http://www.swahilihub.com/image/view/-/4532650/medRes/1954602/-/4mvdyyz/-/mali.jpg

 

Kuihusu Ufaransa licha ya mgogoro wa kidiplomasia kati yake na Italia

Emmanuel Macron

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ahutubu katika kongamano la siku mbili la kutafuta ufumbuzi wa jinsi ya kuzima ufadhili wa makundi ya kigaidi lililoandaliwa Aprili 26, 2018, jijini Paris. Picha/AFP 

Na SAMMY WAWERU, MASHIRIKA na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  17:35

Kwa Muhtasari

Waziri wa Biashara na Uchumi wa Italia, Roma Giovanni Tria, Jumatano amefutilia mbali ziara yake katika nchi ya Ufaransa kwa msingi kuwa meli ambayo angeabiri nayo imejaa abiria.

 

WAZIRI wa Biashara na Uchumi wa Italia, Roma Giovanni Tria, Jumatano amefutilia mbali ziara yake katika nchi ya Ufaransa kwa msingi kuwa meli ambayo angeabiri nayo imejaa abiria.

Hii ni kwa mujibu wa habari zilizochapishwa kwenye ukurasa wa akaunti ya Twitter ya Wizara yake.

"Waziri Giovanni Tria amefutilia mbali ziara yake ya kikazi kuonana na waziri wa Biashara Ufaransa Bruno LeMaire," linasema chapisho hilo.

Chapisho hilo linaeleza kwamba ziara hiyo ilisitishwa kutokana na ombi la nchi ya Italia.

"Mkutano kati ya mawaziri hao ulikuwa na manufaa ya aina yake kwa kuwa walitarajiwa kujadili maswala kuhusu kongamano la muungano wa EU wa hapo Juni," linasema.

Waziri Tria alisema anatumai mkutano mwingine utaandaliwa hivi karibuni.

Hata hivyo, mkutano wake wa Alhamisi na waziri wa biashara wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Berlin utaendelea kama ulivyoratibiwa

Uamuzi wa waziri huyo umejiri baada ya Roma kutaka msamaha kutoka kwa Ufaransa kufuatia kauli yake jinsi Italia ilivyoshughulikia meli iliyowachwa katika bahari ya Meditarenia ambapo raia 629 wa Libya waliokolewa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alicharura Italia, akiitaja kama nchi tepetevu kwa kutoruhusu meli hiyo kushusha abiria hao wa Libya katika bandari yake.

Endapo Ufaransa haitakuwa imeomba radhi, mkutano wa waziri wa usalama wa ndani Italia Matteo Salvini na Rais Macron Paris mnano Ijumaa hautafanyika.

Kuihusu Ufaransa

Ufaransa ni mojawapo ya nchi ambazo viongozi wanaokutwa hatiani kuhusika kwa sakata za ufisadi mkono wa sheria hauwaponyoki.

Mfano, ni wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Nicolas Sarkozy anayeandamwa na kuchunguzwa vikali kuhusu tuhuma kupokea pesa za kufadhili kampeni zake miaka ya awali kutoka kwa kiongozi wa zamani Libya Kanali Muammar Gaddafi.

Maafisa wa polisi Ufaransa wanachunguza tuhuma hizo kuhusiana na ufadhili wa fedha alizotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa urais mwaka wa 2007.

Bw Sarkozy awali, aliwahi kuhojiwa na polisi. Mahakama ilisema rais huyo wa zamani alihojiwa Nanterre, Magharibi mwa Paris. Mnamo 2012 alishindwa katika juhudi zake za kutaka kurejea madarakani.

Mwaka wa 2013, Ufaransa ilianzisha uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba timu ya kampeni ya Sarkozy ilipokea mchango kutoka kwa hazina ya 'pesa haramu' za Gaddafi.

Tuhuma hizo zilitolewa na mfanyabiashara Mfaransa mwenye asili ya Lebanon, Ziad Takieddine na baadhi ya maafisa wa zamani wa Gaddafi.

Raia wa nchi hiyo wanaonekana kuwa wasiostahimili viongozi wafisadi, kwa kumrambisha sakafu Sarkozy katika uchaguzi wa 2012. Hayo ni kinyume na taifa la Kenya ambapo viongozi wanaohusishwa na kashfa za ufisadi wameonekana kurejea madarakani kupitia viti vya kisiasa.

