Upotevu wa mazao ya wakulima udhibitiwe kuwainua wakulima

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  11:07

 

Ili taasisi yoyote iweze kujitegemea na kutoa huduma bora inahitaji vyanzo vya uhakika vya mapato. Inaweza kuwa ni kutokana na kodi, ushuru wa bidhaa au huduma, mikopo au misaada. Vyovyote iwavyo, fedha inahitajika kufanikisha mipango yake.

Kila mkoa nchini una chanzo cha uhakika cha mapato. Ipo inayozalisha kahawa, korosho, tumbaku, pamba, mkonge, alizeti na mazao ya chakula. Mikoa mingine inachimba madini ya aina tofauti. Leo tuzungumzie inayolima pamba ambayo mingi inapatikana Kanda ya Ziwa.

Kwa miaka mingi mikoa ya kanda hiyo imejengwa kwa mapato yatokanayo na uzalishaji wa pamba. Baadhi walilibatiza zao hili na kuliita ‘dhahabu nyeupe.’

Mkoa wa Shinyanga kabla ya kugawanywa na kuipata Simiyu na Shinyanga ulikuwa unazalisha asilimia 40 ya pamba yote nchini. Pamoja na kiwango kikubwa cha uzalishaji, kasi ya kupunguza umaskini na kutengeneza ajira ipo chini.

Pamoja na changamoto ya wakulima wa pamba kuzalisha bila kufuata kanuni na maelekezo, wafanyabiashara nao wameonekana kuneemeka kupitia udanganyifu wanaowafanyia wakulima.

Changamoto kubwa ya wakulima imekuwa ni kuchanganya pamba na mazao mengine ikiwemo mahindi, maharage, kunde au alizeti. Mchanganyiko wa pamba na mazao mengine unatajwa kuhatarisha afya za walaji wa mazao yaliyochanganywa kutokana na aina ya dawa zinazonyunyizwa kwenye pamba kuilinda na wadudu waharibifu.

Hata baada ya mavuno, baadhi ya wakulima wamekuwa na kawaida ya kuchanganya pamba na mchanga au maji kwa lengo la kuongeza uzito. Udanganyifu huu unapaswa kuachwa mara moja kwani hupunguza thamani na ubora wa zao hilo kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya wafanyabiashara wana utamaduni wa kununua pamba kutoka kwa wakulima kwa kutumia vipimo ambavyo havijathibitishwa na Serikali. Pia wapo wanaotumia mizani isiyo na viwango ili kumpunja mkulima jambo linalozua vita kwa kila upande kutaka kumuwahi mwenzake.

Kuviziana huku kati ya wakulima na wafanyabiashara wasio waaminifu kunasababisha kufifisha ubora na thamani ya pamba, kunazikosesha halmashauri za mikoa inayolima pamba mapato inayostahili itokanayo na ushuru wa asilimia tatu kwa kila kilo moja.

Kwa mtazamo wangu, ili kuongeza mapato yatokanayo na ushuru wa pamba, wanasiasa wanapaswa kuwaacha watendaji wa Serikali kusimamia na kutekeleza sheria, taratibu, kanuni, miongozo, maelekezo na maazimio yanayohusiana na uzalishaji wa zao hilo.

Pili, kila halmashauri iingie mkataba makini na kampuni zinazokusudia kununua pamba katika maeneo yao. Kila kampuni ipewe kibali cha kununua pamba kwa kiasi ilicholipia malipo ya awali. Kwa mfano, kampuni Y inatarajia kununua tani 20,000 kutoka halmashauri X uwe ni wajibu wa kampuni kulipia sehemu ya tani hizo kabla ya kuingia sokoni.

Baada ya kiasi kilicholipiwa kununuliwa, kampuni hiyo irudi halmashauri kuomba kibali kipya cha kununua kiasi kingine inachohitaji. Lengo ni kudhibiti takwimu za ununuzi ili kutoza ushuru halali utakaochangia kukuza mapato ya halmashauri, hivyo kuweka mipango sahihi ya kuendeleza kilimo cha zao hilo.

Suala jingine muhimu ni kila halmashauri kuwa na kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa uuzaji na ununuzi wa pamba.

Kikosi kazi hiki ni lazima kiwezeshwe kwa vifaa madhubuti yakiwamo magari na mafuta, posho za watumishi watakaoteuliwa na ni vyema kikashirikisha walinzi wa raia na mali zao hasa nyakati za usiku.

Ni vyema kikosi kazi maalumu kiwe na utaratibu wa kubadili wajumbe kila baada ya muda ili kuepuka kuzoeleka na kupunguza mianya ya rushwa. Uongozi wa halmashauri unapaswa kuwa na ratiba ambayo haitakuwa rahisi kueleweka kwa wafanyabiashara wenye nia ya kufanya ujanjaujanja.

Nne, kila halmashauri iweke katazo la usafirishaji wa pamba baada ya saa 12 jioni. Lengo ni kudhibiti magendo ambayo ni rahisi kufanyika nyakati za usiku. Vilevile, watendaji wa kata, vijiji na wataalamu wa kada mbalimbali wanapaswa kushirikishwa kwenye juhudi hizi za kuimarisha mfumo na kudhibiti upotevu wa mapato katika maeneo yao.

Kubwa zaidi kuelekea uchumi wa viwanda, kila halmashauri inayozalisha pamba ibuni kiwanda kitakachotumia malighafi ya zao hilo ili kupunguza usafirishaji wa pamba ghafi, hivyo kukuza ajira kwa vijana na kupunguza umaskini.

Pia, wadau wote washirikiane kuhakikisha pamba inazalishwa kwa wingi zaidi. Hapa, taasisi na bodi zenye dhamana ya kusambaza mbolea na viuatilifu zinapaswa kufikisha mahitaji hayo kwa wakati.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango