http://www.swahilihub.com/image/view/-/5057850/medRes/2303294/-/kem7blz/-/kope+pic.jpg

 

Unajua madhara ya kope bandia?

Na Aurea Simtowe, Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, April 5  2019 at  10:41

 

Kuna msemo usemao, kiingiacho mjini si haramu. Hiyo ndiyo sababu ya baadhi ya wanawake kuiga mambo mengi hasa ya urembo hata kama mengine yanaweza kuhatarisha afya zao.

Wengi hawataki kuonekana washamba, hivyo hulazimika kubandika kope ambazo zipo za urefu tofauti.

Kope hizo hubandikwa kwa gundi yake maalumu au zile za kubandikia nywele.

Wanawake wengi wanapenda kubadika kope hizo kwasababu hubadilisha muonekano halisi wa sura ambayo huwa ya kuvutia zaidi.

Kutokana na hali hiyo, wanawake wamezichangamkia kiasi cha kunogesha uuzaji wa bidhaa hiyo, siyo tu nchini bali hata katika mataifa mbalimbali.

Watu hawa huonekana sana kufanya hivyo katika shughuli mbalimbali ikiwamo harusi na sherehe kama jando na unyago ili kumfanya mtu aonekane nadhifu na mwenye kuvutia zaidi tofauti na awali.

Mmoja wa mafundi wa kubandika kope hizo, Twaha Kitambaa anasema kwa miaka miwili ya kufanya kazi hiyo (2017-2018), biashara hiyo imezidiki kuongezeka.

Anasema alipoanza alikuwa akibandika kope watu watatu hadi wanne kwa wiki tofauti na sasa idadi hiyo kuwa ya siku moja na wakati mwingine hufika hata 10.

“Kuna aina mbili za ubandikaji, kuna ubandikaji wa kope za mkanda (pamoja) na aina ya pili ni ile ya kuzichambua na kubandika moja moja,” anasema Kitambaa.

Mbali na kubandikwa kwa aina tofauti, pia hubandikwa katika urefu wa aina tofauti kulingana na mahitaji ya mteja.

“Kuna mwingine anataka akibandika mtu asijue hapo tunamuwekea zile fupi na kuzichambua moja moja, lakini kuna wengine wanapenda ndefu sana wengine ‘size’ ya kati ni chaguo la mteja.

“Mwingine anaweza kukuambia umbandike nusu jicho yaani sehemu nyingine abaki na kope halisi hii inaweza kuwa upande wa kulia au kushoto,” anasema.

Pia, alielezea njia wanazozitumia katika kubandika kope huku akisema umahiri na umakini unahitajika kwa sababu bila kufanya hivyo mtu anaweza kuonekana kama kituko mbele za watu badala ya kuvutia au gundi inaweza kumuingia machoni.

“Kila mtu ana ‘style’ yake ya ubandikaji wengine wanachora mstari na kuufuata lakini waliozoea wanajua namna ya kuweka vizuri bila kuhangaika.

“Nikimpaka gundi ya kubandikia, nasubiri kwa sekunde tano hadi sita ndipo naweka kope ili zishike vizuri kwa kutumia mkono ikiwa ni zile za pamoja. Zile za kuchambuliwa tunatumia kifaa maalumu cha kushikia kwa sababu ni nyembamba sana ni ngumu kuzishika kwa mkono.

“Tunapobandika bei huanzia Sh5,000 hadi Sh20,000 kulingana na aina ya ubandikaji unayohitaji lakini kama unahitaji na huduma nyingine huweza kuongezeka,” anasema Kitambaa.

Ak izungumzia njia zinazotumika katika kutoa kope hizo endapo mtu akizichoka na kutaka kuwekewa mpya, anasema zipo nyingi hasa ya maji ya moto.

“Kuna njia nyingine kama mafuta au majimaji yanayoweza kulainisha ile gundi iliyotumika na kumfanya mtu atoe kwa urahisi. Pia, maji ya moto kiasi huwekwa katika kitambaa na mtu kugusisha katika kope hizo na kuzitoa,” anasema Kitambaa.

Wananchi wanasemaje?

Mmoja wa watu wanaopenda kubandika kope hizo, Anna Ibrahim anasema hulazimika kubadilisha kope hizo kila baada ya wiki ili kuendelea kuonekana nadhifu na kulinda afya ya macho.

“Kuna wakati hata hizo siku hazifiki kwa sababu zinachakaa na kuna wakati huanza kubanduka hasa zile za zinazobandikwa kwa pamoja sasa inakuwa haipendezi. Kuna wakati pia zinaweza kukaa hata wiki mbili.

“Napenda tu zinanifanya nivutie zaidi kwa sababu kope zangu halisi ni fupi sana zinaninyima uhuru pale ninapotaka kuzitengeneza,” anasema Ibrahim.

Evelyn Menas anasema ubandikaji wa kope unahitaji mtaalamu aliyebobea katika shughuli hiyo vinginevyo anaweza kukufanya uonekane kituko mbele za watu.

“Mi sipendi na wala sijawahi kufanya hivyo kwanza nahisi kama uzito katika jicho lakini pia kuna wengine huwa naona wamebandikwa badala ya kupendeza wanatutisha tu huko njiani.

“Pia, huwa nahisi kama kuna madhara katika kufanya hivyo kwa sababu wanatumia gundi kukugandisha,” anasema Menas.

Akizungumzia ubandikaji kope, Erick Sokoni anasema mwanamke anayebandika kope ni sawa na anayejaribu kuichubua ngozi halisi ya mwili wake ili aonekane mrembo bila ya kujua kuna madhara yake na hajiamini.

“Sijui ni kwanini huwa wanahangaika hivi kwa sababu naamini vyote vitakuwa na madhara hasa hizo gundi wanazotumia katika kubandika, ikitokea bahati mbaya ikaingia machoni basi nahisi inaweza kumletea madhara makubwa endapo atachelewa kupatiwa matibabu,” anasema Sokoni.

Daktari wa macho anasemaje?

Mtaalamu wa macho kutoka Ona Family Eye Center, Dk Anna Gernanus anasema yapo madhara yanayoweza kuwapata watu wanaobandika kope hasa kupoteza uwezo wa kuona baadaye.

Anasema licha ya urembo huo kushika kasi, kitu kinachowafanya watu kupata madhara ni kutoangalia athari za jambo kabla ya kuiga.

“Jicho ni kiungo kinachohitaji kupewa umakini sana katika utunzaji wake ndiyo maana hata lenyewe limejiwekea ulinzi wa kujifumba kwa haraka pale kitu kinapokaribia kuligusa.

“Hivyo unapoanza kubandika kope kwa kutumia gundi mbalimbali ambazo zimeongezewa kemikali zikiingia katika macho upo uwezekano wa kusababisha matatizo mengi hasa kuathiri sehemu ya ndani ya jicho ambayo inakufanya uone vizuri.

“Endapo itaendelea kufikiwa na kemikali hizo upo uwezekano wa kuanza kupoteza uwezo wa kuona taratibu na baadaye utashindwa au wengine huwa wanaona matokeo yake ndani ya muda mfupi,” anasema Dk Gernanus.

Akitolea mfano wa msichana mmoja aliyeathiriwa na uwekaji wa kope hizo anasema aliathirika kwa kiasi kikubwa na macho yake kumvimba kiasi cha kufanya mtu ashindwe kumuangalia mara mbili.

“Nilikutana naye katika kliniki ya macho CCBRT, amevimba sana na maumivu, mtu huwezi kumuangalia mara mbili na hiyo yote ni kutaka kuonekana mrembo mbele ya macho ya watu,” anasema Dk Gernanus.