Ulaji sahihi wa mlo

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Friday, April 5  2019 at  10:34

 

Huenda wewe ukawa ni mmoja kati ya watu wasiojua kuwa ulaji usiofaa ni kati ya sababu zinazochangia ugonjwa wa Kisukari. Sio wote wanaojua kuhusu ulaji sahihi na unaofaa katika kujiepusha na ugonjwa wa kisukari.

Ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko, kwa maana ya kuwa ni lazima sahani yako itawaliwe na mlo kamili wenye chakula mchanganyiko.

Umuhimu wa kula mlo wenye mchanganyiko wa aina zote tatu ya vyakula, ni kutuwezesha kupata virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini kwa wakati mmoja. Katika maisha ya kawaida ya kila siku, mlo wetu unataliwa na mchanganyiko wa aina mbili tu ya vyakula ambazo ni wanga na vyakula aina ya protini.

Vyakula aina ya wanga ni aina zote ya vyakula ambavyo vinaupa mwili nguvu na joto. Vyakula hivi vimegawanyika katika makundi mawili; wanga aina ya nafaka kama mchele, ngano,uwele, ulezi, mahindi, mtama, dengu, na wanga aina ya mizizi kama ndizi za kupika, maghimbi, mhogo, viazi vitamu, viazi vikuu na viazi mviringo, vyakula aina ya protini ambavyo kazi yake katika mwili kulinda mwili usipatwe na maradhi, ni kama maharage, njegere, karanga, mbaazi, kunde, nyama nyekundu, nyama nyeupe (kuku na samaki) mayai, maziwa, dagaa na wadudu kama kumbikumbi na senene.

Kundi lingine muhimu la chakula ni mboga za majani na matunda. Mboga na matunda vinaupa mwili kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Matunda hutengeneza virutubisho mwilini na pia kuupa mwili madini na vitamin za kutosha.

Umuhumu wa madini na vitamini zinazopatikana katika matunda, hufanya ngozi kung’aa na kuwa nyororo, huimarisha uwezo wa macho kufanya kazi yake, husaidia uyeyushaji wa chakula na umeng’enyaji wa chakula kwa haraka. Pia, kurahisisha upatikanaji wa haja kubwa na kuimarisha ufahamu. Kitu muhimu zaidi katika kupangilia ulaji wa vyakula hivi ni kuwa haishauriwi kula kiasi kikubwa cha wanga na protini kama ilivyo kawaida kwa kila mtu katika jamii zetu.

Ulaji wa aina hii unatufanya tuwe na uzito mkubwa na kupata maradhi ya Kisukari.