UKUTA WA GIZA

Na Patrick J Massawe

Imepakiwa - Thursday, May 9  2019 at  12:31

 

Utangulizi
Alijulikana kwa jina la Marko Kitenge mtoto wa mjini
anayetafuta maisha ndani ya jiji la Dar es Salaam .
Anakutana na Stella Mkwizu dada mzuri pia mwenye
uwezo wa kifedha. Anaendesha gari la kifahari aina ya
Ford Munstang Sports anamilki nyumba huko Mbezi
Beach ufukweni mwa Bahari ya Hindi na ndiko
anampeleka kijana Marko. Mrembo huyo mwenye wingi
wa mali na mapenzi lakini vilevile anafanya biashara
hatari ya dawa za kulevya kwa siri. Hilo ndilo Marko
alitaka kujuana lakini alijutia baadaye baada ya
kuingizwa katika hekaheka nzito inayomwacha mdomo
wazi. Hebu fuatilia hadithi hii nzito na ya kusisimua
kutoka kwa mtunzi wako mahiri Patrick J.Massawe
mpaka mwisho wake.
Jua lilikuwa ni kali sana mchana huo huku pia likiongeza
hali ya joto ndani ya Jiji la Dar es salaam. Muda wa saa
sita na nusu kijana mmoja mtanashati, Marko Kitenge
alikuwa akitembea kwa mwendo wa haraka kuelekea
kwenye kivuko cha kuvukia upande wa pili eneo la
Kigamboni. Hakika alikuwa amechoka hasa kutokana na

mizunguko aliyokuwa akiifanya tangu asubuhi katika hali
ya kutafuta maisha kwa jumla. Na ule ulikuwa ni
utaratibu wake kila panapokucha.
Kwa muda wote aliokuwa akitembea juani alionekana ni
mtu mwenye mawazo mengi yaliyokuwa yanamkabili
kichwani mwake. Upande mmoja begani alibeba kibegi
kidogo ambapo ndani yake alikuwa akihifadhi vitu
mbalimbali muhimu kwa ajili ya kazi zake za kisanii
alizokuwa anafanya na kumpatia riziki. Kimavazi alikuwa
amevalia fulana nyeupe yenye picha ya
mwanamapinduzi wa Cuba Erasto Cheguevara na chni
alikuwa amevalia suruali ya jeans ya rangi ya bluu
iliyopauka na raba nyepesi za rangi nyeupe.
Huku akiangalia saa yake ya mkononi Marko aliongeza
mwenedo kuelekea banda la kusubiria abiria
wanaotarajia kupanda kivuko kwenda ng’ambo ya pili.
Akiwa mbali na banda la kusubiria abiria aliwaona watu
wengi waliokuwa wakisubiri kuvuka, huku kivuko kikiwa
ni kimoja tu kwani kingine kilikuwa ni kibovu na muda
huo kilikuwa kinafanyiwa matengenezo kwenye
karakana ya Jeshi la Wanamaji, Kigamboni.
Kuharibika kwa kivuko kile kulifanya kuwe na adha
kubwa ya usafiri wa kuvuka upande wa pili. Tatizo hili
Marko aliliona na pia alikuwa na haraka ya kuvuka
ukizingatia kuna sehemu nyingine aliyotaka kwahi katika

mihangaiko. Tangu anapoamka asubuhi huwa
anajipangia ratiba ya mizunguko ya siku hiyo na kamwe
hakupenda kuibadili ratiba yake hata kidogo. Sasa baada
ya kufika pale kivukoni ndipo alipoona kuwa ratiba yake
imevurugika na hivyo ikabidi awe mpole. Mcnana ule
Marko alikuwa ametoka kwenye hoteli ya kitalii ya
Mikambo Beach iliyoko Kigamboni ufukweni mwa Bahari
ya Hindi alipokuwa amekwenda kwa ahadi ya kupatiwa
kazi ya ulinzi wa milangoni kwenye ukumbi wa disco
ambalo linafanyika pale kila mwisho wa wiki. Ni ahadi
aliyokuwa ameahidiwa hasa ukuzingatia ni shughuli
alizokuwa anafanya katika kumbi mbalimbali za starehe
zilizoko ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Yeye ni mtu
aliyekuwa amepitia katika mafunzo ya sanaa ya
mapigano kiasi cha kuufanya mwili wake ujengeke
kimazoezi.
Muda siyo mrefu, Marko alifika katika sehemu ile abiria
anasubiria kivuko ambapo palikuwa na abiria wengi
pamoja na magari yaliyopanga mstari yakisubiri
kuvushwa n’gambo ya pili. Wakati huo ndiyo kivuko
kinawajongea taratibu kutoka mjini kuuvuka mkondo
wa Bahari ya Hindi. Baada ya kivuko kufika tu abiria na
magari yaliyokuwa mle ndani yake yakatoka na kuwapa
fursa abiria kupanda akiwamo Marko. Abiria walikuwa ni
wengi waliochanganyika na magari kitu ambacho
kilisababisha msongamano mkubwa ulileta karaha kwa

wasafiri lakini hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuivumilia
hali ile ya miaka nenda rudi.
Hatimaye kivuko kikaondolewa hadi walipofika upande
wa pili upande wa jiji na abiria wakashuka mmoja baada
ya mwingine akiwemo yeye halafu akalitoka eneo lile la
kivuko na kutoka nje kabisa kuelekea kituo cha daladala.
Hata hivyo hakupanda basi bali aliendelea na safari yake
kufuata barabara ya Kivukoni Front kuelekea maeneo ya
Posta ya Zamani . Kwa mbali Marko alikuwa akidokolea
macho bandari iliyokuwa inaonekana kwa mbali meli
kubwa kadhaa zilizokuwa zikipakia shehena. Hadi
alipofika kwenye kituo cha mabasi yaendeyo kasi , Posta
ya Zamani alikutana na umati mkubwa wa watu
waliokuwa wanaelekea sehemu mbalmbali za jiji la Dar es
Salaam.
Hata hivyo, Marko hakusimama pale kwenye kituo hicho
bali aliamua kuendelea na safari yake kuelekea eneo la
Stesheni ambapo alizoea kula chakula cha mchana katika
mgahawa mmoja aliozoea.
Marko alifuata Barabara ya Sokoine Drive kisha akavuka
uande wa pili kupita usawa wa iliyokuwa Shule ya
Msingi ya Forodhani na kuendelea hadi alipouvuka Mtaa
wa Bridge na kuelekea usawa wa Kanisa Kuu la Mtakatifu
Joseph . Wakati huo bado jua lilikuwa kali sana na
kusababisha joto lililomfanya Marko alowe jasho

chapachapa mwili wote huku akitamani kuivua ile fulana
nyeupe aliyokuwa amevaa.
Magari yalikuwa ni mengi ambayo yalisababisha
msongamano mkubwa . Mbali ya magari kuwa mengi pia
walikuwapo na wapita njia waliokuwa katika
mihangaiko yao kama alivyokuwa yeye. Walikuwa
wakipishana huku wakipigana vikunbo lakini hayo yote
hakuyajali. Marko aliendelea na safari zake. Wakati
alipokuwa akivuka Barabara ya Mtaa wa Bridge, gari
moja dogo aina ya Ford Muntang Sports ya rangi
nyekundu ilisimamishwa mbele yake na kupaki kando ,
usawa wa eneo la ofisi za kampuni za meli na boti za
kwenda kisiwani Zanzibar. Lilikuwa ni gari maalumu
lililotengenezwa kwa kubeba watu wawili tu, dereva na
abiria mmoja. Pia ni magari yaliyotumiwa na wenye
uwezo mkubwa wa kifedha mfano kama wasanii
wakubwa, wafanyabiashara wakubwa na kadhalika.
Dereva wa gari hilo alikuwa ni mwanadada mrembo wa
nguvu ambaye muda huu alikuwa ameukumbatia usukani
huku akimkodolea macho mazuri kama vile alikuwa
anamfananisha au anamfahamu. Hata hivyo baada ya
kulipaki gari kando , mwanadada huyo aliufungua mlango
wa upande wa kulia na kumwita Marko kwa ishara ya
mkono na wakati huo alishaanza kuondoka, kuendelea
na safari yake aliyopanga, bila kuhangaika na

mwanadada huyo. Lakini kabla ya kuvuka barabara
Marko alisita kidogo huku akimwangalia mwanadada
huyo kama alikuwa anamwita.
“Unaniita mimi?” Marko akamuuliza mwanadada huyo
ambaye alikuwa anamwangalia kwa sura ya tabasamu.
“Ndiyo nakuita wewe kaka…” mwanadada yule akasema
huku akiendelea kumwangalia kwa macho yake mazuri
yaliyokuwa na mvuto.
“Sawa” Marko akasema na kugeuza na kumwendea pale
alipokuwa amepaki gari upande wa pili wa barabara.
Mwanadada yule akabaki akimwangalia huku ameunda
tabasamu pana.
“Hali yako?” Marko akamsabahi baada ya kumfikia.
“Nzuri kaka! Mambo?” Mwanadada yule akamwambia .
“Mambo safi. Unasemaje dada ‘angu?”
“Nina shida na wewe” akamwambia na kuongeza.
Naomba kama una nafasi tuongozane wote …”
“Shida gani tena dada?” Marko akamuuliza . Akawa na
mshangao!
“Usihofu kaka.” Mwanadada yule akamwambia kwa
upole.
“Kwa nini nisihofu? Na safari ya kwenda wapi wakati
sikufahamu dada angu?”

“Twende tu nina maongezi nyeti na wewe . Pia nafikiri
kuna sehemu nilikuona wewe au sivyo?”
“Nadhani lakini sikumbuki “ Marko akamwambia huku
akijaribu kuvuta hisia kuwa waliwahi kuonana wapi. !
Utakumbuka tu …” usihifu wewe ni mtoto wa kiume.
Tuondoke gari liko barabarani . Trafiki wanaweza
kunikamata …”Manadada yule akamwanbia huku
amekamata kirungu cha gea tayari kwa kuondoka.
magari nayo yalikuwa ni mengi katika barabara hiyo ya
Sokoine Drive kitu ambacho kilisababisha foleni kubwa
mchana huo kama ilivyo ada ndani ya Dar es Salaam.
“Ok, twende.”Marko Kitenge akasema huku akizunguka
upande wa pili na kuufungua mlango upande wa
kushoto. Baada ya kuufungua mlango aliingia ndani ya
lile gari la kisasa ambalo ni maalumu kwa kubeba watu
wawili tu na si vinginevyo. Baada ya kuondoka tu dada
yule aliliondoa gari kwa mwendo wa madoido kiasi cha
kuonyesha ujuzi wake wa kumiliki chombo kile cha
moto. Baadhi ya watu waliokuwa wanakaa upande wa
pili katika ofisi za mawakala wa meli na boti za kwenda
Zanzibar wakabaki wakishangilia…” Mwanadada yule
alimuuliza huku ameangalia mbele.
“Mimi sijambo…” Marko akaitikia huku akiendelea
kumwangalia kwa chati.
“Jina langu naitwa Stella Dickson Mkwizu…”
Alijitambulisha kwa sauti nyororo aliyoirembesha
mdomoni ambayo ingeweza kumtoa hata nyoka pangoni.
“Nashukuru sana kukufahamu. Na mimi naitwa Marko
Kitenge . Marko akajitambulisha kwake.
“Oh usihofu braza tunakwenda nyumbani kwangu Mbezi
Beach…”
“Tunakwenda Mbezi Beach…?” Marko Kitenge
akamuuliza.
“Ndiyo ni nyumbani kwangu. Mengi tutaongea huko au
sivyo?”
“Lakini nina ratiba nyingine dadaagu…” Marko
akamwambia.
“Usihofu kuhusu ratiba braza. Utaendelea na ratiba yako
baada ya kutambulishana au vipi?”
Hakuna taabu. basi tunaweza kwenda…” Marko akasema
huku akiwa haamini kilichokuwa kinaendelea. mbele ya
macho yake.
Ni kama vile Marko alikuwa ndotoni tena ndoto ya
mchana kweupee! Hivi imekuwaje amekutana na
mwanadada huyu anayeonekana kwa mtu wa gharama
aliye tawi la juu? Hata hivyo alivuta subira huku
wakiendelea na safari yao kwa kukata mitaa kadhaa ya
Jiji la Dar es Salaam lilivyokuwa na msongamano mkubwa
wa magari hadi walipotokeza katika Barabara ya Ali
Hassan Mwinyi ambayo nayo waliifuata hadi walipofika
Oysterbay. Wakaifuata barabara ya Obama ambayo
waliendelea nayo huku Marko akiendelea kushangaa na
wala hakuweza kuongea chochote kwa muda ule zaidi
ya kusubiri kitakachoendelea huko mbele ya safari
aliyokuwa anapelekwa.
Ni hadi walipofika mwisho wa safari eneo la Mbezi Beach
pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam. Kwa hakika eneo
hilo lilikuwa tulivu ambalo wamejenga watu waliokuwa
na uwezo wa kifedha na nguvu za kiuchumi. Majumba ya
kifahari yaliyojengwa sehemu hiyo ndiyo yaliyodhihirisha
uwezo wao dhidi ya watu wengine wa kipato cha chini
ambapo uwezo wao ni wa kuishi sehemu za Mbagala,
Keko, Manzese, Tandale, Buguruni, Temeke na
kwingineko palipokuwa na msongamano wa watu kiasi
cha kukosa hewa nzuri na miundombinu duni.
Gari lilifuata barabara ndogo ya kokoto iliyokuwa
inaelekea kwenye jumba moja la kifahari lililokuwa
limezungukwa na geti kubwa ya chuma kwa upande a
mbele na ni moja ya majumba yaliyoota kama uyoga
katika mtaa huo. Baada ya kufika getini Stella alipiga honi
mara mbili na geti likafunguliwa na mlinzi mmoja wa
kampuni ya binafsi anayelinda hapo. Gari likaingia hadi