Si ajabu kuona washukiwa wakuu wa sakata ya ufisadi katika shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) 2022, wakiwania nyadhifa za kisiasa. Hayo Ufaransa ni historia, nchi hiyo ikiamini ufisadi ni makosa makubwa yasiyofaa kupewa mwanya.

Hata hivyo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameonekana kukaza kambi katika vita dhidi ya ufisadi akishikilia “viongozi wafisadi hawana nafasi chini ya utawala wangu”.

Taifa hilo linaloonekana kukua kidemokrasia ni la aina gani? Paris ndio mji wake mkuu na mkubwa, wenye ukubwa wa kilomita 105.4 mraba.

Unapatikana Ufaransa Kaskazini, huku Ufaransa ikiwa ni nchi ya Ulaya na mwanachama mwanzilishi wa Umoja wa Ulaya. Nchi hiyo ina ukubwa wa kilomita 674,843 mraba na kukadiriwa kuwa na zaidi ya watu 63,044,000.

Imepakana na Ubelgiji, Luxemburg, Ujerumani, Uswisi, Italia, Monako, Andorra na Hispania.

Lugha ya taifa nchini humo ni Kifaransa, japo kuna lugha za maeneo kama vile Kibaski, Kibretoni, Kikatalani, Kikorsika, Kijerumani, Kiholanzi na Kioxitania. Hata hivyo, wahamiaji kutoka nchi zilizokuwa koloni za Ufaransa walileta lugha kama Kiarabu na Kiberber kutoka
Afrika Kaskazini.

Ubia wa kipekee

Ufaransa ni kati ya nchi zenye makoloni mengi ambapo ilisambaza lugha yake kote duniani na kutunza uhusiano wa pekee na nchi nyingine zinazotumia Kifaransa.

Utawala wa makoloni hayo ulianza katika karne ya 19, na mengi hasa yalitoka Afrika. Wakati wa vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia, Ufaransa ilivamiwa na Wajerumani lakini hatimaye uliibuka na ushindi na kurudishiwa mikoa ya Alsace na Lorraine iliyokuwa imetekwa na Ujerumani katika vita vya mwaka 1870.

Baada ya vita Vikuu vya Pili vya Dunia ambapo nchi hiyo ilitekwa na Ujerumani kwa kiasi kikubwa, Ufaransa ilipata katiba mpya mnamo 1949, na kujiunga na muungano wa NATO. Mnamo 1951, taifa hilo lilijiunga na Umoja wa Ulaya.

Baada ya kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Indochina mwaka wa 1954, Ufaransa ilipaswa kukubali uhuru wa Vietnam Kaskazini, Vietnam Kusini, Laos na Kambodia.

Aidha, makoloni yake mengi katika Afrika yalipata uhuru bila vita mnamo 1960.

Katika kipindi kizima cha nchi hiyo kutafuta uhuru, Jenerali Charles de Gaulle alichaguliwa kuwa rais chini ya katiba mpya iliyoundwa 1949. Mfumo wa utawala wa katiba hiyo, ulimpa rais mamlaka makubwa. Vyama mbalimbali vilivyoendelea kutetea itikadi ya de Gaulle hata baada ya kifo chake vinaendelea kuwa mkondo muhimu katika siasa za Ufaransa na marais walichaguliwa kupitia mkondo huo kama Jaques Chirac, Nicolas Sarkozy, Francois Mitterand na Francois Hollande.

Tangu mwaka wa 1980 chama cha Front National kilianza kupata kura kikipinga uhusiano wa karibu na Umoja wa Ulaya na wahamiaji kutoka nchi za Afrika Kaskazini. Kwenye uchaguzi wa urais mwaka jana, 2017, awamu ya kwanza ilibainika kwamba wagombea wa vyama vikubwa walishindwa kupata kura nyingi. Awamu ya mwisho ya uchaguzi huo ilikuwa kati ya mgombea wa kujitegemea Emmanuel Macron ambaye aliibuka kuwa rais na Marie Le Pen wa Front National.