Uchambuzi:Tukumbuke huduma ya chakula shuleni

Imepakiwa - Thursday, March 14  2019 at  09:53

 

Tunapojadili mpango na bajeti kwa mwaka 2019/20 tukumbuke na huduma ya chakula shuleni.

Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili Tanzania (Tuki) inaeleza kuwa chakula ni kitu chochote kinacholiwa ambacho huupatia mwili nguvu na joto.

Ripoti ya Programu ya Chakula Duniani (WFP) ya mwaka 2008 inaeleza kuwa huduma ya chakula ni ugawaji wa chakula au vitafunio shuleni kwa wanafunzi ama kuwapelekea nyumbani kwa ajili ya familia zao.

Zipo faida nyingi kwa wanafunzi kupata huduma ya chakula shuleni hasa kuongeza uwezo wa kufikiri, kujadili, kutatua changamoto na kuhimili masomo muda wote wa vipindi.

Tukijikita kwa upande wa elimu ya awali, msingi hadi kidato cha nne ni shule chache zinazotoa kwa ukamilifu huduma ya chakula shuleni. Wanafunzi pekee ambao kwa asilimia 100 wanapata huduma ya chakula ni wale wanaosoma kwenye shule za bweni.

Kimsingi ili kufanikisha kutoa huduma ya chakula shuleni, kwa mtazamo wangu wadau wakuu wanne wanahitajika.

Wadau hao ni wanafunzi, wazazi, Serikali na jamii.

Zipo changamoto kadhaa zinazotajwa kukwamisha utekelezaji wa utoaji wa huduma ya chakula shuleni.

Moja ya changamoto hizo ni mtazamo hasi uliojengeka miongoni mwa wazazi kuwa huduma zote kwa wanafunzi zinapaswa kutolewa na Serikali.

Mzazi anapojitoa kwenye jukumu zima la kumsaidia mtoto kupata elimu na kuiachia Serikali ndipo changamoto ya msingi inapoibuka. Hii inatokana na ukweli kuwa Serikali pekee haiwezi kutoa kikamilifu huduma ya chakula shuleni.

Jamii inayozunguka eneo la shule au yenye uhusiano na shule husika ina jukumu la kuwasaidia wanafunzi kupata huduma ya chakula kwa kutoa fedha taslimu au kwa kununua mahitaji ya chakula ikiwamo mahindi/unga, maharagwe na mengine.

Ili kutekeleza jukumu hili muhimu kwa wanafunzi wa Tanzania, ipo miundombinu inayopaswa kuwapo ili kufanikisha kwa ufanisi utekelezaji wake.

Shule zote zinapaswa kuwa na miundombinu ya kupikia kwa maana ya majengo, vifaa na kuajiri wapishi pamoja na walinzi wa kulinda bidhaa na miundombinu.

Pili, uwapo wa vyanzo vya maji na miundombinu ya kuhifadhi muda wote wa masomo. Tatu ni vyanzo vya uhakika ambavyo ni rasilimali fedha au bidhaa.

Hii ni huduma inayopaswa kuwa na uhakika wa malipo kwa wazabuni endapo taasisi itaamua kupata huduma kwa njia hiyo au kamati maalumu itakayokuwa inaratibu na kusimamia utoaji wa huduma hii shuleni.

Utaratibu uliopo sasa kwa shule nyingi za msingi na sekondari ni kwa wanafunzi kuingia asubuhi na kisha kuahirisha masomo kati ya saa sita na saba mchana na baadaye kurejea shuleni kuendelea na vipindi hadi alasiri.

Muda huo wa mapumziko ya kipindi cha mchana unalenga wanafunzi kurudi nyumbani kwa ajili ya kupata mlo wa mchana na kisha kurudi tena shuleni kuendelea na masomo.

Taarifa mbalimbali zinaonyesha wanafunzi walio wengi huwa hawapati chakula cha mchana wanaporudi majumbani.

Mara nyingi wazazi au walezi wao hutajwa kuwa katika majukumu mengine ikiwamo shughuli za kilimo, ufugaji, uvivu na nyingine za kujiongezea kipato. Hata pale wanapowakuta wazazi au walezi wao, huduma hiyo haipatikani au hupatikana chini ya matarajio kutokana na hali ya kiuchumi katika familia.

Huduma ya chakula shuleni inatajwa kuwa mkombozi wa watoto wengi wa Kitanzania pale itakapotekelezwa kwa vitendo na kuwa na ufuatiliaji wa mara kwa mara.

Huduma ya chakula shuleni inatajwa kupunguza utoro na kuongeza ufaulu katika shule zinazotoa huduma hiyo kulinganisha na zile ambazo hazitoi.

Pamoja na kusaidia watoto kuhudhuria shuleni pia inaongeza uwezo wa watoto kufikiri na kuwa mahiri muda wote wa vipindi.

Serikali inapambana kuibua na kuimarisha viwanda ili kuwa nchi ya viwanda na kuelekea uchumi wa kati, waendelezaji wa viwanda hivyo kwa upande wa utaalamu wa uendeshaji na ufundi ni hawa wanafunzi waliopo shuleni sasa. Swali ni je, Serikali ina lengo la kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa Watanzania wenyewe kumiliki na kuendesha viwanda hivyo?

Na siyo kuwa vibarua na kupewa nafasi za kazi zisizo na staha? Naamini jibu ni ndiyo. Hiyo itakuwa na maana zaidi pale tutakapoweka nguvu kubwa kuimarisha mfumo mzima wa utoaji wa elimu katika shule zetu.

Mwandishi anapatikana kwa simu namba 0685 - 214949 au 0677 - 185865