ndani ambapo alilipaki katika sehemu ya maegesho
mbele ya jumba hilo karibu kabisa na bustani kubwa
iliyozungukwa na kichaka cha maua kando ya bwawa la
kuogelea.
Ama kweli Marko alizidi kuchanganyikiwa na kuendelea
kujiona akiwa katika ndoo hali ile ya kusisimua mchana
huo. Wote wawili walishuka garini halafu Marko akabaki
amesimama huku akishangaa na kumwangalia Stella
aliyekuwa akimwona kwa uwazi zaidi.
Alikuwa amevalia suruali ya jeans iliyobana na kuweza
kuonyesha umbile lake. Pia alivalia fulana isiyokuwa na
mikono huku kichwa chake kilisetiwa nywele vizuri na juu
ya paji lake la uso alikuwa amepachika miwani mieusi ya
jua. Alionekana ni mwanadada wa kileo anayekwenda na
wakati.
“Marko karibu…hapa ndio nyumbani kwangu “ Stella
alimwambia Marko huku akiandaa tabasamu pana.
“Oh aksante sana .” Marko akasema huu akimfuata
nyuma Stella, kuliendeea lile jumba la kifahari lililokuwa
liezungukwa na miti pamoja na bustani za maua kiasi
kuonekana kama himaya ndogo ya kifalme.
Hatimaye wote wakaingia ndani ya jumba lile na kufikia
kwenye sebule nadhifu ambayo Marko alikaa katika sofa
dogo kati ya masofa ya thamani yaliyokuwa pale. Baada
ya sekunde kadhaa akiwa anaangaza macho yake pande
zote za sebule ile akiangalia jinsi watu walivyokuwa
wanaishi maisha ya peponi. Kwani kulikuwa kumeenea
samani za gharama kubwa ambazo mtu wa kawaida siyo
rahisi kuzimiliki.
Kwanza kabisa nyumba hiyo ilikuwa imenakshiwa na
rangi za aina mbalimbali kwa upande wa ndani. Sebuleni
palikuwa pamepakwa rangi ya kijani iliyopauka, sehemu
ya kulia chakula nako palikuwa na rangi ya machungwa
na sehemu nyingine zilikuwa na rangi ya zambarau.