http://www.swahilihub.com/image/view/-/3018364/medRes/1217746/-/qw8bs2z/-/153204-01-02%25284%2529.jpg

 

Ujerumani: Taifa kitovu cha ustawi kiuchumi Ulaya

Angela Merkel

Chansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel akihutubia wanahabari katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya (EU) jijini Brussels, Ubelgiji Desemba 17, 2015. Picha/AFP 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, April 11  2018 at  09:36

Kwa Muhtasari

Ujerumani ni nchi iliyoko Ulaya ya Kati.

 

UJERUMANI ni nchi iliyoko Ulaya ya Kati.

Berlin ndiyo jiji kuu la taifa hili na Kijerumani ndiyo lugha rasmi inayozungumzwa nchini humo.

Kulingana na sensa ya 2014, taifa hilo lina zaidi ya watu 80,716,000 na kuwa na ukubwa wa kilomita 357,050. Miji ya Berlin, Hamburg, Munchen na Koln ikiwa ndiyo yenye watu wengi zaidi nchini humo, na inakadiriwa kuwa na zaidi ya milioni moja kila mji.

Ujerumani imepakana na Denmark, Poland, Jamhuri ya Czech, Austria, Uswisi, Ufaransa, Luxemburg, Ubelgiji na Uholanzi.

Aidha, ina majimbo 16; Baden-Wurttemberg, Bavaria, Berlin, Brandenburg, Bremen, Hamburg, Hesse, Mecklenburg, Saksonia ya Chini, Rhine Kaskazini, Rhine-Palatino, Saar, Saksonia, Saksonia-Anhalt, Schleswig-Holstein na Thuringia.

Taifa hili la mfumo wa shirikisho lina uchumi wenye uwezo mkubwa, ikizingatiwa huuza bidhaa nyingi nje ya nchi kushinda mataifa yote duniani. Hii ni utawala wa kupigiwa upatu, chini ya uongozi wa Kansela wake, Bi Angela Merkel aliye pia Waziri Mkuu.

Takwimu za soko la hisa 2016, zilionesha Ujerumani kwa mwaka hufanya mauzo ya bidhaa zaidi ya dola 310 bilioni nje ya nchi. Huduma mbalimbali za teknolojia mpya, zimeshikilia uchumi wake kwa asilimia 70. Kwenye asilimia hiyo, 41 hutokana na huduma za kompyuta, bidhaa za umeme na dawa. Uundaji wa magari, umeshikilia asilimia 29 huku sekta ya kilimo ikiingiza asilimia 0.9 ya mapato.

Ujerumani inatambulika duniani katika utengenezaji na uuzaji wa magari na vifaa vyake, dawa, vifaa vya stima, vyuma, mashine za viwanda, bidhaa za plastiki, miongoni mwa bidhaa nyingi nyinginezo.

Ujerumani ina ukwasi wa miti, madini kama vile potasiamu, chumvi, urania, gesi na shaba.

Aidha, maonyesho mbalimbai ya biashara duniani hufanyika Ujerumani.

Biashara

Mei 2017, Kansela Angela Merkel aliyashauri mataifa wanachama wa muungano wa EU kujizatiti katika sekta ya biashara ili uchumi wao uimarike.

Aliyataka mataifa hayo lazima yachukue jukumu la kuendeleza maendeleo yake wenyewe bila kuangalia nje ya bara hilo.

"Tunapolenga kuimarisha uhusiano mwema kati ya Uingereza na Marekani, sharti kila nchi ifanye bidii ili uchumi wake uimarike," alisema Kansela huyo.

Kauli yake ilijiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump aliponukuliwa akilalamika kuwa Ujerumani inauza magari mengi sana nchini mwake, na kusema ni biashara mbaya, jambo ambalo halikumfurahisha Kansela Merkel.

Machi 14, 2018, Kansela huyo alichaguliwa na bunge la nchi hiyo kuhudumu kwa awamu yake ya nne. Amekuwa mamlakani kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita.