Ubambikiaji kesi wananchi ufike mwisho

Imepakiwa - Friday, April 5  2019 at  09:28

 

Kama tutawahesabu viongozi mbalimbali waliowahi kutoa kauli dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi kuwabambikia kesi wananchi, hatutawamaliza.

Juzi, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga ameingia katika orodha ya viongozi hao ambao wamewahi kwa nyakati tofauti kukemea tabia ya askari kuwabambikia kesi wananchi.

Akizungumza katika kongamano la watoa huduma za kisheria jijini Arusha, Dk Mahiga alisema tabia hiyo inaathiri utawala wa sheria na kuwafanya wananchi kutokuwa na furaha na Serikali yao.

Ubambikiaji kesi hasa kutoka kwa askari wasio waaminifu, ni suala la miaka nenda rudi na kinachoonekana ni kama vile wahusika wameamua kuweka nta masikioni.

Matokeo ya kuwabambikia wananchi kesi yanaweza kujidhihirisha kwa sura nyingi ikiwamo mlundikano wa mahabusu na wafungwa magerezani. Tunapotoa kilio cha magereza yetu kuelemewa, kumbe yamekuwa yakipokea hata watu wasio na hatia.

Ikumbukwe kuwa kumuweka mahabusi au kumfunga hata mtu mmoja bila hatia ni kupunguza nguvu kazi ya Taifa. Aidha, ni kitendo kinachoweza kuwaathiri kimaisha watu wengi walio nyuma ya mtu huyo.

Tujiulize hivi ni wananchi wangapi maskini waliokaa mahabusu, kufungwa magerezani, kulipishwa faini au kupewa adhabu nyingine mahakamani kutokana na kitendo cha baadhi ya askari kuwabambikia kesi?

Ni dhahiri kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiteseka tena kwenye mikono ya watu waliopaswa kuwa ndio msaada kwao. Licha ya suala hili kuonekana kuwa ni tatizo sugu, bado kunahitajika jitihada za kulivalia njuga ili askari wanaofanya kitendo hiki wasiendelee kuipaka matope Serikali.

Sehemu ya jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha utawala wa sheria na utekelezaji wa Sheria ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017.

Tunaamini pamoja na mambo mengine, usimamizi thabiti wa sheria hii unaweza kuwasaidia wananchi wasioelewa mashtaka, wanaokiri makosa ambayo hawakuyatenda kwa sababu tu ya kutojua cha kusema au namna ya kukisema wanapokuwa kwenye mikono ya vyombo vya dola au mahakamani.

Kuwapo kwa watoa huduma hawa kutasaidia kupunguza vitendo vya uonevu wanavyofanyiwa wananchi hasa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za msaada wa kisheria kutoka kwa mawakili.

Ikumbukwe kuwa jukumu la watoa huduma za msaada wa kisheria ni kuwawezesha na kuwatetea wananchi wasio na uelewa na ambao kwa namna moja ama nyingine wako hatarini kudhulumiwa haki zao.

Tunaziomba taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali kulishupalia suala hili kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu masula ya msingi kama vile makosa na sheria ya jinai, mwenendo wa mashtaka, haki za mtuhumiwa na mengineyo mengi ambayo kwa sababu ya wananchi kutoyaelewa, baadhi yao wamewahi kuonewa na askari wenye nia ovu.

Kikubwa zaidi kwa kuwa huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu uliofurutu, matamko ya kupinga tabia hii pekee hayatoshi.

Badala ya kulalamika kama tunavyoona mara kwa mara, viongozi wakiwamo wenye dhamana ya Jeshi la Polisi wawachukulie hatua za kinidhamu na za kisheria askari wanaohusika. Na hilo lisifanyike kimyakimya, wananchi watangaziwe hatua zinapochukuliwa.