka wizara ya maji kwenda kilimo ili kurahisisha usimamizi.