Umilisi: Dhana ya msingi katika nadharia sarufi zalishi

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  14:06

Kwa Muhtasari

Umilisi ni ujuzi alionao mjua lugha kuhusu lugha yake.

 

UMILISI ni ujuzi alionao mjua lugha kuhusu lugha yake. Ni ujuzi lugha  uliopo katika ubongo wake.

Ujuzi huo huhusu kanuni zinazotawala lugha husika. Ujuzi huu humwezesha kutambua sentensi sahihi, zisizo sahihi na kupambanua sentensi zenye utata.

Ujuzi huo humwezesha kupuuza makosa ya kiutendaji katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, na kukatisha sentensi.

Kwa mujibu wa Chomsky, mtu anapojifunza lugha huanzia na umilisi (ujuzi) na anaendelea kudai kuwa kwa kiasi kikubwa umilisi wanaokuwa nao wazawa wa lugha moja hufanana, ndiyo inayowafanya waelewane katika mazungumzo yao kwamba mzungumzaji anasema kile anachotaka kusema na msikilizaji anaelewa kile kilichosemwa na msikilizaji.

Kulingana na (Rubanza,2003) Umilisi humwezesha mzawa wa lugha:

1.Kuijua miundo ya sentensi katika lugha yake mfano mmilisi wa lugha ya Kiswahili lazima ajue muundo wa sentensi za kiswahili kuwa unaanza na nomino ukifuatiwa na kitenzi na kuishia na kielezi.                                    

Mfano: 

Mama anazungumza na jirani

Baba amekwenda kanisani

Hivyo basi,  mmlisi wa lugha hawezi kuchanganya muundo huu wa sentensi za kiswahili kwa kusema;

Amekwenda kanisani baba.

Kulingana na muundo wa sentensi za kiswahili, muundo wa sentensi zilizopo katika mfano wa pili si sahihi kwani zimekiuka sintaksia ya lughaKiswahili.

2. Kutambua sentensi sahihi na mbazo si sahihi mfano:

Rehema ni kijana mpole (sahihi)

Mtundu mtoto ni wako (si sahihi)

3. Kutunga sentensi nyingi zenye urefu wowote.

Mfano

Dada alikuwa anataka kwenda kwa mjomba ambaye alikuja hapa nyumbani kuchukua kikombe ambacho mama alikinunua katika soko la Tandale ambalo kwa sasa limepoteza umaarufu wake tofauti na miaka ya nyuma kwa kuwa huduma nyingi za kijamii zipo maeneo mengi hivyo mtu hataweza kufunga safari kwa ajili ya kwenda huko ilhali maeneo ya nyumbani kwake kuna huduma hizo…

4. Kutambua sentensi zenye utata.

Mfano:

Mama alimpigia kaka mpira.

5. Kutambua sentensi zenye maana sawa.

Mfano;

Watoto wapo uwanjani wanacheza mpira.

Mpira unachezwa na watoto uwanjani.

6. Kutambua aina mbalimbali za sentensi katika lugha yake,

 Mfano;

Leo ni sikukuu ya mashujaa (sentensi arifu).

Njoo hapa! (sentensi amrishi)

Umenunua kalamu ngapi? (sentensi ulizi)

Kumbe umerudi! (sentensi mshangao)

Hivyo mmilisi wa lugha huweza kuelewa sentensi hizi zinataka nini.