Unayopaswa kujua kuhusu uandishi wa kuleta ufumbuzi

Ndimara Tegambwage 

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  17:08

Kwa Muhtasari

Anayefukua, kulinganisha na kuweka bayana, anakuwa anatafuta suluhisho kwa maslahi mapana ya umma

 

 

Kikawaida mtu mmojammoja huwa na changamoto au matatizo binafsi. Wakati mwingine tatizo la mtu binafsi linaweza kuwa la familia, kijiji na hata taifa. Mazingira kama haya yanahitaji uandishi wa habari wa aina yake.

Hata hivyo, mara nyingi au siku zote, kumekuwa na uandishi wa habari wa kukariri machungu, shida na matatizo ya mtu binafsi, kijiji na hata taifa. Huu ni uandishi wa kukumbushia tu shida na majanga.

Anachokifanya mwandishi wa habari “mpitanjia”, ni kutangaza shida na vilio na kuwaacha wahusika katika lindi la majuto bila fununu ya kinachoweza kufanyika kuondoa majuto.

Mwandishi anakuwa hajui, kama anaowaandika wasivyojua, kuwa mahali fulani kulikuwa na shida, changamoto au matatizo ya aina hiyo lakini yalishatatuliwa.

Sasa wito mkuu katika uandishi wa habari unaolenga kuleta ufumbuzi, ni mwandishi wa habari kuelewa fika mazingira anamofanyia kazi; kujua furaha na karaha za jamii pale alipo; na kufahamu historia ya watu na mazingira anayoripoti.

Awe anajua jamii nyingine karibu au mbali na mahali anakofanyia kazi; changamoto au matatizo yanayosibu jamii hizo na iwapo kulishakuwa na juhudi za kuyakabili na matokeo yake.

Elimu ya darasani ni muhimu kwa maandalizi, lakini pia maarifa ya kujipekulia kwa njia ya kukutana na watu wa rika na viwango tofauti vya elimu na uelewa; na kuwa katika maeneo na nchi tofauti, ni muhimu pia.

Twende kwa mifano hii. Kijiji katika wilaya moja kinaweza kuwa kinasherehekea ushindi ambao ni kuondokana na mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

Haya yalikuwa mapigano ya kugombea ardhi ya malisho na kilimo na yalishasababisha vifo vya watu 27; kuleta ulemavu kwa watu 61 na kufanya watoto kuacha kwenda shule kutokana na woga.

Katika kijiji kingine katika wilaya ya mbali bado wana tatizo hilohilo. Limekuwepo kwa miaka saba sasa. Sasa uandishi wa habari unaolenga suluhisho unataka mwandishi aliye katika kijiji chenye matatizo, atoke nje ya kijiji.

Kutoka nje ya kijiji kuna maana ya kusafiri, kusoma, kutafiti au kukutana na wenye maarifa na uzoefu – kuona vijiji vingine, ndani au nje ya nchi; kupata uelewa, kuhemea maarifa na hatimaye kuandika kwa msingi wa kuondoa majonzi na kuleta faraja na furaha.

Huku siyo kuiga; ingawa siyo vibaya kuiga. Hapa kuna mazingira tofauti yenye matatizo yaleyale; na ambako suluhisho laweza kufanana au kuwa lilelile. Anayefukua, kulinganisha na kuweka bayana, anakuwa anatafuta suluhisho kwa maslahi mapana ya umma.

Kuandika tatizo au juu ya tatizo na kukimbia, hakusaidii jamii unayoripoti. Kuonyesha tatizo lilivyo, kulilinganisha na tatizo jingine la aina hiyo mahali pengine; na kuonyesha lilivyotatuliwa, ndiko kunaongeza thamani ya uandishi.

Kwa hiyo, mwandishi wa habari za kuleta ufumbuzi, anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya uchunguzi wa jamii anayoandika juu yake na changamoto zake.

Sharti awe na uwezo wa kuona, kufikiri na kuhoji. Weka msisitizo kwenye kuhoji: Kwa nini hili liko hivi? Kwa nini liko hivi kwa muda wote huu? Liliwahi kutokea kwingine? Wapi? Lilitatuliwa vipi?

Hii ndiyo maana mwandishi wa habari za kuleta suluhisho anapaswa kuwa na upeo mpana. Hakomei kwenye mapigano na vilio vya wakulima na wafugaji.

Anaweza kutafuta pia jinsi ya kuleta suluhisho kati ya wajasiriamali wachuuzao bidhaa za mkononi na watawala wa majiji ya Dar es Salaam na Mwanza.

Mwandishi anaona jinsi “machinga” wanavyofukuzwa kwa kutumia mgambo; kunyang’anywa bidhaa zao; kushitakiwa na kuswagwa nje ya jiji kila mgeni wa taifa anapokuja kana kwamba ni uchafu.

Wapi kwingine kulikuwa na changamoto au tatizo kama hilo? Walifanya nini? Hali ikoje sasa? Watawala na watawaliwa watajifunza kutokana na upeo wa mwandishi na wale aliokutana nao katika kutafuta suluhisho.

Mifano mingine yaweza kuwa: wengine walifanikiwa vipi katika kilimo cha umwagiliaji; huduma kwa wajawazito; ujenzi wa Katiba inayozingatia uhuru wa mtu binafsi na jamii; siasa za nchi na utawala. Kwa kusoma, kupekua, kuhoji, kusafiri na kuona; mwandishi anajua kipi kilifanyika wapi na jinsi kilivyofanikishwa. Anapata pia njia mpya za ubunifu zinazoweza kutumika. Anaandika kwa shabaha ya kufungua bongo za walengwa wake ili watende na kupata ufumbuzi.