Uchambuzi wa Leo: Ufumbuzi wa tatizo la usafiri Dar

Magari ya mwendokasi kituo cha Kimara mwisho jijini Dar es salaam 

Imepakiwa - Thursday, March 7  2019 at  10:17

 

 Kila uchao, watu wanakimbizana na maisha ambayo kwa kiasi kikubwa yanategemea kipato kwani bila fedha hali inakuwa ngumu. Hakuna cha bure, labda hewa pekee.

Ili kukidhi mahitaji ya msingi ikiwamo chakula na malazi, ni lazima uwe na chochote mfukoni. Kwa msingi huo, ni muhimu kuchakarika kila kukicha. Iwe mjini au shambani, lazima tufanye kazi kwa bidii ili kupata chakula cha kila siku.

Kwa kuitambua kanuni hiyo, wengi tunaamka mapema ili tufanye kazi na kujipatia riziki zetu. Kwa upande mwingine, Serikali inafanya kazi nzuri ya kujenga miundombinu muhimu kurahisisha mawasiliano. Jijini Dar es Salaam, kuna huduma ya mabasi mwendokasi kutoka Kimara hadi Kivukoni, Morocco na Kariakoo.

Mabasi hayo yameleta ahueni kwa misingi kuwa ukibahatika kupanda unawahi kufika uendako tofauti na usafiri mwingine wa umma. Huduma za mabasi haya zinategemewa na watu wengi kuelekea au kutoka Feri, Gerezani na Morocco au Kimara.

Mimi ni mtumiaji mzuri wa huduma hii lakini tangu kuanzishwa kwake kumekuwapo na kero nyingi sana. Kwanza ni uhaba wa mabasi kipindi abiria wanapokuwa wengi.

Pili, mabasi kujaa kuliko uwezo wake hivyo kusababisha adha kubwa wakati wa kupanda au kuteremka. Kiini cha changamoto hii ni abiria wengi kusubiri muda mrefu vituoni wakiwa wamesimama hivyo kulazimika kujazana kupita kiasi.

Vilevile, hatuna utaratibu wa kujipanga kwa mistari ili mabasi yakipatikana watu waingie kulingana na walivyowasili kituoni. Tukianzisha utaratibu wa aliyewahi kufika kituoni ndiye aingie kwanza, yatakuwa ni maboresho makubwa.

Changamoto nyingine ni licha ya vituo vya kusubiria mabasi kujengwa kwa gharama kubwa, vingi havina huduma za msingi kwa ajili ya huduma kwa abiria wanaosubiri usafiri kama vile vyoo au viti na vioski vinavyouza vitu vidogo vidogo mfano juisi, chai au maji ya kunywa.

Abiria anajikuta amesimama muda mrefu pengine hata zaidi ya nusu saa akisubiri mabasi lakini wapambayo hayaonekani. Vituo kama Kimara-mwisho, Korogwe, Fire, City Council (Nyerere Square) Feri (Kivukoni) na Gerezani kuna watu wengi sana na msongamano ni mkubwa.

Hivyo kupata basi ni shida kupindukia hasa ukichukulia uhalisia kuwa abiria anakuwa ameishasimama muda mrefu halafu mabasi yakija yamejaa hivyo hayasimami.

Haifahamiki kero hizi zitaisha lini hata tunajiuliza kulikoni mwendiokasi, je, ni laana badala ya baraka tuliyoisubiri muda mrefu? Naiomba menejimenti ya mwendokasi iwajibike ipasavyo na kuhakikisha huduma inaboreshwa hata kama mabasi hayatoshelezi.

Kufanikisha hilo, nashauri mambo kadhaa kwa faida ya wote. Kwanza usimamizi uimarishwe maradufu ili kuhakikisha mabasi machache yaliyopo yatoe huduma ya kuridhisha.

Vilevile, vituo vyenye abiria wengi mfano Kimara, Korogwe, Ubungo, Fire na Kivukoni kuwe na utaratibu wa abiria kupanga misitari ili wapande kwa utulivu na amani na basi likijaa liondoke pasipo kusukumana wala kukanyagana.

Wasimamizi wahakikishe abiria wanaoteremka wanafanya hivyo kwanza kabla ya wanaopanda. Hali ilivyo sasa, wanaoteremka wanasukumwa na wanaopanda kiasi kwamba inakuwa kero.

Ni vizuri mabasi yatakayoagizwa yawe na milango ya kuteremkia sehemu ya mbele karibu na dereva na milango ya kupanda iwe kati na nyuma. Hii itarahisisha kushuka au kupanda kwani abiria akijua anataka kushuka, asogee mbele.

Uongozi uhakikishe vipindi vya abiria wengi; asubuhi na jioni, mabasi yawe mengi na yasimamiwe vizuri na yafanye kazi ipasavyo.

Inaeleweka kuwa kampuni inayotoa huduma ni moja hivyo iwapo imezidiwa ziruhusiwe nyingine kutoka sekta binafsi kuagiza mabasi ili kuongeza nguvu. Kinachotakiwa ni kuboresha huduma si abiria wateseke kwa kutokuwapo mabasi ya watoa huduma wengine.

Abiria ni wengi hivyo mabasi yawe mengi pia mpaka tuseme naam sasa tupo mwaka 2019 tukielekea uchumi wa viwanda na kipato cha kati bila mizengwe. Kinachotakiwa wenye uwezo wapewe vigezo vya mabasi yanayohitajika kulingana na miundombinu iliyopo, naamini watafanya kweli.

Mwandishi ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori). Anapatikana kwa baruapepe fkilahama@gmail.com