KINAYA: Umaskini hauna fahari, tafuta mali usife kwa sumu ya chuki!

Na DOUGLAS MUTUA

Imepakiwa - Sunday, November 12  2017 at  15:20

Kwa Muhtasari

WAJINGA – kama Mkenya wa kawaida – ndio waliwao! Naam, nimesema na kurudia hapa kwamba, walio na ugumu wa kutumia akili, au wakifanikiwa kufanya hivyo huzitumia kama kofia, huangamizwa kiholela.

 

Wala hawaombolezwi kwa maana kwa walio navyo, kina yakhe na rafiki ya binadamu anayetembea kwa miguu minne – nyakati nyingine akimtafutia mawindo - ni hali moja.

Ni kwa mintaarafu hiyo ambapo najichekea ovyo nikiwaona kina pangu pakavu tia mchuzi wakiruka juu na kushangilia kwa shangwe na vigelegele kwamba kafa mtu barabarani!

Wanaotetea umuhimu wa mali hata ikiwa haiji na furaha husema ni heri kulilia ndani ya gari chapa Mercedes Benz badala ya kulilia juu ya baiskeli au pikipiki.

Kwa muda mrefu nikidhani huo ni uzuzu tu au juhudi za mkata kujiliwaza ili angaa kusukuma siku ya dhiki ikutane na ya faraja, lakini juzi nimesita kidogo na kutafakari.

Ni heri kuishi vyema duniani, kwa wingi wa mali na uhusiano mzuri na watu, hatimaye ukafuata njia ya marahaba katika mazingira tajiri.

Kisha? Ukakutana na Muumba wako na kuwaacha kina yakhe wa chuki wakikuchukia na kukulaani huku matumbo yakiwanguruma kwa njaa.

Rafiki yangu, usidanganywe na mtu kwamba kuishi na umaskini huku ukichukia waliojaaliwa nafasi ya hali, ukaingia kaburini na chuki yako, eti utakwenda mbinguni!

Kuchukia pia ni dhambi, lakini kutajirika si dhambi. Usithubutu kuniambia Biblia Takatifu inasema ni rahisi kwa ngamia kupitia kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuingia mbinguni.

Maskini hujipa nguvu hivyo akishindwa kutajirika, akaamua kuwachukia waliojaaliwa, akasahau chuki ni tiketi ya jehanamu.

Samahani, siwi hodari wa kuhubiri nikubwagie ibada nzima hapa kwa maana leo ni Jumapili. La hasha! Nakusaidia tu kujua kwamba umaskini hauna fahari, tafuta mali upesi!

Usiyawazie haya sana, mnong’ono wangu huu umetokana na chuki inayoenea nchini kiasi cha kuwasumisha wakata wa kutupwa wanaohitaji imani yetu sote.

Unapomcheka mfu eti kwa maana jina lake linaashiria wakati wa hayati yake alikuwa adui, ilhali huna hata ithibati, kisha usingizie kwamba ulipofiwa hakulia nawe, unaugua.

Naam, maradhi mabaya ya sumu inayoitwa chuki na ambayo – kinyume na Ukimwi – hakuna aliyejituma maabarani kuyatafutia tiba; kila mwanasayansi anajua hafui dafu ng’o!

Sina muda wa kupoteza hapa, eti kukukumbusha Gavana Gakuru alikuwa na mke na watoto ambao lazima wanamlia, uwaache wamwomboleze kwa amani. Sikubembelezi!  

Nitakwambia tu ufuatilie kwenye vyombo vya habari uwaone hao unaowaita viongozi wako, ujue chuki yao haijafikia kiwango cha yako kwa maana watakwenda kuwaliwaza mjane na mayatima wa mwendazake.

Aliyetutoka na hao unaodhani unapigania ni wa tabaka moja la juu, wewe maskini wa kutupwa huwezi hata kuruhusiwa kukaribia langoni ukitaka kuhudhuria matanga yake!

Hebu shika hili iwapo umekuwa ukimwombea mabaya ‘Baba’ na Upinzani kwa jumla, yakiwapata mabaya wana wa kuwalia, kinyume nawe usio wa tabaka lao.

Endelea kuwachukia usiowafikia kimaisha, wewe pamoja na wa tabaka lako la chini maafa yakiwapateni muombolezwe na nzi, mwewe na mbwa mkoko!


mutua_muema@yahoo.com