http://www.swahilihub.com/image/view/-/2165278/medRes/620420/-/jjf31o/-/NderituNjoka.jpg

 

Ubabe huu wa kijinsia haumfaidi yeyote

Nderitu Njoka

Mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanaume Nderitu Njoka. Picha/EVANS HABIL 

Na MHARIRI WA TAIFA LEO

Imepakiwa - Thursday, December 21  2017 at  14:21

Kwa Mukhtasari

WAZIRI wa Elimu Dkt Fred Matiang’i Jumatano alitangaza matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE), na kuwapongeza wanafunzi wasichana kwa kufanya vyema.

 

Kwa mara nyingine katika mtihani wa kitaifa, wasichana wameonekana kuwapiku wavulana huku Waziri Matiang’i akitoa changamoto kwa wavulana kutia bidii zaidi ili wasishindwe na wasichana.

Chama cha Maendeleo ya Wanaume (MAWE) kimekerwa na hali hii kikilalamika kuwa matokeo duni ya wavulana yamesababishwa na hatua ya jamii kumuangazia zaidi ya mno mtoto msichana.

Mwenyekiti Nderitu Njoka anasema kila kitu sasa, ikiwemo ufadhili wa serikali, kinafanywa kwa kuwazingatia zaidi wanawake na wasichana kwa hasara ya wanaume na wavulana.

Njoka anataka serikali kuunda sera mahususi za kuhamasisha mtoto wa kiume, kama ambavyo imekuwa kwa mtoto wa kike.

Mashirika ya kuhamasisha wanawake yametofautiana vikali na Njoka, yakitaka kujua kwanini wanaume hawakulalamika wakati wavulana walikuwa wakipepea katika mitihani ya kitaifa.

Huu ni mjadala ambao hautakoma. Isitoshe, kila upande unaenda kombo katika suala hili.

Kwanza, tunakosea kwa kuwagawanya watoto wetu kwa misingi ya kijinsia – huu ni ubaguzi. Iwapo ni lazima tuchukue mkondo huo, iwe ni kwa sababu tumebaini upungufu fulani, wa kweli, katika jinsia moja na tunatafuta suluhisho la kudumu.

Pili, malezi yetu nyumbani lazima yabadilike ili tuwapatie mazingira sawa wavulana na wasichana. Kusiwe na kazi za wasichana na za wavulana: kila mtoto apige deki, aingie jikoni, akachunge mifugo na kuteka maji. Wote wafanye kazi zote, kulingana na uwezo wao, ama wasifanye zozote.

Tatu, shuleni pia kusiwe na masomo ya wasichana na ya wavulana. Tujiulize kwanini wasichana walibobea katika lugha kuliko wavulana. Kwa upande mwingine, kwanini wavulana walifanya vyema zaidi katika sayansi kuliko wasichana.

Lengo ni kuhakikisha wanafunzi wote wanafanya vyema katika masomo yote.

Tatu, pengine umewadia wakati wa kuunganisha kampeni hizi za hamasisho zifanywe sambamba kwa pamoja ili kusiwe na upande utakaohisi kuachwa nyuma.

Hakutakuwa na hofu zozote za ubabe wa jinsia moja iwapo kila mtoto atapata nafasi sawa katika jamii.