http://www.swahilihub.com/image/view/-/5057824/medRes/2303267/-/qx8uvc/-/figo+pic.jpg

 

Ugonjwa sugu wa figo unatibika?

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Friday, April 5  2019 at  10:29

 

Takwimu za umoja wa madaktari wa figo duniani zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi wa figo huweza kupona kwa upasuaji na kupandikizwa mapema figo zenye afya njema.

Matibabu yamegawanyika katika makundi matatu ambayo ni matibabu yasiyohusisha dawa, yanayohusisha dawa na vifaa tiba na upasuaji au upandikizaji.

Visababishi vikuu vya ugonjwa sugu wa figo ni uwapo wa shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa kisukari.

Kwa upande wa matibabu ya dawa, hakuna dawa zinazotibu moja kwa moja ila zipo zinazochangia kufifisha makali ya ugonjwa, kutibu madhara, visababishi na kuboresha utendaji kazi wa figo.

Mgonjwa atahitajika kutumia dawa za kudhibiti sukari na shinikizo la damu ambazo hazina madhara kwa figo.

Ili kupunguza madhara yaliyojitokeza mgonjwa hupewa dawa mbalimbali ikiwamo dawa za kukojoa ili kupunguza mrundikano wa maji mwilini, dawa zenye kuondoa madini ya Phosphorus na za kuongeza vitamini D mwilini ili kukabiliana na matatizo ya mifupa.

Ili kukabiliana na upungufu wa damu, mgonjwa hupewa dawa za madini chuma na za kusisimua uzalishwaji wa kichochezi cha Erythropoetin kinachochochea utengenezwaji wa chembe hai nyekundu za damu.

Kutokana na kukosekana kwa usawa wa tindikali na bezi katika damu mgonjwa hupewa dawa zenye magadi au soda (alkal) ili kurekebisha hali hiyo.

Matibabu kwa kifaa tiba kijulikanacho kama Dialysis Machine ni moja ya matibabu yanayoboresha maisha ya wagonjwa wa ugonjwa sugu wa figo, kifaa hiki ndiyo mbadala wa kazi za figo zilizoharibika.

Matibabu ya upasuaji ni kuziondoa figo zilizo na ugonjwa sugu na kupandikiza figo nyingine, upandikiziaji una matokeo mazuri kulinganisha na matibabu mengine.

Nihitimishe kwa kusema kuwa tatizo hili linatibika lakini katika hatua za awali na itategemea na hali za figo na uimara wa mwili kiafya.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu.