Upimaji wa VVU uanze shuleni

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Friday, April 5  2019 at  11:55

 

Baadhi ya taasisi zina kawaida ya kuwapima wafanyakazi wao virusi vya Ukimwi (VVU).

Hii ni hatua nzuri iwapo huduma hiyo inatolewa kwa lengo chanya kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Upimaji wa VVU unasaidia kuwabaini wagonjwa au waathirika, hivyo kuwapa huduma zinazotakiwa kwa mujibu wa hali zao za kiafya pamoja na kuwapangia kazi wanazoendana nazo.

Hapa namaanisha nini? Namaanisha kwamba upimaji huu wa VVU uhamashiwe kwenye taasisi za elimu nchini na uwe maalumu na wenye vigezo fulani.

Kwa mfano, kuna baadhi ya shule hususan za dini ambazo tayari zimehalalisha upimaji huu wa VVU kila baada ya muda mfupi na baada ya hapo wanafunzi wanaobainika wameathirika, wanaingizwa kwenye mpango mahususi wa kupata matibabu stahili sanjari na ushauri.

Mpango au kazi ya kupima VVU uanzie katika shule za msingi, sekondari na pia vyuoni bila kubagua dini, umma au binafsi.

Kwa haya makundi ya elimu kila mmoja atanufaika kwa namna yake kuliko kuendelea na masomo wakati mwanafunzi akiwa hajitambui kiafya.

Tukianzia shule za msingi kuna baadhi ya wanafunzi wanaozaliwa tayari wakiwa na maambukizi ya VVU na iwapo kundi hili likibainika na kuingizwa kwenye mfumo wa matibabu, itasaidia kuwapunguzia makali ya virusi na kuwa na tahadhari katika maisha.

Pia, elimu ya ushauri nasaha itatolewa dhidi yao na maisha yataendelea.

Kwa wale waliopo sekondari, mara nyingi huu ndio umri hatari kwa vijana maana wanabalehe na hivyo akili, fikra, maumbile na vyote hivyo vikiunganishwa matokeo yake yanakuwa ni kujiingiza katika uhusiano wa mapenzi.

Je, hapa wanafunzi hawa wanakuwa wako katika umri mzuri wa kufanya uamuzi sahihi wa uhusiano? Jibu ni hapana.

Ngono zembe inakuwa na hivyo kama upimaji huu wa VVU utakuwa umefanyika na kuwapata wataalamu wa masuala ya elimu nasaha na saikolojia, angalau vizazi hivi vitanusuriwa kutoka kwenye janga la VVU kwa kuwaepusha kushiriki mapenzi kabla ya ndoa.

Katika elimu ya juu, yaani vyuoni mara nyingi inatafsiriwa kuwa waliopo hapa ni watu wazima na wanatambua mbivu na mbichi. Siyo kweli.

Hapa kuna mpambano wa elimu kwa rika mbalimbali; wapo wazee wanaongeza maarifa, watu wa makamo na hata vijana wadogo.

Ni hapa ambapo utamkuta binti wa miaka 20 akitoka kimapenzi na mzee wa umri wa baba yake kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo umaskini, utashi na hata makundi yasiyo sahihi bila kujua hali zao za kiafya.

Hukohuko vyuoni ndipo utawakuta baadhi ya waathirika wa VVU wakiwaambukiza wenzao kwa makusudi kutokana na tamaa na wakati mwingine kwamba hawezi kufa pekee yake.

Lengo la kupima ni kuwatambua waathirika na kuwapa elimu nasaha ikiwemo kuwasaidia wengi kuachana na baadhi ya mienendo au tabia zinazoweza kuhatarisha maisha au afya za watu wengine.

Ushauri wangu ni kwamba, Serikali itoe mwongozo maalumu kwenye taasisi za elimu kuhusiana na VVU na vilevile ipate takwimu sahihi, na namna ya kulisaidia kundi hilo kwa kupunguza na kutokomeza VVU nchini kwa kuwa inawezekana.

Kwa mujibu wa Audrey Njelekela ambaye ni ofisa kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Mkoa wa Njombe unaongoza kwenye maambukizi ya VVU kwa asilimia 11.4, utafiti huo ni wa mwaka 2016/17.

Anasema Tanzania imeungana na dunia kutekeleza lengo la maendeleo endelevu la kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030.

Inakadiriwa kuwa 2016 kulikuwa na watu takriban 1,400,000 waliokuwa wanaishi na VVU nchini miongoni mwao walikuwapo 120,000 wenye umri wa chini ya miaka 15 na wanawake 750,000 wenye umri kuanzia miaka 15 na kuendelea.

Pia, utafiti wa viashiria vya VVU na Ukimwi kwa mwaka 2016/17 unaonyesha kwamba asilimia 52 ya watu wanaoishi na VVU wanaelewa hali yao ya maambukizi na asilimia 90 wameanza kutumia tiba ya kuongeza kinga mwilini.

Pamoja na changamoto mbalimbali katika kuwahudumia waathirika wa VVU, jamii inapaswa kusimama ili kutimiza wajibu wake kwa kundi hili, kwa kulipa kila aina ya ushirikiano na siyo kuwanyanyapaa waathirika.

Jonathan Mussa anapatikana kwa simu namba 0744-205617